Search This Blog

Thursday, March 27, 2014

YANGA: UKIZEMBEA MAZOEZINI UTASUGUA BENCHI, INGIZO LA TEGETE, JAVU SABABU NI KIWANGO BORA!!


LAZIMA ukomae!.  Hukuna mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans msimu huu.

Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa `Master` ameuambia mtandao huu kuwa mabadiliko ya wachezaji yanayofanywa katika kikosi chao yanatokana na ubora wa wachezaji katika mazoezi.

“Sisi hatujali wewe ni nani. Hutuwezi kumpanga mtu kwasababu labda ana kitu fulani. Nidhamu ya mazoezi  na kuonesha kiwango ndio sababu ya kupangwa katika mechi. Mabadiliko kwetu ni kitu cha kawaida”. Alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema ingizo la Jery Tegete na Hussein Javu kwenye kikosi chao katika mechi mbili zilizopita kumetokana na kuonesha kiwango kizuri wakati wa maandalizi na si vinginevyo.
Tegete na Hussein Javu wameonesha kurudi mchezoni na kuwa mwiba mkali kwa wapinzani, huku Didier Kavumbagu aliyeonekana kuwa chaguo la kwanza akishindwa kuanza.
Aidha, Mkwasa alisema kila mdau anayefuatilia michezo ya ligi kuu, lazima anaelewa kuwa ushindani uliopo katika nafasi za juu ni mkubwa zaidi ya misimu kadhaa nyuma.

“Kila timu imejidhatiti. Kupata ushindi ni lazima ziwepo jitihada za wachezaji kitimu na binafsi. Nafasi tatu za juu zimekuwa ngumu na lazima ujipange”. Alisema Mkwasa.

Mkwasa aliongeza kuwa timu zinazokwepa kushuka daraja zimekuwa na changamoto kubwa katika ushindani, hivyo  kama timu iliyopo nafasi nzuri ikashindwa kujipanga, ni kazi ngumu kupata ushindi.

Mkwasa aliyekuwa kocha mkuu wa Ruvu Shooting mzunguko wa kwanza, alisema kuwa kwasasa wanajiandaa na mchezo wa machi 30 (Jumapili) dhidi ya MgamboJKT, kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.

“Kila mechi ni ngumu kwetu. Ndio maana vijana wetu tunawaambiwa wajiandae kwa kila kitu kitakachotokea uwanjani. Tunakutana na timu inayotoka kufungwa mabao 2-0”.

 “Tunajua hawatakubali kufungwa kwa mara pili, watahangaika sana, lakini mwisho wa siku wajue kuwa Yanga ni timu bora zaidi na kongwe, lazima wakubali kufungwa”. Alisema Mkwasa.

Mkwasa aliwashukuru mashabiki wao kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi  katika michezo yao na aliwaomba kuendelea kuwaunga mkono zaidi ili kufanikisha malengo yao ya kutwaa ubingwa.
“Mpira bila mashabiki si mpira tena. Nasema tena na tena, shukurani sana mashabiki wetu kwa kuwa karibu na timu”. Alisema Mkwasa.

Mechi ya jumapili, itakuwa mechi ngumu zaidi kwa Mgambo kwasababu kupoteza tena baada ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa Azam fc, itakuwa kujipalia mkaa.

Yanga wataingia katika mechi hiyo ya 22 msimu huu wakiwa na pointi 46 katika nafasi ya pili, huku vinara Azam fc wenye pointi 50 kileleni watakuwa na kibarua dhidi ya Simba sc uwanja wa Taifa.

Baada ya kutoka Tanga, aprili 6 mwaka huu, Yanga itacheza dhidi  ya  JKT Ruvu Uwanja wa Taifa.

Aprili 9, Yanga wataikaribisha Kagera Sugar katika dimba la Taifa jijini Dar es saalam.

Aprili 13 katika dimba la Sh. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha, Yanga watakuwa wageni wa  vibonde, JKT Oljoro.

Mechi ya mwisho kwa Yanga itakuwa aprili 19 mwaka huu ambapo watakabiliana na mahasimu wao, Simba Sc.

No comments:

Post a Comment