Search This Blog

Thursday, March 27, 2014

KAGERA SUGAR WAIKOMALIA NAFASI YA KIBADENI, WAGOMA KUWA WATANO MSIMU HUU!!

Na Baraka Mpenja,Dar es salaam

0712461976 au 0764302956

WASHINDI wa nafasi ya nne  msimu uliopita wa ligi kuu soka Tanzania bara, Kagera Sugar  wenye makazi yao  Kaitaba , Mjini Bukoba, mkoani Kagera hawajakata tamaa kuisaka nafasi ya tatu au nne msimu huu.

Murage Kabange, kocha msaidizi wa Kagera Sugar amesema kuwa katika mechi tano walizobakiza wamejiandaa kupata ushindi ili kutetea nafasi yao ya nne au kupata ya tatu.

“Mwaka jana tuliishia nafasi ya nne. Msimu huu tumekuwa na majeruhi wengi. Kikubwa kwasasa tunajipanga kuibuka na ushindi katika michezo yote iliyosalia”.

“Malengo yetu ilikuwa ni kutwaa ubingwa au kushika nafasi ya pili. Kushuka nafasi ya nne hatukutarajia. Lakini kutokana na matatizo ya kikosi chetu, sasa tunaiwinda nafasi ya tatu au kusalia nafasi ya nne kama mwaka jana”. Alisema Kabange.

Kocha huyo alisema maandalizi yao kuelekea mchezo wa jumapili dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Kaitaba yanakwenda barabara,hivyo wana matumaini ya kufanya vizuri.
“Tunanoa makali ya safu ya ushambuliaji ili kuipa makali. Pia tunarekebisha kasoro zilizopo safu  ya kiungo na ulinzi. 
Tunatarajia kufanya vizuri dhidi ya Ruvu Shooting”. Alisema Kabange.

Akizungumzia mechi tano zilizosalia, Kabange alisema wanahitaji kujiandaa kwa umakini mkubwa kwasababu kuna ushindani wa hali ya juu.

“Hukuna mechi nyepesi hata kidogo. Tunacheza na Ruvu Shooting jumapili. Baada ya hapo tutawasubiri Simba nyumbani. Mechi hizi kwanza ukiziangalia zitakuwa ngumu, lakini tunafanya maandalizi mazuri”. Aliongeza Kabange.

Mbali na mechi hizo mbili, Kagera Sugar pia wamebakiza  kiporo kimoja dhidi ya Yanga aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Baada ya mechi hiyo, watasafiri mpaka Tanga kuwavaa Mgambo JKT uwanja wa Mkwakwani aprili 13 mwaka huu.
Kibarua chao cha  mwisho ni aprili 19 dhidi ya Coastal Union uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.

Mpaka sasa, Kagera Sugar wameshuka dimbani mara 21 na kujikusanyia pointi 32 katika nafasi ya 5.

Mbele yao wapo wekundu wa Msimbazi Simba ambao wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 36 katika nafasi ya nne.

No comments:

Post a Comment