Search This Blog

Monday, March 17, 2014

RAGE ANA POINTI, SIMBA MAMBUMBUMBU.



Na Eliya Rioba.

Ninaposikia kauli za viongozi wa vilabu vyetu hapa Tanzania, huwa najiuliza maswali mengi sana. Weekend hii umefanyika mkutano wa wanachama wa Simba Sports club katika bwalo la polisi pale Oyster Bay. Katika mkutano huo, mwenyekiti wa sasa wa klabu hiyo alitoa kauli zenye utata kidogo, miongoni mwa kauli zake ilikua hivi, “Simba oyeee…. Mimi sitagombea tena katika uchaguzi ujao, sina njaa, mimi sio masikini…. Hata mkinizomea nasemaje, sina njaa wala si masikini, msiwe kama mambumbumbu”.


Kauli hizi za mwenyekiti wa klabu hii ya simba, zimeibua hoja kadhaa kichwani mwangu ambazo nazitafakari katika makala hii.

Simba Sports Club, timu iliyoanzishwa miaka ya 1930, na kuwa na wapenzi na wanachama wanaokadiriwa kufikia milioni tano (5) kwa ujumla, hadi leo inafanyia mikutano yake kwenye bwalo la polisi.


Simba Sc, miongoni mwa timu zenye umri mkubwa hapa Tanzania, (inakadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 75), ina jengo kariakoo ambalo hata kupata eneo la kuegesha gari ni taabu.

Hadi leo, timu hii iliyowahi kufika makundi ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2003, haina mkataba na kampuni yoyote ya utengenezaji wa vifaa vya michezo, kama Adidas au Nike wala kampuni yoyote kubwa, bali inategemea vifaa vya mchezo kutoka kwa wadhamini wa ligi.


Hadi leo, pesa za usajili wa wachezaji zinatoka mifukoni mwa watu wachache, na hata mauzo ya wachezaji hao hurudi kwenye akaunti zao binafsi za benki, na hakuna mwanachama mwenye uhalali wa kuhoji matumizi ya fedha hizo. 




Hizi ni baadhi ya hoja nilizonazo kichwani mwangu, ambazo zinaashiria ukweli wa kauli ya mwenyekiti wa Simba, kwamba wanachama wake ni mambumbumbu. Sina maana ya kumtukana wala kumkejeli mtu, ila nia yangu ni kuwafumbua macho wanachama wa Simba, ili kama ni kufanya mabadiliko, basi wakati ndio huu wa kuondokana na kauli za kudhalilishwa kutoka kwa viongozi wao.


Hivi Simba Sc, ni kampuni, ama taasisi, ama biashara ya watu binafsi? Kwa utaratibu uliopo kwasasa, inaashiria kwamba Simba Sc ni taasisi Fulani, inayopata udhamini kutoka kwa wadhamini wa ligi na wadhamini wa timu, ambapo ndani yake inafanyika biashara ya WATU Fulani wachache. 

Mfano mzuri ni pale mwenyekiti wa club hii alipoamua kufanya usajili wa mchezaji mmoja kutoka Zanzibar, na usajili ule ulifanyikia sebuleni kwa mwenyekiti huyu, kwa kumkabidhi kitita cha fedha, wakapiga picha, zikaenea mitandaoni. Endapo mchezaji huyu akiuzwa kwenda timu nyingine kwa kitita kirefu zaidi, ni mwanachama gani mwenye uhalali wa kuhoji matumizi ya pesa za mauzo yake? Maana hakuna mwanachama anayejua pesa za manunuzi yake zilitoka wapi, ndio maana nimesema kwamba ni biashara ya watu binafsi.


Kama Simba Sc ingekua ni kampuni, leo hii mambo yangekua tofauti. Timu ingeweza kujitegemea kiuchumi, ingekua na waajiriwa wa kudumu ambao wangeifanya timu hii kuwa biashara ya kudumu kwa faida ya wanachama na wapenzi wote kwa ujumla na si kwa watu wachache peke yake. Makampuni mbali mbali yangeweza kuwekeza kwenye timu hii kwasababu imani ya matumizi ya pesa ingekuwepo.



Soka ni mchezo wa burudani, na wala si siasa. Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na washabiki wengi wa mpira wa miguu. Mchezo huu umekua ni miongoni mwa burudani zinazopendwa na watanzania wengi nchini na nje ya nchi kwa kwa ujumla, miongoni mwao ni wanasiasa, wasanii wa burudani mbali mbali pamoja na wafanyabiashara. 

Miongoni mwa watu maarufu nchini ambao ni wapenzi wa timu ya Simba Sc ni pamoja na wasanii wa muziki wakiwemo, Professor Jay, Mwana FA, Afande Sele na wengine kibao. Kwa Wanasiasa kuna akina Mohammed Dewji, Zitto Kabwe, Professor Kapuya na wengineo. Je, ni mara ngapi watu hawa maarufu nchini wenye uwezo mkubwa wa ushawishi, wamewahi kuhudhuria mikutano ya wanachama? Kama hawajawahi kuhudhuria, umewahi kujiuliza ni kwanini? Je, unadhani hawana kadi za uanachama? Kama ni kweli hawana, jiulize ni kwanini?


Kaizer Chiefs, Orlando Pirates, TP Mazembe, na Azam Fc, ni miongoni mwa timu chache Afrika kuanzishwa baada ya club ya Simba Sc kuwepo, ambapo mafanikio ya timu hizi ni ndoto kwa timu hii ya Simba. Sio kwasababu timu hizi zilianza zikiwa na matajiri ama pesa lukuki, ila ni kwa sababu ni timu zilizoanzishwa kwa mipango madhubuti ya kiutendaji.

Hadi lini klabu kubwa kama Simba itaendelea kutawaliwa na watu kama akina Rage, wenye kauli za udhalilishaji wa wanachama wake? Kuna wakati timu ilifanya vibaya, mwenyekiti akapigiwa simu na radio moja kwa ajili ya mahojiano ili kujua chanzo cha kufanya vibaya, jibu lake likawa kwamba yeye hachezi uwanjani, hivyo hawezi kujua tatizo ni nini.



Binafsi simlaumu Rage, ila nalaumu aina ya mfumo wa utendaji kazi wa timu hii. Rage ni mbunge, na ni mfanyabiashara. Hategemei mshahara wa Simba Sc kuishi, ndio maana amesema yeye si masikini. Lakini kama Simba Sc ingekuwa ni kampuni, hakuna mwenyekiti wa kampuni yoyote duniani angeweza kuwajibu wanachama wa kampuni yake kama alivyofanya Rage. Sasa basi, ni jukumu la wanachama wa Simba Sc, kuuangalia upya mfumo wa utendaji kazi wa timu hii. Kama watapenda kuendelea kuitwa mambumbumbu, basi waendelee na aina ya mfumo uliopo, maana watabadilisha majina ya viongozi tu, utendaji utabaki vile vile. Lakini kama wanataka kuondokana na udhalilishwaji wa kauli za viongozi wao, basi ni vyema kuubadili mfumo ulipo wa utendaji kazi.

4 comments:

  1. Mmh..Mbumbumbu SC.........

    ReplyDelete
  2. hoja yako nmeipenda, mbali na ukweli kwamba timu zetu zinaendeshwa na mifumo isiyofaa ktk maendeleo ya soka lkn inaonekana rage ni mtu asiye na chembe ya ustaarabu, mara nyng mikutano yake anaendesha kibabe na dharau juu labda ni kwsbb wkt anachukuwa madaraka wanachama walikuwa na imani sana naye pengine kuliko kiongozi yeyote aliyewahi kuiongoza simba, hivi mambo anayofanya rage simba yangekuwa yanafanywa upande wa pili yaani yanga nini kingetokea kwa kiongozi kama huyo? nadhani asingevumiliwa, wanachama wa yanga wanamaamuzi kuliko simba, kauli za rage haoneshi kama mtanzania ni dhahiri anadhihirisha usomali wake kwani ni mnafiki na hafai kuwa kiongozi wa soka la kisasa, simba wache watukanwe na huyo rage wao wameyataka wenyewe, wakati wanamchagua walisema rage anafaa sana eti mzee wa FITINA sasa matusi ndio fadhila zake kwa wanasimba, kweli ni mambumbu hakuna ubishi

    ReplyDelete
  3. Hivi hilo agizo la TFF kwa klabu zote kurekebisha katiba zao ifikapo tarehe 20/3/2014 linaihusu Simba tu?mbona Yanga na klabu zingine wako kimya hakuna mkutano wala mchakato huo wa Katiba.Rage ni mjanja sana ametumia nafasi hiyo kukwepa mkutano mkuu uliokuwa unatakiwa na wanachama.Rage amecheza mpiraSimba sc na ameongoza Simba sc kwa miaka minne sasa,hivyo anawajua wanachama na washabiki wa simba kiundani,kwa hiyo anaposema ni mbumbumbu yuko sahihi kwani amewadanganya kwa miaka minne na wamemvumilia mpaka anamaliza muda wake.Ukiona hadi Kaburu anayeaminika kwa fitna amemshindwa Rage akamua kuondoka yeye kwa kujiuzulu ujue huyu jamaa ni kiboko.Angalia Malinzi aliingia kwa mbwmbwe nyingi na kumwagiza Rage aitishe mkutano mkuu ndani ya siku 14 lakini hadi leo mkutano huo haujaitishwa badala yake wamefanya mkutano wa kurekebisha katiba tu.

    ReplyDelete
  4. mzee wa saigon,kkooMarch 19, 2014 at 9:10 AM

    Hakuna mtu aliewaweza simba kama Aden,wamelazimika kumsubiri mpaka amalize muda wake wa uongozi bila kupenda sio kama loyd nchunga alivyoiachia yanga kinyonge namna ile

    ReplyDelete