Search This Blog

Wednesday, March 19, 2014

PAWASA, MWAISABULA WAIPA UZITO WA JUU MECHI YA YANGAVS AZAM LEO TAIFA, WAAMUZI CHONDE CHONDE MSISABABISHE YA MACHI 10, 2012!!

Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


INAWEZEKANA baada ya dakika 90 za mtanange wa kesho baina ya Young Africans dhidi ya Azam fc, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam,  picha ya timu gani inaweza kupewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 ikafahamika.
Mchezo wa kesho umevuta hisia za mashabiki wengi na kuwafanya makocha wa timu zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc na Hans Van Der Pluijm wa Yanga kutuliza akili zao kwa lengo la kupata ushindi mechi ya kesho.
Kitendawili kinachosubiriwa kuteguliwa ni je, Azam fc watawafunga Yanga kwa mara ya pili msimu huu katika mechi za ligi kuu?.
Ikumbukwe septemba 22 mwaka jana, timu hizi zilikutana katika mchezo wa ligi kuu na Wana Lambalamba kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Lakini kabla ya mechi hiyo, Yanga waliwafunga bao 1-0 Azam fc katika mchezo wa Ngao ya jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu 2013/2014.
Mechi zilizopita, Yanga walitoka suluhu dhidi ya Mtibwa uwanja wa Jamhuri, wakati Azam fc walishinda mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union.

Azam fc wapo kileleni wakijikusanyia pointi 43 katika mechi 19 walizocheza, wakati Yanga wameshuka dimbani mara 18 na kujikusanyia mzigo wa pointi 39 katika nafasi ya pili.
Mtandao huu ulipata nafasi ya kuzungumza na kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula `Mzazi` , lengo likiwa ni kujua mtazamo wake kuelekea mechi ya kesho.

Katika mahojiano hayo maalumu, Mwaisabula alianza kwa  kusema mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa Yanga, kwasababu wameathiriwa na matokeo ya mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
“ Kutoka suluhu na Mtibwa kutawafanya wacheze kwa nguvu kutafuta matokeo ya ushindi. Hawatakubali kufungwa au kutoka sare kwani wakipata matokeo hayo, kutawafanya wapunguze hadhi yao ya kutetea ubingwa wao”.
“Lakini Azam fc wapo kwenye reli, wapo kwenye mwendo mzuri. Wanashinda mechi zao, wanaonekana kuiandaa  timu yao vizuri. Ukizingatia haya utaona kuwa mechi ya kesho itakuwa na upinzani mkubwa”. Alisema Mwaisabula maarufu kwa jina la `Mzazi`.
Mwaisabula aliendelea kusema kuwa Azam fc wamewekeza sana kwenye timu yao, hivyo hakuna wanachohitaji msimu huu zaidi ya ubingwa.

“Azam wamechukua nafasi ya pili zaidi ya misimu miwili, mwaka huu hakuna wanachokitafuta zaidi ya Ubingwa. Naamini kesho kila timu itacheza kwa malengo ya kutafuta pointi tatu muhimu”. Aliongeza Mwaisabula.
Aidha, Mwaisabula alisema kwa namna timu hizi mbili zilivyosheheni nyota wenye gharama kubwa hategemei mizengwe ya nje ya uwanja.
“Kinachotakiwa ni mpira kuchezwa uwanjani, mambo ya nje ya uwanja,  nadhani yasiwe  na nafasi kwa sasa. Timu zimesajili kwa gharama kubwa, hakuna maana ya kumwaga fedha kwenye timu, halafu unafanya mizengwe nje ya uwanja. Binafsi sikuelewi kabisa”. Alisema.

Naye beki wa zamani wa Simba, Moro United na APR ya Rwanda, Boniface Pawasa alisema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa timu zote kwasababu itaweza kutoa nafasi ya timu yoyote kujikita kutafuta ubingwa ua kutoka katika mbio za ubingwa.
“Kisaikolojia, Yanga unaweza kusema wameathirika kidogo na kupoteza mechi dhidi ya Al Alhy katika mazingira ambayo walikuwa wanaamini kuwa wanaweza kusonga mbele. Pia hawajashinda mechi iliyopita. Sisi wataalam wa mpira tunaamni mwisho wa mechi moja ni mwanzo wa mechi nyingine. Wajipange kwa lkesho”. Alisema Pawasa.

Aidha, Pawasa alishauri upande wa tatu wa mchezo kwa maana ya waamuzi kuwa makini zaidi katika mechi hiyo muhimu kwa timu zote.
“Waamuzi lazima wachezeshe  kwa kufuata sheria 17. Mechi za mwishoni huwa waamuzi wanabeba lawama nzito, cha msingi wawe makini katika maamuzi kwasababu ni mechi kubwa itakayoamua hatima ya timu zote”. Alisema Pawasa.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa machi 10, mwaka 2012 wakati Yanga ikilala 3-1 dhidi ya Azam fc, Uwanja wa Taifa, wachezaji wa Yanga walimpiga mwamuzi wa kati Israel Mujuni Nkongo baada ya kutoridhishwa na maamuzi.

Mbali na kupigwa kwa mwamuzi, pia mashabiki wa Yanga  walifanya fujo na kuvunja viti mpaka ikawalazimu polisi kutumia nguvu kutuliza ghasia hizo.
Kutokana na hali hii kutokea, ndio maana Pawasa aliwataka waamuzi kuwa makini zaidi katika mchezo wa kesho.
Historia inaonesha kuwa klabu hizi mbili zimekutana mara 12 katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara tangu wana Lambalamba wapande daraja msimu wa 2008/2009 ambapo Yanga imeshinda mara nyingi.

Mechi 11 zilizopita za ligi kuu, Wanajangwani wameibuka na ushindi katika mechi tano,  wakati Azam fc wao wameshinda mechi nne, huku timu hizo zikichoshana nguvu katika mechi mbili.
Kwa matokeo haya ya mechi zilizopita, unaweza kuwapa Yanga nafasi ya kushinda, lakini kwenye soka kuna wakati historia haileti matokeo.
Kwasasa vikosi vyote viko imara, huku vikiwa na makocha wenye historia Tofauti.

Mabeki wa Azam fc ambao kwa asilimia kubwa wanategemewa kuwa Erasto Nyoni, Said Moradi, Gadiel Michael na Aggrey Morris  watakuwa na mtihani mwingine wa kuwazuia washambuliaji wa Yanga ambao wanaweza kuwa Emmanuel Okwi, Khamis Kiiza, Didier Kavumbagu, na Simon Msuva.
Kama Mrisho Ngassa yuko fiti na tayari kwa kuanza kesho, basi ni hatari nyingine kwa upande wa Azam fc.
Wakati mabeki wa Azam fc wakipeana shughuli na washambuliaji hao wa Yanga, nao Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Nadir Haroub Canavaro, Oscar Joshua watakuwa majaribuni kuwazuia wakali wa wana  Lambalamba, John Raphael Bocco `Adebayor`,  Kipre Herman Tchetche, Brian Umony, na kiungo mshambuliaji Himid Mao.

Langoni mwa Azam fc atakuwepo Mwadini Ali wakati Yanga anaweza kuanza Juma Kaseja kufuatia kipa namba moja, Deogratisu Munish `Dida` kuwa majeruhi.
Kwa ubora wa makipa hawa, milango ya timu zote itaweza kuwa katika mikono salama.
Vita nyingine kesho ni baina ya Haruna Niyonzima `Fabregas`, Frank Domayo (kuingo wa ulinzi) dhidi ya viungo wa Azam fc, Michael Balou na fundi, Abubakar Salum `Sure Boy`.
Hapa ufundi wa hali ya juu unategemewa kutoka kwa wapishi hawa wa dimba la kati kwa timu zote.

No comments:

Post a Comment