Search This Blog

Sunday, March 30, 2014

YANGWA YAVURUGWA 2-1 NA MGAMBO, MBEYA CITY YAINYONGA 1-0 PRISONS, MTIBWA YAINYAMAZISHA COASTAL, JKT RUVU MAMBO SAFI!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam

0712461976

HUWEZI amini!. Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara wameweka rehani nafasi yao ya kutetea taji lao msimu huu baada ya kufumuliwa bila haruma mabao 2-1 na wapambanaji wa kukwepa kushuka daraja, Mgambo JKT katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.

Yanga wakiwa na kikosi kamili gado waliingia uwanjani wakiwa na imani kubwa ya kuibuka na ushindi ili kuwasogelea Azam fc wanaozidi kutesa kileleni.

Maafande wa Mgambo walianza kushusha kirungu cha kwanza katika dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Fully Maganga.

Bao hilo  lilidumu mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamaliza.

Mbaya zaidi, Mgambo walilazimika kubaki pungufu kwa dakika 60 baada ya mchezaji wao Mohamed Neto kutolewa  nje kwa kadi nyekundu dakika ya 30 kipindi cha kwanza.

Baada ya kipindi cha pili kuanza, Yanga waliingia kwa kasi wakihitaji kupata bao la kusawazisha.

Dakika ya 50, Yanga walifanikiwa kupata penati na nahodha wake, Nadir Haroub `Canavaro` aliukwamisha mpira kimiani kwa shuti kali.

Dakika ya 69, Mgambo JKT walipata  penati  iliyokwamishwa kimiani na Malima Busungu na kuandika bao la pili kwa maafande hao wa Jeshi la kujenga Taifa.

Mpaka dakika 90 zinamalizika, Mgambo walikuwa mbele kwa mabao mawili, huku kikosi cha Hans Van Der Pluijm kikiambulia bao moja la kufutia machozi.

Mechi nyingine iliyokuwa ikiangaliwa kwa jicho la tatu ni baina ya vinara wa ligi kuu, Azam fc dhidi ya Simba SC kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Azam fc wamefanikiwa kuvuna pointi tatu muhimu baada ya kuikung`uta Simba sc mabao 2-1.

Mabao ya Azam fc yalifungwa na Hamis Mcha `Vialli` mnamo dakika ya 16 kipindi cha kwanza, lakini Simba sc walisawazisha dakika ya 45 ya kipindi hicho kupitia kwa Joseph Owino.

Azam fc waliandika bao la pili na la ushindi kupitia kwa nahodha wake, John Raphael Bocco `Adebayor` katika dakika ya 56.

Baada ya mchezo huo, afisa habari  Azam fc, Jafar Idd Maganga amesema bado wanaendelea kupambana mpaka dakika ya mwisho ili kujua kama watabeba ubingwa.

“Tunamshukuru Mungu tumeweza kucheza kadri ya uwezo wetu na kuwafunga Simba mabao 2-1. Vijana wetu wameendelea kukomaa na kuonesha kuwa wao ni bora. Ligi bado sana, tuna mechi nyingine, tutahakikisha tunashinda  zote na kujihakikishia ubinwa”. Alisema Jafar.

Kwa upande wa Simba Sc wameendelea kuwa wapole na kukubali matokeo ya uwanjani.

Afisa habari wa Simba, Asha Muhaji alisema mechi ilikuwa ngumu kwao kutokana na ubora wa Azam fc, hata hivyo timu imecheza vizuri na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.

“Mpira ndivyo ulivyo. Matokeo ya uwanjani lazima uyakubali. Wenzetu walitumia nafasi vizuri na kushinda. Tunasahau ya leo tunajiandaa na mechi ijayo”. Alisema Asha.

Mechi nyingine imepigwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ambapo wagonga nyundo, Mbeya City FC walikuwa na kibarua kizito dhidi ya Tanzania Prisons.

Ulikuwa mchezo muhimu kwa timu zote, lakini ulikuwa muhimu zaidi kwa Prisons kwasababu wapo katika hatari ya kushuka daraja.

Dakika 90 zimemalizika kwa Mbeya City Kuvuna Pointi tatu muhimu kufuatia ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo limefungwa dakika ya pili ya kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji hatari, Paul Nonga.

Afisa habari wa Mbeya City, Freddy Jackson alisema Prisons walijipanga vizuri kwa lengo la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 mzunguko wa kwanza.

“Mbeya City nafasi bado tunayo. Sisi tunafukuzia nafasi mbili za juu. Kufungwa kwa Yanga leo kwetu ni heri. Tunajipanga kushinda mechi zote. Lolote linaweza kutokeo, Kupoteza kupo”.

“Hata hao wa juu wanaweza kupoteza na ndio maana umeona Yanga wamefungwa. Mungu atapanga mwisho wa siku nani ashike nafasi hizo”. Alisema Freddy.

Tanzania Prisons kupitia kwa katibu mkuu wake, Sadick Jumbe wamekiri kuzidiwa maarifa na Mbeya City, hivyo hawana cha kulaumu zaidi ya kujipanga mechi zijazo.

“Timu ilicheza vizuri, lakini tulifungwa mapema na kuharibikiwa na mchezo. Bado tunasema, nafasi yetu ipo hata kama Mgambo wameshinda leo dhidi ya Yanga”.

“Ona maajabu ya Mpira, Yanga wametoka kutufunga mabao 5-0, leo wamefungwa 2-1 na wanyonge wenzetu. Lolote linaweza kutokea katika soka.” Alisema Jumbe.

Mechi ya Azam fc dhidi ya Simba, Mgambo na Yanga, Mbeya City dhidi ya Prisons zilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kwa mashabiki na makocha wa timu hizo zinazowania nafasi tatu za juu.

Baada ya Azam fc kushinda, wametia mguu mmoja ndani mwingine nje katika mbio za kutwaa ubingwa mwaka huu.

Sasa wameshatimiza michezo 23 kwa kujikusanyia pointi 53 kileleni, huku Yanga wakicheza mechi 22 na kuvuna pointi 46 kibindoni katika nafasi ya pili.

Matokeo ya Azam yamekuwa faraja kubwa kwa kocha Joseph Marius Omog wa Azam fc kwasababu sasa ameweka pengo la pointi 7 dhidi ya mabingwa watetezi Yanga.

Kwa maana hiyo, Yanga wameweka ubingwa wao reheni na nguvu kubwa inahitajika kuwazuia Azam fc ambao hawajafungwa mpaka sasa.

Yanga wamebakika kiporo kimoja dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, April 9mwaka huu.

Hata hivyo bado watahitaji kujipanga zaidi kwasababu matokeo yanayopatikana uwanjani kwa sasa yamekuwa ya ajabu kidogo.

Wakati wanaelekea Tanga, bila shaka walidhani wanaenda kuvuna pointi tatu muhimu mbele ya Mgambo na kila mtu alikuwa anafikiria hivyo kutokana na ubora wao na kiwango walichoonesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Prisons.

Mtandao huu jana uliwapa tahadhari Yanga kuwa wasiende kirahisi  na hii ilitokana na  maneno ya kocha msaidizi wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa aliyesema  kuwa Mgambo ni timu ndogo, hivyo watahangaika sana, lakini mwisho wa siku wajue Yanga ni timu kubwa na kongwe.

Hakuna aliyetarajia matokeo ya leo, na hii imezidi kuwapa hofu zaidi Yanga katika michezo yao iliyobaki dhidi ya Kagera Sugar, JKT Ruvu, JKT Oljoro na Simba sc.

Yanga lazima watulize akili zaidi kuhakikisha wanashinda mechi zote kama kweli wanahitaji kutetea ubingwa wao.

Nao Azam fc wamebakiwa na mechi tatu dhidi ya Ruvu Shooting, Mbeya City na JKT Ruvu.

Katika mechi hizo tatu, Mbili atasafiri kwenda mkoani Pwani na nyingine atakwenda Mbeya, baada ya hapo atamalizia nyumbani kwake Azam Complex, Chamazi.

Mbeya City baada ya ushindi wa leo, wamefikisha pointi 45,  pointi moja nyuma ya Yanga.

Hii imezidi kuwapa njia Mbeya City kuwania nafasi mbili za juu.

Kama matokeo yanayopatikana ndio haya, huwezi kutabiri kirahisi nani anaweza kutwaa ubingwa.

Nafasi ya kubeba taji ipo wazi kwa timu tatu za juu na klabu yoyote inaweza kupoteza mchezo na kujiweka mazingira magumu zaidi.

Katika mechi nyingine leo hii, Kagera Sugar wameshindwa kutamba katika dimba lake la nyumbani, Kaitaba, baada ya kulazimisha suluhu ya bila kufungana na Ruvu Shooting ya Pwani.

Pale Manungu Complex, Mtibwa Sugar wamewafumua wababe wengine wa Simba sc, Coastal Union mabao 3-1.

Nao maafande wa JKT Ruvu wameimaliza kabisa Rhino Rangers baada ya kuifunga mabao 3-1 katika dimba la Azam Complex, hivyo kuwafanya maafande hao wa Tabora kuendelea na safari yao ya kuiaga ligi kuu.

No comments:

Post a Comment