Search This Blog

Tuesday, April 1, 2014

MNYAMA SIMBA ASHIKWA PABAYA KAITABA, KAGERA SUGAR `WAKESHA` KUPIGA JALAMBA!!

Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


WAKATA Miwa wa Kagera Sugar  aprili 5 mwaka huu wanawasubiri kwa hamu kubwa katika dimba la Kaitaba,  wanyonge wa Coastal Union na Azam fc katika mechi mbili zilizopita, Wekundu wa Msimbazi, Simba sc.

Simba watasafiri kuwafuata Kagera Sugar katika mechi hiyo ya mwisho ya ugenini msimu huu, huku wakiwa wapole zaidi kwasababu hawana chao katika nafasi mbili za juu.

Kocha msaidizi wa Kagera, Murage Kabange ameuambia mtandao huu kuwa baada ya juzi  dhidi ya Ruvu Shooting ambapo walitoka suluhu ya bila kufungana, kikosi chao kipo katika hali nzuri na wameanza maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya Simba.

“Tunamshukuru Mungu kikosi chetu kimeimarika mechi hizi za mwisho. Tumesumbuliwa na majeruhi karibu msimu mzima. Mechi zilizobaki tutahakikisha tunashinda. Ilitakiwa tuanze  na Ruvu Shooting, lakini bahati haikuwa upande wetu”.

“Mchezaji wetu Salum Kanoni alikosa penati.  Ilikuwa nafasi nzuri ya kupata bao, kakini ndio Mpira”. Alisema Kabange.

Kocha huyo alisema mechi ijayo dhidi ya Simba itakuwa ngumu kwasababu Simba ni timu nzuri japokuwa imekuwa na msimu mbaya.

“Mshambuliaji Amisi Tambwe ni hatari sana. Wapo wengine ambao wana kiwango kizuri, lakini tunajiandaa kikamilifu ili kupata ushindi dhidi ya wapinzani wetu”.

 “Tunajua kwasasa hatuwezi kuchukua ubingwa wala nafasi pili. Tunapigania nafasi ya tatu au ya nne ambayo tulishika mwaka jana. Chini ya hapo si matarajio yetu hata kidogo”. Alisema Kabange.

Kabange aliongeza kuwa mashabiki wao wamekuwa wavumilivu na kuwatia moyo zaidi katika mechi zao za nyumbani, hivyo amewataka kujitokeza zaidi mechi ijayo katika dimba la Kaitaba.

Wakati Kagera Sugar wakiwa katika maandalizi kabambe, Simba wamekuwa katika hali tete baada ya kufungwa mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union na Azam fc.

Kocha mkuu wa klabu hiyo, Dravko Logarusic alikaririwa kuwa anashangazwa na matokeo ya timu hiyo, licha ya kucheza vizuri na kutengeneza nafasi za kufunga.

Loga mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa ligi imekuwa ngumu kwake kwasababu timu zote zimejiandaa vizuri.

“Huwezi kuingia uwanjani kwa kujiona ni timu kubwa. Timu ndogo zimekuwa zikioneshs upinzani mkubwa zaidi msimu huu.”.

“Nawashangaa wachezaji wengi wa kiafrika, wanapocheza na timu kubwa wanaonesha kiwango kikubwa, lakini wakikutana na timu ndogo wanacheza chini ya kiwango”. Aliwahi kutamka Loga.

Hata hivyo Simba kupitia kwa Afisa habari wake, Asha Muhaji walisema wao wanakubaliana na matokeo yanayotokea uwanjani na kilichobaki ni kufanya vizuri mechi zilizosalia ili kulinda heshima yao.

Mechi dhidi ya Kagera itakuwa ngumu kwa Simba kwasababu hata rekodi zinaonesha kuwa timu hizi zimekuwa mahasimu wakubwa tangu mwaka 2010.

Katika mechi saba walizokutana, Mnyama aliyekosa meno kwa sasa ameshinda mechi mbili, wakati Kagera wameshinda mara moja na kutoka sare mara nne.

Mechi ya mzunguko wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kufuatia Kagera kusawazisha dakika za lala salama kwa mkwaju wa penati iliyofungwa na Salum Kanon.

Bao hilo lilileta kizazaa kwa mashabiki wa Simba kwani walilipuka kwa kufanya fujo na kung`oa baadhi ya viti vya uwanja wa Taifa na kulilazimu jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi  kuwaondosha mashabiki hao uwanjani.

Sababu ya fujo hizo ilikuwa ni kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi baada ya kuwazawadia penati, `Wanankulukumbi`  Kagera Sugar.

Mpaka sasa timu hizo zipo katika nafasi tofauti kwenye msimamo wa ligi kuu msimu huu.

Simba sc wapo nafasi ya nne kwa pointi 36 baada ya kushuka dimbani mara 23.

Wakati Kagera Sugar wapo nafasi ya tano kwa pointi 33 baada ya kushuka dimbani mara 22, huku wakiwa na kiporo dhidi ya Yanga Aprili 9 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment