Search This Blog

Sunday, March 23, 2014

MNYAMA CHALI TAIFA, ABURUZWA 1-0 NA COASTAL UNION, AZAM FC CHEREKO KILELENI, RUVU SHOOTING KICHEKE, MGAMBO YABANWA NA MTIBWA SUGAR!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


MNYAMA Simba amevutwa sharubu na wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga baada ya kulala bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara, uwanja wa Taifa jijini, Dar es salaam.
Bao la Coastal Union limefungwa katika dakika 45 kipindi cha kwanza kupitia beki wa pembeni, Hamadi Juma  kufuatia mabeki wa Simba kujichanganya.
Matokeo hayo ni mwiba mkubwa kwa kocha wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic  na kujiondoa katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Hata hivyo Simba wangeambulia sare endapo mshambuliaji wake Ramadhan Singano `Messi` angekuwa makini dakika ya mwisho kabisa kwani alipoteza nafasi ya wazi akiwa yeye ni golikipa.
Katika mchezo huo, Simba walijitahidi kutengeneza nafasi hasa kipindi cha pili, lakini safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Amisi Tambwe ilikosa umakini.
Pia walionekana kutokuwa mchezoni kwa baadhi ya dakika kitu ambacho kinadhihirisha kuwa Simba wamepoteza matumaini ya kuwania ubingwa msimu huu.
Kwa matokeo ya leo,Simba sc inaendelea kuwa katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 36 kibindoni.
Coastal Union sasa wanafikisha pointi 29, lakini bado wanaendelea kusalia nafasi ya 7.
Baada ya mechi ya leo, Afisa habari wa Simba, Asha Muhaji ameuambia mtandao huu kuwa matokeo ya leo yamewaumiza zaidi kwani walitegemea kupata ushindi.
“Tumeyapokea matokeo kwa maumivu. Hatutegemea kupoteza mechi. Tulipata nafasi za kufunga, lakini wachezaji wetu walishindwa kuzitumia. Cha msingi tunaangalia mechi zijazo”. Alisema Asha.
Asha aliongeza kuwa mashabiki wa Simba sc wasikate tamaa kwasababu mechi bado zipo na kocha wao Dravko Logarusic anaenda kufanyia marekebisho kikosi chake.
“Matokeo yamelishitua benchi la ufundi. Lazima wakae chini kurekebisha makosa. Mashabiki wasivunjike moyo. Mpira huwa una matokeo ya aina tatu. Kufunga, kufungwa na kutoa sare au suluhu. Tukubali matokeo na kujipanga upya”. Alisema Asha.
Wakati Asha akisikitishwa na matokeo hayo, msemaji wa Coastal Union, Hafidh Kido alisema kikosi chao kilifanya kazi nzuri na kuibuka na ushindi mnono.
“Kocha Yufus Chipo amekibadili kikosi chake ili kupata matokeo. Amewatumia vijana wadogo zaidi. Hakika mipango yake umetimia. Tumepata ushindi huu ambao ni dalili nzuri ya kufanya vizuri mechi zijazo. Tunawaambia mashabiki wetu kuwa mechi zilizosalia ni ushindi tu”. Alisema Kido.
Huku Azam Complex, Azam fc walikuwa wenyeji wa JKT Oljoro ambapo dakika 90 zimemalizika kwa Azam fc kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Afisa habari wa Azam fc, Jafar Idd Maganga ameuambia mtandao huu  kuwa matokeo ya leo yanazidi kuwapa moyo katika harakati zao za kuwania ubingwa.
“Ni mechi ya 21 bila kupoteza. Tunazidi kukaa kileleni kwa pointi 47. Sasa tunajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Mgambo JKT Kule Tanga. Mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na mazingira ya wapinzani wetu kwani wanataka kukwepa kushuka daraja”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa msimu huu hakuna wanachohitaji zaidi ya ubingwa.
Mechi nyingine ilikuwa katika dimba la Mlandizi, Mabatini mkoani Pwani ambapo Ruvu shooting waliwakaribisha wauza mitumba wa Ilala na wenyeji wakishinda kwa mabao 2-0.
Mabao ya Ruvu Shootimg yamefungwa katika dakika ya 6 na 63 kupitia kwa mshambuliaji hatari, Elias maguri.
Masau Bwire , msemaji wa Ruvu Shooting ameuambia mtandao huu kutoka Mabatini kuwa mechi ya leo ilikuwa nzuri zaidi kwa upande wao.
“Ashanti walikuja kwa kasi wakitaka pointi tatu, lakini tuliwatuliza na kucheza soka safi, hatimaye kuwafunga. Hapa Mlandizi ni chereko chereko tu. Sasa mipango ni kushinda mechi zijazo na kuwaonesha watanzania kuwa Ruvu Shooting ni timu ya hatari”. Alisema Masau.
Huko Tanga katika dimba la CCM Mkwakwani, Magambo JKT waliwakaribisha Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
Dakika 90 zimemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban Dihimba alisema mechi hiyo ilikuwa nzuri kwao, lakini washambuliaji wao walikuwa wanashindwa kutulia kila wanapofika eneo la hatari.
“Sasa tunahamishia nguvu katika mchezo ujao dhidi ya Azam fc. Ya leo yamepita. Tunaweka mikakati mizuri ya kuwafunga Azam. Tunafahamu itakuwa mechi ngumu, lakini mashabiki wetu waamini kuwa tumejiandaa kwa mechi zote zilizosalia”. Alisema Moka.
Naye msemaji wa Mtibwa Sugar, Tobias Kifaru alisema kilichobaki kwao ni kutafuta njia ya kubakikia ligi kuu.
“Ligi imekuwa ngumu kwetu. Tumekubali yanayotokeo. Sasa tunapigania kubaki ili tujipange kwa msimu ujao. Mashabiki lazima wakubali kuwa timu zimejipanga zaidi msimu huu”. Alisema Kifaru.

1 comment: