Search This Blog

Thursday, March 27, 2014

MAKINDA WA KANDANDA BONGO KUMBUKENI KUNA MAISHA MENGINE BAADA YA SOKA, JIPANGENI SAWA SAWA!!



Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

0712461976 au 0764302956
KATIKA uumbaji wa Mungu alimfanya binadamu apitie hatua kuu tatu ambazo ni utoto, ujana  na uzee,  hatimaye kurudi mavumbini.
Kimsingi hatua ambayo hutengeneza maisha ya mtu ni Ujana. Ukifanya makosa wakati mwili wako unaruhusu kufanya kazi na una nguvu za kutosha, basi utaaisoma namba wakati wa fainali uzeeni.
Upo msemo usemao `Chezea ujana, fainali uzeeni`. Hakika maneno haya si mepesi hata kidogo kama kweli unajua kutafakari kwa umakini.
Ujana ndio kila kitu kwa maisha ya baadaye. Ni muda ambao unaweza kusuka au kunyoa.
Kuna misemo ya vijana wengi ukipita mitaani. Mojawapo ni `tumia pesa ikuzoee`. `Ponda raha maisha yenyewe mafupi`.
Misemo hii ni rahisi kuitamka na ukiwa mzembe wa kufikiria unaweza kuiamini kirahisi na kuvurugwa  katika maisha yako ya baadaye.
Sina tatizo na matumizi ya fedha kwa mtu, lazima pesa itumike. Lakini kivipi  na katika mipango ipi?, hapo ndipo hoja inapokuja.
Unapokuwa na pesa hakika inashawishi sana kuponda raha. Siku ikikata na ukakosa kabisa, utakumbuka mpaka mia moja uliyotumia.
Soka la Tanzania kwasasa limeanza kutawaliwa na vijana wadogo ambao wanapata pesa nyingi.
Kupokea pesa nyingi  katika umri wao wa miaka 18, 19, 20, 21 na 22 ni jambo la faraja sana.
Hii inadhihirisha kuwa mpira sasa ni biashara na ajira nzuri kwa Watanzania.
Kuwa na kipaji cha soka, imegeuka lulu kwa maisha ya vijana wengi na familia zao.
Nafahamu kuwa vijana wanaocheza soka katika klabu kubwa za Simba sc, Yanga, Azam fc na nyingine wanapata pesa nzuri kulingana na mazingira ya klabu hizi.
Wengine wanacheza soka la kulipwa mfano Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto.
Pengine wapo wengi walionufaika na soka la kulipwa, lakini sasa wapo Tanzania. Na wengine wanaendelea kupambana nchi za watu.
Siwakatazi vijana kutumia pesa watakavyo kwasababu ni zao na wanazitolewa jasho uwanjani.
Lakini kuwakumbushani kuwa yapo maisha mengine baadaye baada ya soka ni jukumu la msingi.
Kila jambo lina wakati wake.  Kuna muda umri unakurusu kucheza soka, ila itafika muda mpira utakwisha.
Haijalishi utaishaje, muhimu utambue kuwa utakwisha na utarudi katika maisha ya kawaida.
Ukisharudi mtaani na kuachana na ajira yako ya soka kwani huwezi tena kung`ara, ndipo utagundua misemo ya `tumia pesa ikuzoee`, `ponda raha maisha yenyewe mafupi` , haina maana kwa mtu mwenye malengo.
Vijana mnaopata pesa kwenye mpira, jaribuni kuwa wastaarabu na matumizi yenu na kupunguza mambo yasiyo ya msingi.
Pesa unayopata  leo, kesho inaweza ikatoweka. Kama hukuwekeza hata sehemu moja, utaishia kuwakimbia watu wakiwemo waandishi wa habari.
Ukikutana na  wachezaji wengi waliocheza soka miaka ya nyuma hapa Tanzania, wengi wao mambo yao si mazuri kiuchumi.
Sina haja ya kuwataja, lakini bila shaka hata wewe msomaji ulishawahi kuwaona wakihangaika katika maisha ya mtaani.
Najua kuwa soka la miaka 10 iliyopita lilikuwa halilipi kama la miaka ya leo. Kumekuwa na mabadiliko kimaslahi hata wakongwe wa soka wanakiri hili.
Ni jambo jema ninapokutana na mchezaji wa zamani akiwa anaendesha mambo yake vizuri na hana shida za hapa na pale.
Nafurahi zaidi ninaposimuliwa maisha ya nyuma na namna ambavyo mchezaji huyo alikuwa anajipanga kwa maisha mengine baada ya soka.
Wapo walioanzisha miradi mikubwa baada ya soka. Wengine walijenga nyumba na kurudi shule baada ya maisha ya mpira kufikia kikomo.
Ukipita katika ofisi mbalimbali utakutana na baadhi ya wachezaji wa zamani wakifanya kazi kwasababu walimalizia nguvu zao kwenye masomo.
Wengine hawakuendelea kusoma, lakini mambo yao yamebakia kuwa safi kutokana na mipango yao wakati wakiwa na nguvu.
Kulingana na uhalisia niuonao kwa wakongwe wa soka, napata cha kuandika kwa vijana hawa wanaosifika kwasasa katika medani ya soka.
Kusikilizia busara za wakubwa huwa kunamjenga mtu. Wazee wengi wanawashauri vijana hawa kujipanga kwa maisha ya baadaye.
Soka huwa linaisha kwa aina yake. Unaweza kushuka kiwango na kuachwa kwa aibu na klabu unayoona umefika katika maisha yako.
Pia kumbuka unatumia viungo vya mwili. Hatuombei yatokee, lakini huwa yapo. Unaweza kuvunjika mguu na usirudi tena uwanjani kwa kiwango chako.
Hapo ndipo tatizo linapoanzia kama ulikuwa unaponda raha bila kuwa na malengo.
Wachezaji wetu  mlio na vipaji vya soka, tambueni kuwa yapo maisha mengine baadaye.
Kama unahamu ya kusoma, soka lisiwe kikwazo kwako. Endelea kupiga kitabu kwani kuna watu wamesoma  sana huku wakicheza soka.
Wengine walisoma baada ya kumaliza soka. Waliweza kujilipia gharama za shule kwasababu waliwekeza kidogo walichopata.
Itakuwa mbaya sana utakapokuwa unazunguka mtaani ukiwaeleza kuwa !aaah` sema basi tu!ningekuwa na hela ningerudi shule!
Watu watakupa pole tu na kukupotezea. Cha msingi ujue kuwa maisha mengine yanakusubiri.
Chonde chonde vijana wetu mnaocheza soka. Maisha sio kuwa na gari la kubebea warembo kwa sifa na tambo nyingi mtaani kueleka katika kumbi za starehe. Eti kwasababu tu wewe ni nyota wa Simba, Yanga au Azam fc.
Umiza kichwa sana na pangilia maisha yako. Jijange kwa maisha ya baadaye ili uje kuwa na heshima.
Siku moja ukija kutoa tuzo za wanamichezo bora wa TASWA kwa heshima ya mchezaji mstaafu, huku mambo yako yakionekana  kuwa safi na unapendeza, jamii yako itakuheshimu na kuthamini mchango wako.
Lakini ukizembea, mwisho wa siku utakimbia mjini na utawakimbia watu wakiwemo wanahabari wanaotaka kujua mambo yako.
Utawaita majina mengi tu, mara wanafiki, mara watu wa majungu, kumbe hayo ulijitakiwa mwenyewe.
Someni nyakati. Tumieni nguvu zenu kuwekeza kwa maisha ya baadaye.
Nawatakieni kila la heri katika maisha yenu ya soka…

No comments:

Post a Comment