Search This Blog

Tuesday, March 4, 2014

KWANINI SIMBA SC ILIWEZA KUIVUA UBINGWA ZAMALEK 2003 KATIKA ARDHI YAO?

Wakati zikiwa zimebakia takribani siku tano kabla ya wawakilishi wa Tanzania bara katika michuano ya kombe la CAF Champions League - Dar Young Africans kuwavaa mabingwa watetezi Al Ahly katika dimba la Cairo Stadium uliopo ndani ya mji mkuu wa Misri, Cairo, mtandao huu utakuwa unakuletea namna gani klabu ya Simba - mahasimu wa Yanga walivyoweza kuvunja rekodi na kuivua ubingwa Zamalek.
Simba walishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam, Yanga nao pia wameshinda 1-0 dhidi ya wapinzania wao. Kinadharia inaonekana Yanga wana nafasi ya kuvuka kwenda hatua ya mbele kwa sababu tayari wameshapata ushindi nyumbani, ingawa rekodi yao katika viwanja vya timu za kiarabu sio nzuri. Ila pamoja na haya Yanga bado wanaweza kuiondoa kwenye michuano Al Ahly. Simba waliweza hata pia Yanga inaweza, ila kwa mbinu gani. Swali ni kwa namna gani wataweza kupata matokeo chanya jumapili ijayo dhidi ya Al Ahly.
 Mtandao huu unakuletea mahojiano na katibu mkuu wa zamani wa Simba Kassim Dewji, akielezea namna ambavyo Simba na watanzania kwa umoja wao walivyoiwezesha klabu hiyo ya msimbazi kuvunja rekodi na kuitoa Zamalek ndani ya ardhi yao.
 Friends Of Simba wakiwa jijini Cairo..

SAFARI - KUTOKA DAR TO CAIRO
"Kwa kawaida kwa wakati huo ndege inapotoka Dar hupitia Nairobi kisha Khartoum then Cairo. Kwenye ndege tulikuwa viongozi, wachezaji pamoja na wazee wa kamati ya ufundi. Mzee mmoja wa kamati ya ufundi alituambia lazima ili vitu vikae sawa lazima tufike Cairo kwenye muda aliotupangia, sisi kama viongozi tulishajua kwamba suala lile halitowezekana kwa sababu ndege lazima ingepita Khartoum - Sudan kwanza hivyo tusingefika Cairo muda aliotaka, tulipomwambia hivyo akasema tumuachie yeye atajua cha kufanya na tungefika Cairo muda uliotakiwa.
"Tulipokuwa tunakaribia Khartoum, pilot alipokuwa akifanya mawasiliano na wenzake uwanja wa ndege wa Khartoum akaambiwa hali ya hewa ni mbaya sana, mpaka tunafika Khartoum pilot alishindwa kuuona hata uwanja wenyewe na hivyo ikamlazimu kupeleka ndege moja kwa moja mpaka Cairo na tukafika muda ule ule aliotaka yule mtaalam."
 Aliyekuwa kocha wa Simba Aggrey Siang'a

MAANDALIZI - HOTEL - BASI LA TIMU
"Tangu tunafika kule wote tulikuwa tunajua hila na karaha za wapinzani wetu hivyo tulijidhatiti kukabiliana na hali yoyote ya kutoodhofisha. Uwanja ndege tuliposhuka kwa sababu kuna wenzetu walikuwa wameshatangulia hivyo walikagua basi tuliondaliwa na kulisafisha kwa kila namna kuhakikisha lilikuwa na usalama. Tuliondoka na kuelekea kwenye hoteli waliyotuandalia.
HOTELINI - CHAKULA
"Tulipofika hotelini tukavifanyia uchunguzi vyumba vyote, tukaridhika tukawaruhusu wachezaji waingie vyumbani. Vyakula vya wachezaji tulikuwa tunapika wenyewe na vyakula vya hotelini tulikuwa tunakula viongozi, wadau na mashabiki tulioenda nao Misri. 
"Wakati tunajiandaa kulala wachezaji wote wakiwa wameshaingia vyumbani kwao, mie nikiwa chumbani kwangu nikawasha TV nikakuta zimeongezwa TV stations kadhaa zinaonyesha filamu za ngono. Nilipoona vile nikajaribu kuanza kupiga simu kwenye kila chumba, nikashangaa kuona simu inapokelewa mara 1, hivyo nikagundua wachezaji walikuwa macho wanaangalia ule ujinga, na muda huo ilikuwa saa 7 usiku. Baada ya kugundua hilo jambo niliwafuata viongozi wenzangu tuliokwenda nao na tukajadili lile suala na kuona lilikuwa limefanyika kusudi na uongozi wa hoteli ili kuwafanya wachezaji wasilale mapema na kuwahamasisha kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu, ukizingatia kwenye ile hoteli juu kabisa na chini kwenye basement kulikuwa na kumbi za starehe hivyo walikuwepo madada poa. 
 Aliyekuwa katibu mkuu wa Simba Kassim Dewji

"Hivyo tulikubaliana na viongozi wenzangu kwamba tuhame hotel ili kuepeukana na mambo yale. Zamalek walipokuja Dar tuliingia contract ya kuwapa hotel waitakayo hapa Dar na wenyewe kutupa hotel tutakayotaka kule Cairo. Hivyo nasi tulipokuwa hatujaridhika na hotel waliyotupa tuliwataarifu na mwanzoni waligoma kubadilisha, lakini kwa sababu mkataba ulikuwa unawabana, ikabidi wakubali kutubadilishia. 
"Wachezaji wote wakahama pale hoteli na baadhi ya viongozi, wakaenda kukaa kwenye apartments. Viongozi na mashabiki wengine walibakia pale hotelini. Uzuri wa kuhamia kule kwenye apartments, ambazo kila moja ilikuwa na vyumba vitatu - ilikuwa rahisi kuwasimamia wachezaji. Kwenye apartment walikaa wachezaji wawili na kiongozi mmoja. Vyakula tuliendelea kupika wenyewe.
KUKATAA OFA YA SHOPPING NA KUPELEKWA KUONA PYRAMID
"Zamalek walikuwa na kila aina ya mbinu katika kuhakikisha wanawatoa wachezaji katika kuweka umakini kwenye mchezo. Walikuja na kutueleza kwamba watupeleke shopping tukawajibu kwamba hatukuwa na fedha za kufanya shopping, wakatupa ofa ya kumfanyia shopping kila mmoja wetu. Tukawaambie tungekwenda lakini kwa sasa concentration yetu ilikuwa kwenye kujiandaa na mechi. Pia walitupa ofa ya kutupeleka kuona Pyramid, tukawapa ahadi ya kwenda siku kadhaa mbele.
"Siku moja kabla ya mechi wakati tukitoka mazoezini dereva wa basi akaanza kutupeleka kwenye shopping mall, tulipostukia tukalamzisha apeleke gari hotelini.
ULINZI NA USHIRIKIANO
"Moja ya vitu vilivyochangia kwa asilimia fulani kuweza kuwatoa Zamalek ulikuwa ni ushirikiano wa Simba kama timu, taasisi, wadau wa soka, na watanzania kwa ujumla. Viongozi wote tulienda, Friends of Simba almost wote walikuwa kule, watanzania wengine ambao sio washabiki wa Simba kama akina Dr Ramadhan Dau (Pan African), Godfrey na Joseph Kusaga nao walijumuika nasi kule Cairo kuhakikisha ushindi unarudi Tanzania.
"Mdhamini wetu mkuu kupitia kampuni ya Mohamed Enterprises, Mohamed Dewji alikuwa nasi bega kwa bega siku zote tulizokuwa Cairo. 
"Tulikuwa tunagawana zamu za kulinda kila kitu, wakati wa mazoezi viongozi wengine tulienda na timu, wengine walibaki kuhakikisha kuna usalama katika vyumba tulivyofikia.
"Waziri wa michezo wakati huo Juma Kapuya na wazira yake kwa ujumla walitupa ushirikiano wote tuliohitaji." 
SIKU YA MECHI - UWANJANI
"Siku ya mechi kabla hatujaondoka hotelini tuliongea na wachezaji kuwapa moyo na kuwaweka sawa kisaikolojia. Mdhamini wetu Mohamed Dewji alitoa ahadi ya kiasi cha fedha kizuri kwa wachezaji endapo wangeshinda. Hivyo wachezaji walikuwa na kila aina ya sapoti waliyohitaji. Watanzania kadhaa nyumbani na kule ugenini walikuwa wakituombea dua na kheri ya ushindi.
"Tuliwahi kufika uwanjani masaa matatu kabla ya mchezo kuanza, lakini hatukuingia vyumbani. Viongozi kwa kushirikiana na wadau wengine tulienda kukagua dressing room, tulipiga deki na kuhakikisha hakukuwa na mchezo wowote mchafu uliofanyika dhidi yetu. 
"Tuliingia vyumbani wakati wa kwenda kukaguliwa tu na refa kwa sababu ilikuwa ni sheria, lakini wakati huo tulikuwa tumeshajiridhisha chumba kilikuwa kisafi. Wakati tunaelekea uwanjani, Crescentus Magori aliamua kubaki chumbani ili kulinda Zamalek wasije kufanya michezo yao ya kupuliza madawa ndani ya vyumba ambayo huwachosha wachezaji, Magori alikaa mpaka tuliporudi mapumziko. Kipindi cha pili ndio tukaenda nae uwanjani kwa sababu Zamalek wasingeweza kufanya chochote kwa kuwa hatukuwa tunarudi tena uwanjani baada ya kipindi cha pili."
UBORA WA TIMU
"Hayo yote tuliyoyafanya yalikuwa asilimia 20 tu, asilimia 80 zilizobaki zilibaki uwanjani kwa wachezaji. Kwa hakika Simba ilikuwa na timu bora, kocha bora na uongozi bora. Siang'a alikuwa kocha mshindani ambaye hakupenda kufungwa, kwa ushirikiano wetu sote ndio maana tukafanikiwa. 
"Wachezaji walijituma sana pamoja na vitendo vya refa lakini hawakukata tamaa walijitahidi na kufanikisha kazi iliyowapeleka uwanjani.
USHAURI KWA YANGA
"Yanga wana timu nzuri, wanachopaswa kujituma na kupanga vizuri. Lazima kuwe na ushirikiano mkubwa ndani ya timu, kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki kwa kushirikiana na watanzania wote pasipo kujali itikadi za timu.
"Serikali pia inabidi nayo iwape ushirikiano mkubwa Yanga. Viongozi waache kutafuta sifa binafsi, umoja ni kitu muhimu, timu inapofanya vizuri kila mtu atapata sifa yake."


2 comments:

  1. yanga wana timu nzuri lkn nna wasiwasi na beki yao hasa katikati maana kuna mechi wanacheza vizuri kuna mechi beki inakatika na ushauri mmepewa na kassim ufanyieni kazi

    ReplyDelete
  2. Simba ilikuwa na mgeni mmoja tu kwenye first 11. Yanga inao 5.soka letu linazama

    ReplyDelete