Search This Blog

Friday, March 28, 2014

KUELEKEA DAR ES SALAAM DERBY: SIMBA TUMPELEKE DALALI NA MO INDIA ILI KUIKOMBOA TIMU YETU


Unamfahamu mtu anaitwa Mohamed Dewji aka "MO"? Na vipi huyu anaeitwa Hassan Dalali aka "FIELD MARSHAL" je, unamfahamu? Bila shaka jibu ni ndio. Basi tunachotakiwa kukifanya wanachama wa Simba ifikapo May 4 ni kuwapandisha ndege hawa jamaa na kuwapeleka India, kule ambapo kuna madaktari bingwa wa upasuaji. Tuwape kazi jopo la madaktari bingwa wa upasuaji ya kumpasua Mo kichwa na kuchukua akili zake kisha wakazihamishia kwa Hassan Dalali, au wampasue Field Marshal Hassan Dalali kifua na kuchukua moyo wake na kuuhamishia ktk kifua cha Mohamed Dewji, kisha tupate mtu mmoja mwenye akili za Mo na moyo wa Dalali, atakaetuongoza ktk kipindi cha miaka minne ijayo. Unajua kwanini tunapaswa kufanya hivi?

Unaikumbuka Simba iliyokuwa chini ya udhamini wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited? Simba ile iliyokuwa inavaa jezi zilizoandikwa METL kifuani, mwanzoni kabisa mwa miaka ya 2000? Hii ndio Simba bora kabisa niliyowahi kuishuhudia mimi ktk maisha yangu. 
Ilikuwa Simba hatari zaidi kuwahi kutokea kuacha ile ya akina Masatu mwanzoni mwa miaka ya tisini wakati huo nikiwa kinda na akili ndio zinaanza kutambua soka ni kitu gani. 

Simba hii iliyokuwa chini ya Mohamed Enterprises ilikuwa balaa, hapa bongo ilipewa jina la "SIMBA DOZI" maana ilikuwa mtu akipona sana ni 3 na ndio Simba iliyotingisha Africa baada ya kuiadabisha Zamalek nyumbani kwao na kuwavua ubingwa wa klabu bingwa Africa, ktk wakati ambao fitna za kiarabu ndio zilikuwa ktk kiwango cha juu kabisa. 

Pesa na akili za Mohammed Dewji zilikuwa zikitumika vyema wakati ule lkn mmiliki huyu wa kampuni ya METL hakuridhika na hali ya timu nje ya uwanja, alitaka timu iondokane na mfumo tegemezi wa ufadhili na badala yake timu iwe na uwezo wa kujiendesha yenyewe na kuwa na mipango endelevu kama program nzuri za vijana na kuwa na vitega uchumi pamoja na uwanja. Lkn wapuuzi wachache wasiokuwa na akili waliokuwa ktk system walimpinga kwa nguvu zote. 
Jamaa alikasirika kuona watu hawana mwelekeo na wanapinga mipango mizuri ya maendeleo, hatimaye akaamua kuondoka zake na kuwaacha na mauzauza yao. Huwezi amini ila ni ukweli usiopingika kuwa tangu kuondoka kwa Mohamed Dewji pale Simba, timu ilipoteza mwelekeo na mpaka leo bado tunahangaika tu na hakuna cha maana.

Hapo katikati kabla ya kuja mwanasiasa Ismail Aden Rage takribani miaka minne iliyopita, alipita mzee wangu 'Field Marshal' Hassan Dalali. Huyu mzee hakufanikiwa sana lakini walau afadhali kuliko wote waliopita baada ya Mo kuondoka na bora zaidi ya huyu mwanasiasa anaejiita msomi lakini ndio katuvurugia kabisa timu yetu. Chini ya mzee Dalali umoja wa wanamsimbazi uliopotea kwa muda mrefu ulirejea na tukasahau kabisa misuguano ya kipuuzi ya wenyewe kwa wenyewe. Ndani ya uwanja timu haikuwa mbaya sana hatukufungwa hovyohovyo kama ilivyo sasa, na ktk miaka minne ya Dalali hakuna mwaka tuliokosa kikombe na miaka yote ya Dalali tulikuwemo katika mashindano ya kimataifa. Ila mzee wangu Hassan Dalali alifeli sana katika maendeleo ya timu nje ya uwanja.

Uchaguzi unaokuja Simba tunakiwa tumpate mtu mwenye akili za Mohammed Dewji na moyo wa Hassan Dalali ili timu yetu ipige hatua na kuwa na maendeleo nje na ndani ya uwanja. Kiukweli hatuhitaji tena mwanasiasa na wala hatuhitaji mtu mwenye fedha kuiongoza Simba, bali mwenye akili za maendeleo kama alivyo "MO' na mwenye moyo wa kuitumikia club na kuleta umoja miongoni mwetu kama alivyo "FIELD MARSHAL". Na hii ndio sababu ya kuwapeleka India watu hawa ili wakaunganishwe na tupate mtu mmoja aliekamilika atakaetupeleka ktk kilele cha mafanikio.

Severin Machila Mwanakijiji

No comments:

Post a Comment