Search This Blog

Tuesday, February 18, 2014

SAKATA LA OKWI LAMPELEKA MFANYAKAZI WA TFF KWENYE KAMATI YA MAADILI KWA UDANGANYIFU,

WATANO WALALAMIKIWA KAMATI YA MAADILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili wa waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi.

Riziki Majala na Army Sentimea ambao ni wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni waamuzi wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha taratibu.

Naye Sabri Mtulla analalamikiwa na TFF kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.

Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo.

TWIGA STARS, ZAMBIA KUCHEZA MACHI 2
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) itachezwa Machi 2 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Twiga Stars tayari imeingia kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.

Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.

Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.

Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.

STAND UNITED YAIKATIA RUFANI KANEMBWA JKT
Stand United ya Shinyanga imekata rufani Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikipinga Kanembwa JKT ya Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo kwenye mechi ya kiporo iliyozikutanisha timu hizo.

Mechi hiyo namba 22 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ilichezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika rufani yake, Stand United inadai kwenye mechi hiyo Kanembwa JKT ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika dirisha kidogo kinyume na maelekezo kutoka TFF kwa timu hizo kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo hawawezi kucheza mechi hiyo.

Wachezaji wanaodaiwa kusajiliwa dirisha dogo na kucheza mechi hiyo ni Hamidu Juma, Ibrahim Shaban Issa, Joseph Mlary, Lucas Charles Karanga, Raji Ismail, Salvatory Kulia Raphael, Seif Ibrahim Zaid na Yonathan David Sabugowiga.

Dirisha dogo lilifunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani yake inaombwa ipewe pointi tatu na mabao matatu kwa Kanembwa JKT kuchezesha wachezaji wasiostahili.

Awali mechi hiyo ilichezwa Novemba 2 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, na kuvunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada ya Kanembwa JKT kugomea pigo la penalti dhidi yao.

RAIS MALINZI AENDA KUJITAMBUSHA CAF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameondoka leo (Februari 17 mwaka huu) kwenye Cairo, Misri kujitambulisha kwa uongozi wa juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Akiwa Cairo, Rais Malinzi ambaye alichaguliwa Oktoba 28 mwaka jana atakutana na Rais wa CAF, Issa Hayatou pamoja na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.

WATATU WAOMBEWA UHAMISHO WA KIMATAIFA
Wachezaji watatu wanaocheza mpira wa miguu nchini Tanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili wakacheze katika nchi za Thailand na Ujerumani.

Mchezaji Khamis Mroki Jamal aliyekuwa na timu ya Daraja la Kwanza ya Polisi Dar es Salaam ameombewa ITC na Chama cha Mpira wa Miguu Thailand (FAT) ili akajiunge na Kabinburi ya nchini humo.

Said Ali Nassor aliyekuwa akichezea FC Turkey ya Zanzibar na Samuel Chuonyo wameombewa na ITC na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) kwa ajili ya kujiunga na klabu ya VfB Eichstatt.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika ikiwemo ridhaa ya klabu zao za hapa Tanzania itatoa ITC hizo.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

6 comments:

 1. Hili sakata la Okwi mbona linafanana na lilie la Drogba aliyeamua kuikacha timu ya Shanghai Shenhua ya China na kwenda zake Galatasaray baada ya timu hiyo ya China kutomlipa mishahara yake.FIFA ilimpa Drogba provisional licence kucheza Galatasaray na hata Schalke 04 ya ujerumani ilipowakatia rufaa Galatasaray kwa kumchezesha Drogba katika mechi baina yao UEFA ilipiga chini rufaa hiyo.Ipo mifano mingi ya kutumia katika kesi hii kama vile Godfrey Walusimbi dhidi ya Don Bosco ya DRC ambye FIFA ilimpa provisional clearance kuchezaURA huku akiwa na mkataba na Don Bosco na sasa ameuzwa Gor Mahia.Mfano mwingine ni wa Olanrewaju Kayode wa Netanya ya Israel ambaye alikuwa na mkataba na Asec hadi juni 2014 lakini akenda Heartlad kwa provisional clearance na sasa amepelekwa kwa mkopo Netanya.Mbona suala hili linakuwa nongwa kwa Okwi?

  ReplyDelete
 2. Usimba na Uyanga naona utalifikisha soka letu pabayakuanzia tff mpaka kwa ninyi waandishi.hivi kama yanga walikamilisha masuala ya tms na itc kutakuwa na kitu cha kumfanya huo mjumbe aonekane kadanganya? mizengwe imeanza baada yausajili wake kuwa published.kwa uwelewa wangu pingamizi linakuja baada ya kinachopingwa kuanza.sasa huyu mjumbe anashtakiwa kwa kipi?hili suala linachujuliwa kishabiki kiasi cha kukera.Kwa okwi ana kitu gani mpaka mizengwe inazushwa kila kukicha juu yake?tuache unazi kwa maendeleo ya soka letu.

  ReplyDelete
 3. Huyo mwajiriwa wa TFF ni mwanafamilia wa soka kweli?kesi yake inastahili kushughulikiwa na mamlaka yake ya ajira/nidhamu ambayo ni Katibu Mkuu wa TFF na siyo kaMATI YA MAADILi

  ReplyDelete
 4. Hao walioweka pingamizi mbona hawakuwahi kulalamika kwamba pingamizi lao halikusikilizwa?Nina wasiwasi huenda pingamizi hilo limepikwa hivi sasa baada ya kuona hata FIFA wamekubali hakuna kipingamizi cha Okwi kucheza Yanga. baadhi ya watu waliongia TFF kwenye uchaguzi wa 2013 kama Kaburu na Kidao pamoja na wale walioteuliwa na Malinzi kwenye kamati ya Sheria kama Hanspope ndio wanaoendekeza ujinga huu kwani bado ni wachanga katika uongozi wa ngazi ya kitaifa kama tff

  ReplyDelete
 5. Ongeeni mambo mengine achaneni na hayo ya Okwi , mchezaji mwenyewe kwanza
  umri umeenda,hebu toeni mawazo jinsi ya kujenga timu yetu ya Taifa.

  ReplyDelete
 6. Yanga hata mkimsajili Okwi zile goli tano hazitarudi OKWI wa 2012 sio wa 2014 Ameshazeeka.

  ReplyDelete