Search This Blog

Wednesday, February 12, 2014

NIONAVYO MIMI:TUNAHITAJI NIDHAMU YA JUU TUNAPOCHEZA SOKA NA WANAWAKE.

Na Oscar Oscar Jr
0789-784858
Mechi ya Mtibwa Sugar vs simba iliyopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri pale Morogoro wiki moja iliyopita,ilimalizika kwa matokeo ya sare ya 1-1,Mussa Hassan Mgosi akiifungia Mtibwa sugar na Hamis Tambwe akiisawazishia timu yake ya Simba.Jonisia Rukyaa toka Bukoba ndo mdada aliyekuwa mwamuzi wa kati wa mchezo huo.

Kisaikolojia na tamaduni za kwetu,zinamuonea sana mwanamke.Mwanaume siku zote anajiona yuko juu,nafsi yake haikubali kuongozwa na mwanamke.Mwanamke nae anapokuwa kiongozi wa mwanaume,hupoteza hali ya kujiamini ingawa sio wote! Jambo hili sio kwenye soka tu,hutokea hata kwenye ofisi nyingine lakini pia ni lazima nikiri kwamba wapo baadhi ya wanawake wanauwezo mzuri sana wa kuongoza wanaume na mambo yakanyooka.

Wachezaji wengi wa Simba na wale wa Mtibwa walipewa kadi za njano nyingi sana,na Shabani Nditi nahodha wa timu ya Mtibwa sugar kuzawadiwa kadi nyekundu.Ukichunguza vizuri kadi hizo utagungua kwamba chanzo ni wachezaji kumdharau mwamuzi wa kike na mwamuzi huyo kujihami baada ya kuhisi anadharauliwa.Jonisia Rukyaa aliitendea haki mechi ile sema tu,hata angechezesha vipi,hawezi kupewa Ballon D'or!

Watangazaji wa skysports Andy Burton na Andy Gray waliwahi kuingia matatizoni mara baada ya kutoa comment zao za kumbeza mwamuzi mdada wa EPL Sian Massey.Kocha wa zamani wa manchester united Sir Alex Ferguson aliwahi kuulizwa kama na yeye anafikiria kuajiri Daktari wa kike kama klabu ya chelsea inavyomtumia mdada Daktari mwenye shahada ya Uzamili(masters) Eva Carneiro,Ferguson alijibu "mchezo wa soka ni mchezo wa wanaume hivyo wachezaji wake hawatokuwa huru kueleza matatizo yao kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa daktari wa kike"

Kumekuwa na mtazamo hasi sana kwa wanawake wanaojihusisha na mchezo wa soka lakini ukweli utabaki pale pale,tuna wauguzi na madaktari wengi tu wa kike na kama tutawakwepa viwanjani,tutakutana nao Hospitali.Tatizo kwenye soka sio mwamuzi wa kike au wa kiume ni ukweli usiopingika kwamba mchezo huu uko kwenye kasi sana na kwa mwamuzi ambaye hapati fursa ya kutazama tukio zaidi ya mara moja,ni rahisi sana kufanya makosa.

Nadhani kabla ya kuwanyooshea kidole kina Israel Mkongo,Oden Mbaga na wengine kwamba wamepewa kitu kidogo au wanaonyesha mapenzi kwa timu fulani ni lazima kwanza tuwapongeze kwa kazi ngumu sana wanayoifanya.Makocha hufanya makosa,wachezaji wanakosea,viongozi wa timu wanakosea na hata wachambuzi wa soka nao kuna muda wanakosea.Unadhani waamuzi ni malaika?

Hakuna maamuzi ya refa ambayo yanaweza kupongezwa,akitoa kadi ya njano anapewa lawama,kadi nyekundu ndo kabisa usiseme.Akitoa penati ndiyo kabisa ataambiwa alikula pesa,akiongeza dakika 8 baada ya dakika 90 za awali kumalizika,atapigiwa kelele mpaka basi! Ni kweli lazima nikubali kwamba kuna muda wanafanya makosa ya kizembe lakini ni wazi kwamba kasi ya mchezo wa soka siku zote inawaacha waamuzi nyuma sio Tanzania tu,hata ulaya na ndiyo maana wanataka tekinolojia ianze kutumika ili kumsaidia mwamuzi kuweza kumudu kasi ya mchezo.

No comments:

Post a Comment