Search This Blog

Friday, February 21, 2014

NIONAVYO MIMI: BARCELONA NA KADI NYEKUNDU KWA WAPINZANI NI KULWA NA DOTO.


Na Oscar Oscar Jr.
0789-784858
Baada ya klabu ya Fc Barcelona kutolewa kwenye nusu fainali ya UCL msimu uliopita na klabu ya Bayern Munich kwa jumla ya mabao 7-0 ambapo Barcelona ililala kwa mabao 4-0 ugenini kwenye dimba la Arianze Ujerumani na kuja kumaliziwa nyumbani Camp Nou kwa mabao 3-0, watu wengi waliibeza na kuidharau klabu hiyo yenye maskani yake kwenye kitongoji cha Katalunya huko nchini Hispania.

Katika ulimwengu wa soka, hakuna timu ambayo itacheza mechi zake zote bila kufungwa na, kufungwa au kushinda mechi moja au mbili,sio kipimo sahihi cha kujua kama timu imepanda au imeshuka kiwango.Real Madrid mwaka 2011 ilifungwa bao 5-0 mbele ya Barcelona,Arsenal alifungwa bao 8-2 dhidi ya Man united pale Old Trafford,Bayern Munich msimu huu imefungwa bao 3-2 dhidi ya Man city tena pale pale Arianze Arena kwa hiyo,hakuna timu ambayo haifungwi.

Moja kati ya mijadala mikubwa wiki hii kwenye medani ya soka,ilikuwa ni kuhusu kadi nyekundu na penati ambazo zilitolewa kwenye michezo ya UCL kati Man city vs Barcelona na ule wa Arsenal vs Bayern Munich.Mchezo wa Arsenal ulimfanya golikipa Wojciech Szczesny kupewa kadi nyekundu na Bayern kuzawadiwa penati wakati ule wa Man city,ulimfanya pia Martin Demichelis kupewa kadi nyekundu na Barcelona kuzawadiwa penati.

Kabla ya kuanza kulalamikia kadi nyekundu na penati ambazo zinatolewa,nataka tujikumbushe kidogo baadhi ya sheria ambazo zinazungumzia mazingira ya kutokea kwa penati na mchezaji kupewa kadi nyekundu.Kadi nyekundu inaweza kutolewa endapo mchezaji atafanya moja kati ya makosa yafuatayo;
1.Mchezaji kumtemea mate mchezaji mwingine 2.Kushika mpira kwa makusudi(kasoro golikipa na awe kwenye eneo lake) 3.kutumia lugha ya matusi 4.Kucheza madhambi makubwa na kumnyima mchezaji wa timu pinzani nafasi ya kuweza kufunga goli.Hapa nimetaja kwa uchache tu.

Kupitia sheria 17 za mchezo wa soka,mwamuzi wa mchezo anaweza kuipa timu penati endapo moja ya yafuatayo yanaweza kutokea mpira ukiwa mchezoni ndani ya eneo la penati; 1.Kumshika mchezaji wa timu pinzani 2.kuushika mpira kwa makusudi 3.Kusukuma 4.kumzuia mchezaji pinzani nafasi ya kufunga ukiwa kama mlinzi wa pili wa mwisho na mengine mengi,hayo ni kwa uchache tu.Mara ngapi umeona yakitokea haya kwenye soka na mwamuzi asifanye chochote?

Sasa tukirudi kwa kipa wa Arsenal Szczesny,utaona kuwa amefanya makosa yote mawili.Moja ni kumzuia nafasi ya kufunga Arjen Roben kwa rafu aliyomchezea ambayo ni kadi nyekundu na pili,kosa hilo limetokea ndani ya eneo la penati ambapo kwa mujibu wa sheria ni penati ya bila utata.Demichelis naye alimzuia Messi nafasi ya kufunga na pili,tukio hilo lilifanyika ndani ya eneo la penati hivyo,adhabu zote mbili ni sahihi.Dante alipewa kadi ya njano na arsenal kupewa penati kwa sababu hakucheza madhambi makubwa dhidi ya Ozil lakini,kwa sababu kosa hilo lilifanyika ndani ya penati,mwamuzi aliamuru kupigwa kwa penati hiyo.

Tangu mwaka 2008 timu ya Barcelona ilipochukuliwa na kocha Pep Gaudiola,imesumbua timu nyingi sana kutokana na aina ya uchezaji wake na ingawa kocha Gaudiola ameondoka klabuni hapo,makocha wote waliomfuatia kama Tito Vilanova,Jordi Raula(alikuwa msaidizi) na kwa sasa timu ipo chini ya kocha Gerrardo Martino wameendelea kutumia mfumo ule ule wa awali.Ni kweli kuna uwezekano timu hii ikawa imepungua ubora ukilinganisha na mwaka 2009 na 2011 walipotwaa ubingwa wa UCL lakini,ni makosa makubwa kudhani kwamba Barcelona ndiyo imekwisha kisoka.Barcelona bado ni timu bora Duniani na inastahili kuheshimiwa.

Lakini kwa nini kila siku wachezaji wa timu pinzani wapewe kadi nyekundu wanapocheza dhidi ya Barcelona na timu hiyo kupewa penati nyingi? Katika kutafakari kwangu,nimepata majibu yafuatayo;

Jambo la kwanza nililogundua ni staili wanayotumia Barcelona.Barcelona wanatumia "Tiki -Taka style" ambapo wanamiliki mpira kwa muda mrefu huku wakipiga pasi fupi fupi na pindi wanapopoteza mpira,wanaondoka kama nyuki kwenda kuutafuta kwa adui na ndani ya muda mfupi,unarudi tena kwenye himaya yao.Aina hii ya uchezaji ni kama "Sumbua bwege" ambapo timu pinzani wanazunguka dakika nyingi sana uwanjani bila kuupata mpira na kwa sababu hiyo ni rahisi sana kupandwa na jazba na kujikuta wakicheza rafu na kuambulia kadi nyekundu.

Barcelona pia inaundwa na wachezaji ambao ni wadanganyifu na mfano mzuri ni Sergio Busquets,Alex Sanchez bila kumsahau Pedro Rodriguez.Wachezaji hawa ni waongo sana na endapo mwamuzi hatokuwa makini,wanaweza kusababisha penati na kadi nyingi nyekundu.Mfano mzuri ni nusu fainali ya UCL kati ya Barcelona vs Inter Millan 2010 ambapo Thiago Motta alipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu ya kawaida tu kiungo Sergio Busquets.Busquets alichezewa rafu mguuni lakini alipodondoka chini,alikuwa akishika kichwa utadhani umechomwa na mkuki!

Kuna muda naona kabisa mapenzi ya waamuzi nayo yanapelekea uwepo wa kadi nyingi nyekundu na penati pengine ambazo hazistahili.Robben Van Persie akiwa na arsenal mwaka 2011 aliwahi kupewa kadi nyekundu kwa kosa ambalo huenda hakustahili.Kama hiyo haitoshi,tumewahi kushuhudia Barcelona akipewa penati mbili kwenye mechi moja dhidi ya Ac Millan.Kutoa penati mbili sio tatizo,lakini ni lazima ziwe zinastahili kutolewa.Timu inayofanya vizuri daima inapendwa na hapa,naona kabisa hili jambo linawatia upofu baadhi ya waamuzi.

Kutokana na ubora wa Barcelona,timu nyingi sana zimekuwa zikikamia pindi wanapokutana.Jose Mourinho akiwa na Real Madrid alifikia kipindi anamuingiza kiungo na mlinzi Pepe kwa ajali ya kucheza tu vurugu uwanjani dhidi ya Xaiv,Iniesta na mtaalamu Messi.Unadhani kwa hali kama hii utaacha kweli kupewa kadi nyekundu? Takwimu zinaonyesha ni mara chache sana kwa timu hasa za Uingereza kucheza UCL na wasipate kadi nyekundu.Ligi ya Uingereza inatumia zaidi nguvu na hata ukirejea kwenye mechi ya man city na Barcelona ya wiki hii,hilo limejidhihirisha.

Na mwisho niseme tu,uwepo wa Messi uwanjani kuna muda inakuwa kero kwa sisi watazamaji kwa sababu analindwa na waamuzi kupita kiasi.Hata ikitokea kaguswa kidogo tu,filimbi inapulizwa na ikiwezekana kadi inatolewa kwa mchezaji aliyemfanyia madhambi hayo.Hakuna namana watu wanaweza wasigusane kwenye mchezo wa soka na kama hawataki Messi aguswe,ni bora wangempeleka akacheze mchezo wa Tennis ambako mchezaji mmoja yuko Magharibi na mwingine yuko Mashariki.

1 comment:

  1. Ndugu ulianza vema maoni yako pamoja na kuwa chini ya Mgandamizo wa ki-EPL,,hapo mwishoni Utanganyika umechukua nafasi yake. Big Stars wanalindwa ktk modern football,, labda itakapobadilika. Hizi si enzi za Sembuli.

    ReplyDelete