Search This Blog

Sunday, February 16, 2014

KUELEKEA BRAZIL: KUNDI B; NI MARUDIO YA FAINALI YA WOZA 2010


  HISPANIA vs HOLLAND

 Na Baraka Mbolembole
 Wiki iliyopita tulitazama kwa ufupi kuhusu historia za timu ambazo zinaunda kundi la kwanza kati ya makundi nane ya michuano ijayo ya kombe la dunia inayotarajiwa kuanza juni 12, nchini Brazil. Kwa kujikumbusha tu ni kwamba kundi A, linajumuhisha timu za Brazil, Mexico, Cameroon na Croatia. Leo, tunatazama kundi B, ambalo linajumuhisha timu nne ambazo zote zilikuwepo katika fainali zilizopita, WOZA 2010. Mabingwa watetezi Hispania, makamu bingwa Uholanzi, Chile na Australia

Hispania itaanza kutetea ubingwa wake Juni 13 kwa kucheza na Uholanzi katika mpambano ambao utakuwa ni sawa na marudio ya mchezo wa fainali zilizopita katika uwanja wa Soccer City, Afrika ya Kusini, mchezo ambao ulishuhudia bao la ushindi lililochelewa zaidi katika mchezo wa fainali, kiungo Andres Iniesta alifunga bao hilo katika dakika ya 117, na kuipatia nchini yake taji la kwanza la dunia. UHolanzi tayari wamepoteza michezo miwili ya fainali na timu hiyo ya kocha Luis Van Gaal, inatajwa kama moja ya timu bora kwa sasa dunia.
Hispania ilishinda michezo yake sita kati ya nane katika hatua ya kufuzu, katika kundi ambalo lilijumuhisha pia mataifa ya Ufaransa, Finland, Georgia, na Belarus, La Roja walikusanya pointi 20, huku wakimaliza na wastani wa mabao 11 ya kufunga. Uholanzi kwa upande wao walikuwa vinara wa mabao katika timu za Ulaya, imefuzu fainali za Brazil kwa asilimia 99.9  ya ushindi, ikiwa imeshinda michezo tisa kati ya kumi  ya kundi ambalo lilikuwa na timu za Romania, Hungary, Uturuki, EStonia na Andorra. ILikusanya pointi 28 kati ya 30 walizotakiwa kupata, huku wakiwa na wastani wa mabao 28 ya kufunga.

Wakati, nchini za Chile na Australia zitakuwa pia uwanjani siku hiyo, zinaweza kutumia mwanya wa vigogo hao kupambana katika mchezo wa kwanza na kuzima jaribio la wawakilishi hao wa ulaya kuvuka kundi hilo kama inavyotabiriwa na wadadisi wengi wa soka dunia. Siwezi kuzungumzia vikosi kwa sasa kwa kuwa muda bado upo na kunaweza kutokea mabadiliko katika muda uliobaki. Hila kwa sasa, Hispania inaonekana kuwa na tatizo katika safu yaa mashambulizi, mfungaji wao bora David Villa bado anapigana kujiweka sawa katika kikosi cha Atletico Madrid, Roberto Soldado ambaye alipewa nafasi kubwa katika michuano ya mabingwa wa mabara, juni mwaka uliopita ameonekana kukosa makali katika kikosi cha Tottenham, Fernando Torres si yule tena aliyekuwa mfungaji wa kutisha ulaya, amekosa makali kwa sasa.

Ni Alvaro Negredo na muhamiaji Diego Costa ambao kwa sasa wanaonekana kwenda sawa na msimu huu katika vilabu vyao, Negredo kwa upande waManchester  City amekuwa mchezaji mwenye mchango mkubwa katika ufungaji na kusaidia wenzake kufunga. Kwa mtindo wa uchezaji wa Hispania, kocha Vicente Del Bosque anaweza kumtumia huyo zaidi kwa kuwa aliwahi kumpa nafasi akiwa timu ya Sevilla. Costa anaweza kuingia hapo kutokana na shabaha yake ya kufunga, ila bado timu hiyo inaweza kucheza bila mshambuliaji asilia, na kuwategemea Cecs Fabregas au Pedro Rodriguez. Kiwango cha viungo wengine wa Jesus Navas na David Silva bila shaka kunaweza kumpasua kichwa kocha Van Gaal ambaye ataondoka katika kikosi cha Orange mara baada ya fainali hizo na kumpisha Guus Hiddink.

Hispania wamewahi kumaliza katika nafasi ya nne katika fainali za mwaka 1950 ambazo zilichezwa nchini humo ndiyo timu pekee kutoka barani ulaya kutwaa ubingwa huo nje ya bara lao. Australia , Socceroos, walifika hatua ya mtoano mwaka 2006 katika fainali za Ujerumani na kutolewa na Italia, walifanya vibaya katika fainali za Afrika Kusini na kushindwa kuvuka kundi ambalo lilikuwa na timu za Ujerumani, Ghana, na Serbia. Timu hiyo kwa sasa inaundwa na wachezaji wengi vijana huku wakitaraji kumtumia kiungo mshambuliaji Tim Cahill kama muhimili wa timu yao. Chile yenyewe uiliishia hatua ya mtoano baada ya kuvuka kundi ambalo pia liliwajumuisha Hispania.


 Hispania imecheza michezo 56 ya fainali za kombe katika mara 14 walizocheza miaka ya nyuma, wameshinda mara 28, wametoa sare mara 12 na wamepoteza michezo 18. Wamefunga mabao 88 na kuruhusu mengine 59 katika nyavu zao.
Jorge Sampaoli kocha wa timu ya Taifa ya Chile , kiungo wa zamani wa Argentina ataiongoza Chile katika fainali zake za tisa mwaka huu. Chile imecheza michezo 29, wakishinda mara tisa, sare wakipata mara sita, wameppoteza michezo 14. Wamebahatika kufunga mabao 34 huku wakiruhusu mabao 45, Uholanzi wenyewe wamefuzu kwa fainali zao za tisa mwaka huu na hawajawahi kutwaa ubingwa huo .


Ili kukwepa kukutana na wenyeji Brazil katika hatua ya pili, Hispania inatakiwa kupiga  hesabu za kumaliza juu ya kundi ili kuikwepa timu hiyo ambayo iliwafunga mabao 3-0 katika fainali ya mabara, katikati ya mwaka uliopita. Orange kwa upande wao wanataraji kuwatumia wachezaji wao waliocheza mchezo wa fainali, haitakuwa na Mark Van Bommel, ila wachezaji wao kama Arjen Robben, Rafaer Van De Vart, Wesley Sneijer, Robbin Van Persie wanatarajiwa kuibeba timu hiyo ambayo ilitolewa katika hatua ya makundi katika fainali za Ulaya mwaka 2012.

Makipa, Tim Krul, 25, Cillessen, 24, na mzoefu Martin Stekelenburg wanatarajiwa kuongoza jahazi la Orange, kocha Va Gaal, anakabiliwa na changamoto ya safu ya ulinzi ambayo kwa sasa inaoneka kuwa na wachezaji wenye wastani wa umri wa chini, Blind, 23, De Vrij, 21, Janmaat, 24, Van Aanholt, 23, Van der Wiel, 25, Veltman, 22 ukitazama umri wa walinzi hawa bila shaka Van Gaal atakuwa na wakati mgumu kuwakabili wachezaji wazoefu wa Hispania, na hata Chile ambao wanao wachezaji wakali kama Alexs Sanchez, Artulo Vidal, Marcel Isra, Medel, J.  Fernandez na wengineo wengineo wengi. Ndugu msomaji ni timu gani ambazo unafikiri zitafuzu kwa hatua ya mtoano kutoka katika kundi hili? Wiki ijayo tutalitazama kundi la tatu la michuano hii


NYEPESI NYEPESI

Ujerumani ilitumia wachezaji 22 kati ya wachezaji 23 waliokwenda katika fainali za kombe la dunia, 2010. Ni idadi kubwa zaidi ya wachezaji kwa timu. New Zealand na Korea Kaskazini zenyewe zilitumia wachezaji 15 tu katika michuano hiyo, idadi ndogo kuliko timu nyingine zote.

Miloslav Klose, anahitaji bao moja tu ili kuifikia rekodi ya ufungaji wa muda wote ya michuano hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na gwiji wa zamani wa Brazil, Ronaldo De Lima, mwenye mabao 15. Klose hadi sasa amefunga mabao 14.

Cafu, beki huyu wa zamani wa Brazil anashikilia rekodi ya kucheza michezo mingi ya fainali za kombe la dunia. Alicheza michezo yote saba wakati Brazil ikicheza fainali mwaka 1994, 1998 na 2002, pia alicheza michezo mitano katika fainali za Ujerumani.

No comments:

Post a Comment