Search This Blog

Sunday, February 9, 2014

KATIKA SOKA LA TANZANIA, WATU WANARUHUSIWA KUINGIA NA VISU UWANJANI!


Na Baraka Mbolembole

Tukio la mwisho la mshabiki wa soka nchini kuchomwa kisu kutokana na mambo ya soka, ni lile lililotokea miaka 13. Wakati wa mchezo wa marejeano wa iliyokuwa michuano ya kombe la washindi barani Afrika, kati ya Simba SC na Ismaillia ya Misri katika uwanja wa Uhuru. 
Shabiki mmoja wa timu ya Ismaillia alichomwa kisu katika kilichotajwa kama kisasi kwa Waarabu hao ambao waliinyanyasa sana Simba nje ya uwanja katika mchezo wa awali huko Misri. 


Kiujumla usalama katika viwanja vya soka nchini unaonekana kutokuwa na matukio ya kutisha, ila ni wakati sasa wa kudhibiti vitu vyenye ncha kali kuingizwa viwanjani. 

Katika mchezo wa Mtibwa Sugar na Simba, jumatano iliyopita, kulikuwa na visu ambavyo kwa hesabu ya haraka vinaweza kuwa kati ya 25-50, ni hatari.

Jamani, Harakati ni njia ya maisha tu ambayo watu wa jamii fulani wanaitumia. Kwa upande wangu nimekuwa nikipita ' mlengo wa kushoto' zaidi katika kufikisha mtazamo wangu kwa watu ama jamii ya mchezo wa soka. Mimi ni mtu ambaye siwezi kufanya chochote, ila mara zote napendelea kuwa wazi katika ninachokuwa ninakiamini. 
Kama ni makosa, nitahitaji msamaha ila sijaweza pata majibu kama kuwasilisha hoja mahala ni makosa. Mtu wa soka ndiye hasa nimekuwa nikimlenga katika maandishi yangu, kumshahuri, kumkosoa, kumsifia na pengine kumpatia mbinu mpya ili aweze kwenda sambamba na mahitaji ya mchezo. 
Soka ni Dini Mpya, klabu ndiyo madhehebu yetu. Hata mimi ninapenda pia, Ninapenda haswa, ila kwenye hoja ya msingi mapenzi yanakuwa kando.
Kichwa cha habari katika hoja yangu ya leo kinasema; ' KATIKA SOKA LA TANZANIA, WATU WANARUHUSIWA KUINGIA NA VISU UWANJANI'

Ni hoja ya kipuuzi?. Inawezekana ikawa hivyo kwa wale ambao akili yao katika viwanja vya soka ni mapato zaidi pasipo kuwa na asilimia walau moja ya usalama wa watoaji pesa hizo, ambao kimsingi ni mashabiki.
Usalama upo sikatai lakini ni ule unapatikana mahala kwa majukwaa yale ambayo hukaa watu mashauhuri, mgeni rasmi na wageni wengine. Katika mchezo wa Mtibwa Sugar na Simba SC, siku ya jumatano iliyopita. Kwa hesabu ya haraka kunaweza kuwa kulikuwepo kwa visu kati ya 25-50, v
isu hivi ni vile ambavyo hutumiwa na wafanyabiasha za miwa, machungwa, n.k.

Kwa kumbukumbu za nyuma, mwaka 1995, wakati wa mchezo wa ligi daraja la pili kati ya Mount Meru ( AFC Arusha) na timu ya FC Bom ya Ilala, aliyekuwa mchezaji hatari wa FC Bom, Shukuru Koya alichomwa kisu na kupoteza maisha mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo. 
Koya ambaye alifunga mabao yote mawili ya timu yake katika ushindi wa mabao 2-1, alivamiwa na mashabiki uwanjani hapo, Sheik Amri Abeid, Arusha na kuchomwa kisu. 
Ni muda mrefu umepita, ila ni wakati wa kutilia mkazo usalama wa wachezaji na mashabiki kwa kudhibiti watu kuingia na visu
uwanjani. 
Haijalishi mfanyabiashara au mtu mwingine. Uwanjani hususani
ndani ya uwanja si mahala kwa biashara. Inakuwaje wanaruhusiwa?.

Wahusika wa hili wanaweza kudhibiti na hali hiyo isiwepo tena. Lipo ndani ya uwezo wao, wakiamua inawezekana, ila wamekuwa wazuri katika kulinda mapato kuliko kutazama usalama. 
Pesa zinalindwa sana, ni vyema katika hilo, lakini vipi kuhusu usalama wa watu?. 
Soka ni mchezo mzuri, mchezo wa hatari na tukio moja tu la kukera linapotokea linaweza kuamsha vurugu kubwa, sasa jamani hawa wauza miwa na machungwa si watakuwa wamekaribisha hatari kubwa uwanjani. 
Ni mtazamo tu ambao kwa msemo wa Kiswahili, Chukua tahadhari kabla ya hatari unaweza kusimamisha hoja yangu hii. Yule, shabiki wa Ismailia hakufa, ila Koya alipoteza maisha yake kwa kuwa tu alifanya kazi yake vizuri uwanjani na mtu mwenye hasira zake akamuhuku kwa sheria zake mwenyewe. Ni hatari, na inashangaza kuwa katika soka la Tanzania watu wanaingia na visu uwanjani. Inashangaza, wanazuia chupa za maji, alafu wanaruhusu visu uwanjani. Ni upuuzi. Nimewasilisha tu ndugu zangu.
0714 08 43 08

No comments:

Post a Comment