Search This Blog

Sunday, January 19, 2014

WANASOKA WA TANZANIA HAWAPIGI PASI, HAWAKIMBII UWANJANI,.....

 
Na BARAKA MBOLEMBOLE
 
Tanzania ipo katika mkakati mzuri wa kuhakikisha soka la Tanzania linapiga hatua na kuondokana na hali ya unyonge wa kushindwa kufuzu hata kwa michuano ya kimataifa kwa miaka mingi sasa. Timu ya Taifa ya Tanzania inajivunia na rekodi yake ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria na michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN mwaka 2009, nchini Ivory Coast. Kwa upande wa vilabu ni Simba pekee ambayo inashikilia rekodi ya kufika hatua ya juu zaidi katika michuano ya Afrika, iliweza kufika hatua ya nusu fainali mwaka 1974 ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika ( ligi ya mabingwa kwa sasa) na kutolewa na Mehala El Kubra ya Misri, na iliwahi kufika hatua ya fainali ya michuano ya shirikisho mwaka 1993, na kupoteza mbele ya Stella Abdjan ya Ivory Coast.

Hayo ndiyo tunaweza kusema ni mafanikio ya juu zaidi katika soka la Tanzania. Tangu wakati huo hadi sasa Tanzania imeendelea kuwa na wachezaji wenye vipaji, ila wale wenye usongo wa kushindana kimataifa wakizidi kupungua. Wakati timu ya Taifa ilipotwaa taji la Castle mwaka 2001, wachezaji wengi walionekana kucheza kwa usongo michuano hiyo, ni wakati ambao soka la Tanzania lilikuwa likichezwa kwa mtindo wa kujitolea na mapenzi. Hali ni tofauti sana na miaka ya hivi karibuni ambayo imeshuhudia timu ya Taifa ikifuzu kwa michuano ya CHAN, na kutwaa ubingwa wa Challenge mara moja, mwaka 2010. Hali na hamasa ya soka la mapenzi na kujitolea limeondoka.

Kwa sasa wachezaji wanahitaji pesa nyingi ili kufanya kazi, iwe klabuni kwao au katika timu ya taifa. Hivyo ndivyo inavyotakiwa kwa wakati huu ambao hali ya maisha ikizidi kupanda, na soka kuwa kazio inayotoa malipo mazuri zaidi. Ila, kwa nini tunashindwa kuwa bora kama miaka ya nyuma? Nje ya matatizo ya kiutawala, mfumo mbovu wa mashindano, uendelezwaji wa wachezaji vijana, wachezaji wa Tanzania wamekuwa na mapungufu mengi ya kiufundi katika uchezaji wao, inawezekana mimi nikawa nimeyaona machache ila umefika wakati wa kuwapa ukweli wachezaji wao kuwa wanatakiwa sasa

 KUPIGA PASI ZA NGUVU, 

Wakati wa mchezo wa Simba na Yanga mwezi uliopita, wachezaji wa timu hizo kubwa za Tanzania walionekana kuanguka anguka. Hao walikuwa wachezaji wa timu kubwa zaidi, zenye makocha bora zaidi, inakuwaje kwa wale wa timu kama Mgambo JKT, ambayo inakosa walau bajeti ya kugharamia na kuendesha kambi yao ya timu?. Kiujumla wachezaji wengi kwa sasa wanakosa nguvu za kutosha na hilo linatokana na wachezaji wenyewe kushindwa kujilinda na kufanya mazoezi ya ziada.

Timu inayokosa stamina mara zote huishiwa pumzi na hilo huchangia timu kutocheza kwa kasi. Wachezaji kama Amri Kiemba, Wazir Mahadhi, Frank Domayo, Salum Abubakary, ni kielelezo tosha katika hilo kwa kuwa mchezo wao wa taratibu hufanya timu nzima kucheza pasi za za kudonyoa, na si kuupiga mpira. Itazame Barcelona inapokuwa katika mchezo wowote tazama namna wanavyokuwa wanapasia wa kupigiana pasi za nguvu hata kama wapo karibu karibu, wanaufanya mpira kukimbia kwa kasi hivyo inawabidi waukimbilie ni hapo ndipo unaweza kuona ubora wao wa pasi za haraka zinazoambatana na kasi. Wanakuwa timamu kimwili na kiakili, na wanapasia mipira ya nguvu. Mtazame Ramadhani Chombo, ni kiungo mwenye kipaji ila hapigi pasi bali huwa anagusa tu mpira, huyu anawakilisha wachezaji wengi wa Tanzania ambao sasa wanatakiwa kubadilisha stahili yao ya upigaji pasi na kucheza pasi ambazo zitakuwa zinaikimbiza timu.

KUKIMBIA UWANJANI...

Nilikuwa nikitazama mchezo wa Manchester City na Cardiff City ambao City walishinda kwa mabao 4-2. Ukiitazama timu hiyo ambayo ilikuwa ikitamani kucheza kama Barca, utaona hivi sasa wameongeza kasi katika uchezaji wao. Pasi za nguvu na wachezaji wakikimbia uwanjani muda wote. Hakuna kusimama. Bao ambalo lilifungwa na Jesus Navas ni kielelezo kuwa magoli marahisi ya City yanatokana na wachezaji wake kukimbia mchezoni, Edin Dzeko alipiga pasi laini, na Navas akatoka pembeni ya uwanja na kuukuta mpira huo umeshapoa, umbali ambao alitoka Navas ulikuwa ni mrefu kuliko  aliotoka mlinzi wa Cardiff, ila ni Navas ambaye aliwahi kufika katika mpira na kuupiga ' kibao kikali'. Aliwekewa pasi njiani naye akakimbia huku akiwa na nguvu. Kama mchezaji unakuwa unasajiliwa kwa pesa ya kutosha basi inakiwa kujituma na kujitolea kama Navas. Kukimbia uwanjani ni jambo lisilofanyika kwa mastaa wa soka Tanzania.

KUCHEZA KWA MUDA....

Mara nyingi timu za Tanzania zimekuwa zikifungwa mabao katika dakika 15 za mwanzo, iwe kwa klabu au timu za Taifa. Makocha wengi huwaagiza wachezaji wao kumaliza mechi mapema. Timu nyingi hushjambulia dakika 15 za kwanza, hupumzika katika robo saaa ya pili na hushambulia tena kwa kasi katika robo ya mwisho. Hivyo wanakuwa na dakika 30 za kufanya mashambulizi na dakika 15 za kupumzika mchezo. Hapa ni lazima wachezaji wao na uwezo wa kumiliki mpira, kupiga pasi sahihi, kukaba kwa nafasi, huku wakimtumia mchezaji mwenye sifa kama za Saimon Msuva kuwasaidia katika mbinu zao. Mchezaji hasiyechoka haraka na mwenye kasi. Wachezaji wa kitanzania hawachezi kwa maelekezo ya kuzingatia umuhimu wa kucheza kwa muda uwanjani na hilo hupekea kukosa uelekeo muda mwingi uwanjani.


KUMSUMBUA MPINZANI HADI MPIRA WA MWISHO...

Arsenal ilikuwa na mechi ngumu sana siku ya jumamoso dhidi ya mahasimu wao wa London Fulham, ila baadae wakashinda kwa mabao 2-0 na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu England. Wakati Fulham walipomuingiza Darren Bent na kuwa na Dimitor Berbatov pia ilikuwa na maana kuwa kosa lolote watakalofanya kurusu bao ndani ya dakika 10 za mwisho lingeweza kuwanyima ushindi. Si mara moja Fulham kutoka nyuma na kupata sare au ushindi dhidi ya Arsenal katika dakika za mwisho. Somo hilo alikuwa nalo Laurent Koncienly ambaye alimfuata mshambuliaji wa Fulham na kumgasi na akashindwa kufunga bao la wazi. Kukata tamaa na kuamini tayari umepitwa ni jambo moja, ila kugeuka na kumfukuza mpinzani ni kitendo ambacho huondoa hutulivu kwa mpinzani wako na hivyo anaweza kuingia katika hali ya kuwa na mapepe na kushindwa kufanya maamuzi ambayo angeweza kuyafanya kwa uhuru kama asingehisi kitu chochote kumharasi. Stamina, mbio, na moyo wa kujituma ni mambo yenye msukumo sana kwa mchezaji wa kisasa.

KUFUNGA BAO SI MSAADA WA MWISHO KWA TIMU YAKO...

Wachezaji wengine wanafikiri kufunga ni jambo muhimu sana kuliko kuisaidia timu yao kupata ushindi wa jumla. Mtazame kiungo Jacky Wilshere wa timu ya Arsenal. Jacky kwa sasa amekuwa akifunga mabao tofaoti na mwanzoni ila mchango wake si mkubwa sana kwa timu. Sijui ni kusifiwa sana ama vipi lakini hamasa ya Jacky hushuka anapofunga mabao. Wakati fulani Jose Mourinho aliwahi kumtoa Joe Cole uwanjani japo alikuwa ameshafunga bao muhimu la timu, baada ya mechi Jose alisema aliamua kumtoa nje Cole kwa kuwa aliona mechi imekwisha kwa upande wake baada tu ya kufunga bao. Ni hivi ndivyo ilvyokuwa kwa wachezaji wengi ambao wanapongia katika orodha ya mara kwa mara ya wafungaji mabao katika timu hujisahau majukumu yao mengine na kujikuta wakiicha timu ikiyumba.

MASHUTI YA MBALI....

Mbona siku hizi hakuna wapigaji wa mashuti ya mita 18 na zaidi, wako wapi kina Gerlad Hillu, Salvatory Edward, Abdi Kassim, SAid Sued, Mecky Mexime wapya? Hao ni wachache tu, soka la Tanzania halina wapigaji wa shati ya umbali mrefu na bahati mbaya limekosa hadi viungo wa kucheza pasi za kupenyeza. Mtazame Yaya Toure, mchezaji bora hupiga pasi nne hadi sita za aina tofauti mchezoni, na kupiga mashuti ya kushtukiza wakati wowote, Sued na Mecky walikuwa walinzi wa pembeni ila ufiti wao ulikuwa ukiwafanya kupasua na mpira kutoka nyuma na kusonga nao mbele kabla ya kupiga shuti la kushtukiza. Wachezaji wa sasa hawapigi mashuti japo wapo wanaojitahidi kufanya hivyo ila si kwa kiwango cha juu.

1 comment:

 1. Nadhani umetoa wazo zuri sana, lakini tujiulize tatizo liko wapi? Mara nyingi huwa tunakuwa na uono wa tatizo lakini pia ni vyema zaidi pia tukawa na udadisi wa kwa nini hatuwi kama inavyotakiwa tuwe?
  Umetoa mifano mingi mizuri lakini timu au wachezaji tajwa wanaofanikisha hayo ni Pro, fanya utafiti uangalie coaching progam zao halafu uje utazame Amateur coaching program utaona tofauti kubwa sana, na hii inatokana na mambo mengi sana ambayo cpati nafasi ya kuzungumzia yote ktk colum hii.
  Labda kwa mtazamo wangu finyu na wa harakaharaka ningeishauri tff ipitie program za team ambazo angalau ni semi-profession halafu zijaribiwe kutumika na Vilabu vyetu vya league kuu, lakini bado utaona kuna mikwamo ya miundo mbinu ya soka ya nchi, uchumi wa vilabu na ufukara wa wachezaji wenyewe.
  Na kabla ya yote pia tazama team za bench la ufundi za kila team, je zinafanana na team zetu? Pro team ina zaidi ya watu nane ktk bench la ufundi bila kuwaweka madaktari, walimu wa Gym na wataalam wa diet wanao support coaching program ya team.
  Juzi tu Arsenal imefanya ukarabati wa daktari wa team ili kutazama kwa nini wachezaji wa team yao wanapata serious injury zinazowaweka nje muda mrefu kuliko team nyingine ktk EPL.
  Shaffih Dauda kuna mengi sana ya kubadilishana mawazo iwapo utawekwa mtandao wa wadau kuchangia hoja kama hizi za msingi ambazo unazileta, na zikasaidia kujua tunaanzia wapi?
  Niishie hapa kwanza, Im a soccer coach.

  ReplyDelete