Search This Blog

Saturday, December 28, 2013

KAGERA SUGAR KUANZA MAZOEZI RASMI JANUARI 2, THEM FELIX ATAMBA KUPASIA NYAVU ZAIDI!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam.

KLABU ya Kagera Sugar inaingia kambini desemba 31 mwaka huu, lakini mazoezi yataanza rasmi januari pili mwakani kujiwinda na mzunguko wa pili  ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi januari 25, 2014.

Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange ameuambia mtandao huu kuwa nia yao ni kurejesha makali yao kama msimu uliopita.

“Mipango ya kambi imekamilika, mimi na kocha mkuu Jackson Mayanja tunajiandaa kukisuka kikosi chetu upya. Kuna makosa yaliyokuwepo mzunguko wa kwanza, tuliyagundua mapema na sasa kazi ni kurekebisha tu”. Alisema Kabange..

Kabange aliongeza kuwa katika dirisha dogo la usajili wamemuongeza  Andrew Mathew kazembe kutoka Abajalo FC  ili kukamilisha idadi ya wachezaji 25.

“Tulitumia muda mrefu kumchunguza mchezaji huyo, tumezingatia nidhamu na uwezo wake, kwa kiasi kikubwa atatusaidia ngwe ya pili  ya ligi kuu bara”. Aliongeza Kabange.

Aidha kocha huyo alisema tatizo la safu ya ulinzi limepata dawa baada ya beki wao wa kati, Amandus Nestar kurejea uwanjani  kufuatia  kupoma tatizo lake la mguu.

“Karibu mzunguko mzima, Nestar amekuwa akisumbuliwa na mguu, madaktari wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha anarejea uwanjani. Hivi ninavyozungumza na wewe, beki huyo yuko tayari kuanza mazoezi na hali hii itaimarisha safu yetu ya ulinzi”. Alisema Kabange.

Kwa upande wake mshambuliaji hatari wa Kagera Sugar, Them Felix alisema kuwa anajiandaa vikali kuhakikisha anaisadia klabu yake kufanya vizuri na hatimaye kuingia tatu bora msimu huu.

Them aliongeza kuwa mchezaji wa mpira wa miguu hana mapumziko, pale timu inapopewa mapumziko, yeye anatakiwa kutafuta njia mbadala ya kufanya mazoezi binafsi ili kulinda uwezo wake na kasi yake.

“Binafsi nimekuwa nikifanya mazoezi na Bukoba Veteran, nimejijanga vizuri na nina uhakika wa kufanya vizuri. Kikubwa Mwenyezi Mungu atupe afya njema”. Alisema Them.

Msimu wa mwaka jana, Kagera Sugar ikiwa chini ya kocha Mkongwe, Alhaji Abdallah Athuman Seif `King Kibadeni Mputa` ilishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Simba, ya pili Azam fc na mabingwa walikuwa Dar Young Africans.

Msimu wa mwaka huu, klabu hii haijawa na matokeo mazuri sana kwani mpaka mzunguko wa kwanza unamalizika, tayari imeshajikusanyia pointi 20 katika nafasi ya sita.

No comments:

Post a Comment