Search This Blog

Tuesday, November 5, 2013

TUMBA SWED ATAMBA KUIUA SIMBA ALHAMISI

BEKI Tumba Swed wa Ashanti United ambaye anaongoza kwa kufunga mabao kwa upande wa mabeki akiwa amefunga mabao matano hadi sasa, amesema piga ua lazima ataifunga Simba katika mchezo wa keshokutwa Alhamisi.
Swed ambaye ana undugu na mabeki Salum Swed wa Mtibwa Sugar na Said Swed wa Coastal Unioni, hadi amefunga mabao matano na kushika nafasi ya sita katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu ya Bara.
Akizungumza na mtandao huu jijini Dar es Salaam, Swed amesema mara nyingi kabla ya mchezo huwa anajiwekea lengo la kufunga na huwa hivyo, sasa kuelekea mchezo dhidi ya Simba ana uhakika atazifumania nyavu.
“Nafanya mazoezi ya maana kuhakikisha nafunga angalau bao moja, huwa namuomba Mungu sambamba na wachezaji wenzangu walau nipate nafasi ya kufunga. Nina uhakika asilimia 70 naweza kufunga na kuongeza idadi ya mabao niliyofunga hadi sasa.
“Simba si timu ya kubeza lakii hata sisi tumejiandaa vya kutosha kuweza kufanya vizuri na kujiweka katika nafasi ya kubaki katika ligi hii. Tunachoomba ni siku ifike na mwamuzi achezeshe kwa haki ili kila timu ipate kile ilichojiandaa nacho,” anasema Swed.
Wakati Simba ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 baada ya mechi 12, Ashanti yenyewe ina pointi 10 ikiwa katika nafasi ya 11 baada ya kucheza mechi 12 pia.
Ashanti ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda msimu huu wa Ligi Kuu huku nyingine zikiwa ni Mbeya City na Rhino Rangers ya Tabora.

No comments:

Post a Comment