Search This Blog

Saturday, November 2, 2013

MALINZI AKABIDHIWA OFISI TFF, TENGA AMKABIDHI SH. Mil 35, NYAMLANI AINGIA MITINI


RAIS mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi mchana huu amekabidhiwa rasmi ofisi za shirikisho sambamba na viongozi wenzake walioingia madarakani wikiendi iliyopita tayari kwa kuanza kazi.
Malinzi alikabidhiwa ofisi na nyaraka mbalimbali na rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Chilla Tenga huku viongozi kadhaa wa serikali wakishuhudia.
Miongoni mwa viongozi waliokuwepo katika ofisi hizo ni Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo.
Kabla ya kufanyika kwa makabidhiano hayo, Tenga alipata muda wa kuhutubia ambapo aliuomba uongozi mpya ulioingia madarakani kuhakikisha unaendeleza dhana ya utawala bora ambayo ilienziwa na uongozi wake ulioingia madarakani kwa mara ya kwanza Desemba 2004.
Tenga pia aliutaka uongozi mpya chini ya Malinzi kuhakikisha inatekeleza mradi wa utengenezaji wa makao makuu ya TFF pamoja na miradi iliyobuniwa kuzunguka ofisi hizo kwa kuzingatia eneo la makao makuu hayo.
“Nakutakia uongozi mwema ndugu yangu Malinzi na timu yako, jambo la muhimu ni kuhakikisha ile dhana ya utawala bora ambayo sisi tuliianza nyie hakikisheni inaendelea na mnakuwa makini na wawazi katika mambo yenu hasa fedha maana huko ndiko kwenye maneno mengi.
“Pia hakikisheni huu mradi wa kuboresha ofisi za TFF unafanyika haraka ili uweze kuendana na hadhi ya taasisi hii nyeti katika michezo nchini, nadhani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmeweka mtaji mzuri wa kiungozi na hata umma utawaona ninyi mnafaa kuendelea kusukuma gurudumu ili la maendeleo ya soka nchini.
“Mimi namfahamu ndugu yangu Malinzi kama mfanyabiashara tena mwenye mafanikio makubwa, sasa kwa kuongoza TFF nadhani atafanya vitu vingi kuhakikisha TFF inafaidika na weredi wake katika biashara,” alisema Tenga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi alisema ana uhakika uongozi mpya wa TFF utafanya kazi kwa kushirikiana katika kuinua soka nchini na kuweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
“Sitoi sifa hizi eti kwa kuwa huyu (Jamal) ni mdogo wangu, lakini imani yangu ipo kwa watu wote waliochaguliwa naye katika kuongoza soka nchini, nadhani hawa wataweza kutufikisha mahala tunapokutaka,” alisema Dioniz Malinzi.
Kwa upande wake, Thadeo aliupongeza uongozi ulioondoka marakani huku akiutakia uongozi mwema uongozi ulioingia madarakani chini ya Malinzi.
“Tenga na wenzake wamefanya kazi nzuri na ninyi mnaoanza kazi leo mna kila sababu ya kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa na Tenga na wenzake, mkifanya hivyo itaonekana wazi wajumbe hawakukosea kuwachagua,” alisema Thadeo.
Naye Silaa aliwasifu TFF kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki na aliwatakiwa uongozi mwema Malinzi na wenzake.

TENGA AKABIDHI SH. 37 MILIONI KWA MALINZI
Uongozi ulioamliza muda wake umekabidhi kiasi cha fedha Sh. 35 Milioni tu kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kutoka ndani ya taasisi hiyo.
Tenga alisema mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba fedha taslimu ni Sh. 33,518,000 na dola za kimarekani 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya timu ya Taifa ya Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita. 
Hata hivyo, Tenga alisema leo hii kiasi cha Sh. 664,000,000 kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki ijayo.  Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika.
Tenga alisema zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya Sh. 672,000,000 yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa.
MALINZI APIGA MKWARA VURUGU, UONGOZI WA KISASI
Muda mfupi bada ya kukabidhiwa ofisi, Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi alisema kamwe hatovumilia kuona watu wanafanya au kuhusika na vurugu, kabla, wakati na baada ya mchezo wowote wa soka nchini kwani kwa kufanya hivyo ni kukandamiza soka la Tanzania.
“Haingii akilini kwa shabiki aliyeacha familia yake anakwenda uwanjani na kuanzisha vurugu zisizo na maana, kama unahisi timu yako imeonewa zipo taratibu za kufuata ili kila mtu aweze kupata haki yake, narudia tena vurugu si suluhisho la kupata haki na sisi tutawashughulikia watu wa namna hii,” alisema Malinzi.
Malinzi alisema chini ya utawala wake atahakikisha kila kitu kinashughulikiwa na uongozi husika kwani haiwezekani mwamuzi kuadhibiwa na kamati isiyohusiana na uamuzi.
“Kila mwenye makosa sasa ataadhibiwa na kamati inayohusika na mkosaji moja kwa moja, kama ni mwamuzi basi kamati ya uamuzi ndiyo itakayoshughulika naye an si vinginevyo,” alisema Malinzi.
NYAMLANI AINGIA MITINI
Aliyekuwa mgombea urais wa TFF, Athuman Nyamlani ambaye katika uongozi uliopita alikuwa makamu wa rais, hakuweza kuonekana katika makabidhiano hayo na haikufahamika mara moja sababu ya yeye kufanya hivyo huku akiwa ni mmoja wa viongozi wa juu waliomaliza muda wao.

No comments:

Post a Comment