Search This Blog

Tuesday, November 26, 2013

DRFA kuwakomalia makocha Ligi Daraja la Pili

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimezitaka timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha makocha wao wanakuwa na taaluma ya ngazi ya pili (Intermediate) na mikataba ya kazi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa DRFA Kenny Mwaisabula amesema Dar es Salaam kuwa timu zote zinatakiwa kutekeleza agizo ili kuendana na malengo ya chama hicho katika kukuza na kuendeleza mchezo huo.
“Tunazitaka timu zote zinazoshiriki Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam kuwa na makocha wenye taaluma hiyo Ngazi ya Pili (Intermediate), tunafanya hivi ili kuendana na dhamira yetu ya kukuza na kuendeleza mpira wa miguu.
“Kama mtakumbuka vizuri DRFA iliendesha mafunzo ya ukocha wa Ngazi ya Pili (Intermediate) Juni mwaka huu ikiwa na nia njema ya kuhakikisha mafanikio yanapatikana, tumekuwa mstari wa mbele na mfano wa kuigwa katika kuendeleza mpira wa miguu hasa taaluma ya makocha,” alisema.
Alisema timu hizo zimepewa mechi tatu kutekeleza agizo hilo na iwapo hawatatekeleza zitachukuliwa hatua.
Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam  ilianza Novemba 23 ikishirikisha timu 32.
Kamati ya Mashindano ya DRFA inaongozwa na Mwaisabula, wakati Makamu Mwenyekiti ni Shaaban Mohamed huku wajumbe wakiwa ni Hugo Seseme, Daudi Kanuti,  Kassim Mustapha,  Abeid Mziba na  Bakari Mtumwa.
Imetolewa Novemba 26, 2013
Mohamed Mharizo
Ofisa Habari Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

No comments:

Post a Comment