Search This Blog

Wednesday, October 23, 2013

YANGA YAIKARIBISHA RHINO DAR LEO, SIMBA KAZI IPO MKWAKWANI MBELE YA COASTAL



YANGA na Simba kwa pamoja leo zinashuka katika viwanja viwili tofauti kupambana na Rhino Rangers na Coastal Union katika muendelezo wa Ligi Kuu ya Bara.
Yanga ambayo ni mabingwa watetezi wenyewe watakuwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, kuvaana na Rhino ya Tabora inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JW).
Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro amesema vijana wake wamefuta makosa na sasa wapo tayari kuikabiri Rhino Rangers leo.
“Kikosi kipo sawa kupambana na Rhino hapo kesho (leo), kama ni makosa tumeshayafanyia kazi na nadhani tutafanya vizuri zaidi katika mchezo huu na kilichobaki sasa ni muda kufika tuweze kuingia uwanjani,” anasema Minziro.
Yanga ilianza mazoezi juzi Jumatatu asubuhi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyora jijini Dar es Salaam baada ya Jumapili kutoka sare na Simba ya mabao 3-3 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa.
Hadi sasa Yanga ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 16 katika michezo 9. Rhino yenyewe ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 7 katika michezo 9.
NAKO mjini Tanga, Simba inashuka dimbani leo mchana kupambana na Coastal Union ya mjini humo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekile Kamwaga ameuambia mtandao huu kwamba, kikosi cha Simba kiliwasili salama Jumatatu jijini Tanga tayari kwa mchezo huo wa leo na wachezaji Henry Joseph, Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud hawapo katika kikosi hicho.
“Timu imefika salama Tanga tangu Jumatatu mchana na hali ya kikosi kizima ni nzuri kinachosubiriwa sasa ni muda kufika ili tuweze kutazama pambano hili safi na la kuvutia kwetu sote, kwani Coastal ni timu nzuri ambayo ina wachezaji kadhaa ambao wamewahi kuwika na klabu mbalimbali za hapa nchini.
“Sisi kama Simba tunaamini tuna timu nzuri ambayo inaweza kupambana na timu yoyote na kutwaa ubingwa hivyo wakazi wa Tanga na miji ya jirani wajitokeze kwa wingi uwanjani kutazama pambano hili la kuvutia,” anasema Kamwaga.
Naye Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora amesema kikosi cha timu yake kimejiandaa vya kutosha na hakuna tatizo lolote linaloikabiri timu yake kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Simba.
“Sisi tupo vizuri kabisa tunaisubiri Simba kwa hamu kubwa kuweza kupambana nao kwani tumejiandaa vizuri chini ya kocha wetu Joseph Lazaro ambaye amejiunga nasi hivi karibuni akichukua nafasi ya Ahmed Morocco.
“Tuna wachezaji wengi wazuri ambao wamewahi kutamba na timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, tunachohitaji sisi ni kufanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” anasema Aurora.

No comments:

Post a Comment