Search This Blog

Tuesday, October 29, 2013

YANGA, MGAMBO JKT KUVAANA TAIFA LEO

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Bara leo itashuka katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupambana na Mgambo JKT katika mchezo wa raundi ya kumi na moja ya ligi hiyo.

Yanga inaingia uwanjani leo ikiwa na pointi 19 ilizopata katika mechi 10 ilizocheza huku ikiwa nafasi ya nne. Azam inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 20 huku zote zikiwa zimecheza mechi 10. Mbeya City ni ya tatu ikiwa na pointi 20 katika mechi 10.

Kwa upande wao, Mgambo wanaingai uwanjani wakiwa na pointi tano walizopata katika mechi 10. Timu hiyo inaburuza mkia katika ligi hiyo.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya leo kutakuwa mchezo utakaozikutanisha timu mwenyeji za mkoa huo ambazo ni Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment