Search This Blog

Monday, October 21, 2013

MAKALA: SIMBA vs YANGA- MATOKEO YAMETENDA HAKI?


NA BARAKA MBOLEMBOLE

Mashabiki wa Yanga watalalamikia sana uchezaji wa safu yao ya ulinzi huku wale wa upande wa Simba wakibaki wasiamini kilichotokea katika pambano la mahasimu wa soka la Tanzania, ambalo lilimalizika kwa sare ya kufungana mabao 3-3, siku ya jumapili iliyopita.

Kocha wa Yanga, Ernie Brandts aliishia kuwatupia lawama wachezaji wake kutokana na kupoteza uongozi wa mabao 3-0 hadi nusu ya kwanza ya mchezo, huku akiwaambia kuwa hawana hadhi ya U-pro. Alishangaa kuona wachezaji wake wakiona wamemaliza mechi baada ya kuongoza mchezo na kusahau kuwa soka ni mchezo wa dakika 90, huku wakitambua wanacheza mchezo mkubwa. Kocha wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni yeye aliishia kusikitikia kiwango cha chini kilichooneshwa na timu yake, na wakati wa mapumziko aliwaambia wachezaji wake, "Najua kuna timu mbili ndani yetu, ipo timu ya uwanjani na timu ya nje ya uwanja. Ila hayo mabao yanatosha, nendeni kipindi cha pili mkacheze mpira". Unazitazanaje kauli hizi?

Kwa maoni yangu, Kwanza, nampongeza mwamuzi na wasaidizi wake. Israel Nkongo na wenzake waliingia uwanjani wakiwa chini ya ulinzi mkubwa wa polisi, haikuwa ' fair' kwa mtazamo wangu. Alijengewa mazingira mabaya ya kutokuwa na imani naye, huku upande wa kila timu ' ukimkataa' kabla ya mchezo. Alichezesha vizuri kwa muda wote, alikuwa na kasi, pumzi na uwezo wa kuyatazama matukio kwa usahihi, alishindwa kusimamia ipasavyo rafu ambayo Jonas Mkude alimchezea Frank Domayo, ilikuwa ni kadi nyekundu ya moja kwa moja, ilikuwa ni bahati kwa Simba.

Pili, nawasifu wachezaji kwa kucheza bila ubabe, ukitoa rafu mbaya aliyocheza Mkude, mchezo haukuwa na rafu za ubabe. Ndiyo zilikuwepo faulo wakati fulani lakini hazikuwa za kutisha. Tatu, nazilaumu timu zote kwa kukosa umakini katika muda mwingi wa mchezo. Nne, nalisifu benchi la ufundi la Simba kwa kuwarudishia imani wachezaji wao kuwa mechi ilikuwa haijaisha, na wachezaji wakafanya kweli. Yanga nawalaumu, kama ulikuwa ukifuatilia mechi kwa umakini baada ya wao kufunga bao la pili, walianza kukosa nidhamu ya mchezo, nyodo na mchezo wa madaha ukashika hatamu na kujiona kama tayari wamemaliza mechi. Magoli mawili ya vichwa waliyofungwa yanaonesha kuwa timu nzima haikuwa mchezoni. Walifungwa mabao ya wazi.

MRISHO NGASSA 

Baada ya kufunga bao la kuongoza kwa upande wa timu yake katika dakika ya 15 ya mchezo, Ngassa tayari alikuwa amemaliza mechi kwa upande wake. Alikuwa msumbufu, hatari na mchezaji aliyeivuruga ngome ya Simba kwa dakika 20 za kwanza za mchezo. Hata bao lake alilofunga lilitokana na kasi yake ambayo ilimsaidia kubadilishana nafasi kwa haraka na Hamis Kiiza wakati Didier Kavumbagu akiwa amemiliki mpira na walinzi na mmoja wa walinzi wawili wa kati wa Simba, Kiiza akakimbia pembeni na alipopigiwa pasi na 'Kavu' aliiunganisha kwa mtindo wa ' krosi kiki' ambayo iliyokuwa ni ya haraka na Ngassa akajikuta akifunga bao muhimu la kuongoza na kukomboa mali zake.

Yanga, wakatengeneza bao la pili baada ya kuwazidi nguvu Simba, ambao walikuwa wakianguka anguka mara kwa mara. Kiiza akafunga mara mbili. Kocha wa Simba, King alisikitishwa na uchezaji wa timu yake katika kipindi cha kwanza. Simba ilikuwa inacheza kama timu isiyo na kocha. Kuna wachezaji walionekana kucheza vizuri, ila kundi kubwa lilionesha kiwango cha kufadhaisha. Ramadhani Singano, hakuwa na makali yake, na alishiriki mara kwa mara kuisaidia Yanga. Mipira mingi ilikuwa ikifia katika miguu yake, alionekana mzito, na aliisadia Yanga kupata bao la tatu baada ya kukumbwa kikumbo na Athumani Idd ' Chuji' na kunyang'anywa mpira uliozaa bao la tatu la Yanga.

Abdulhalim Humud alifanya mambo kuwa magumu zaidi kwa upande wa timu yake. Mkude alikuwa na bahati alipopewa kadi ya manjano na si kadi nyekundu, na baada ya tukio lile alionekana kuimarika katika suala la nidhamu. Ila alipoteza kujiamini na kujikuta akipiga pasi mbovu za mara kwa mara na wakati fulani alionekana kushindwa kumiliki mpira hata kwa sekunde moja. Yanga walitawala kila idara katika kipindi chote cha kwanza, huku idara yao ya kiungo ikitawanya mipira katika wingi na kuongoza mchezo, Chuji alicheza vizuri katika nafasi ya kiungo-mlinzi, msaada wake mkubwa ilikuwa ni kumzima Mkude na kumghasi kila alipokuwa na mpira. Domayo alikuwa na macho makali katika mchezo huo alipiga pasi nyingi sahihi kitu ambacho kilifanya Yanga kukimbia huku wakiwategemea Ngassa na Kiiza katika mbio, 'Kavu' katika kumiliki mpira na Niyonzima kama, kiungo mchezesha timu akitokea pembeni.

Humud ambaye alikuwa na jukumu la kuhakisha, Domayo hapati muda mwingi wa kutulia na mipira na kupiga pasi ndefu huku akiwalinda walinzi wake wa kati, alionekana mzito, na asiye jiamini na kugeuzwa mchezaji wa ' ovyo'. Kiwango cha chini cha Humud kilipelekea timu nzima kushindwa kuwa na kasi, na kujikuta wakipotezwa uwanjani na mfumo wao wa 4-4-2 dhidi ya ule wa 4-3-3 walioutumia Yanga. Sijui kwa nini King aliishia kusema timu yake ina makundi mawili ndani yake, labda ni kutokana na kiwango cha chini cha mchezaji kama Humud .

BRANDTS
 Kocha huyu wa Yanga alifanya mabadiliko ya kipuuzi, pale alipomtoa Kiiza na kumuingiza Saimon Msuva. "Mimi nashindwa kuelewa kiukweli kile kilichotokea. 3-0 hadi 3-3!. Kocha aliniambia nikakabe tu" anasema Msuva wakati nilipozungumza naye leo hii. Sikatai kuingia kwa Msuva, ila kocha Brandts alitakiwa kumtoa mmoja wa wachezaji wake wa nafasi ya kiungo, Niyonzima au Domayo kama aliona kuna ulazima wa kufanya mabadiliko. Alipigwa bao na King ambaye aliamua kucheza kamari kwa kuwaingiza ' yosso', Said Ndemla na William Lucian na kuirudisha timu yake katika mfumo wa 4-3-3 kutoka ule wa 4-4-2.

"Ni matokeo ya kawaida tu katika mchezo wa soka. Wakati nipo katika benchi niligundua kuwa Niyonzima ndiye alikuwa tatizo kubwa kwetu. Alikuwa akimuumiza kichwa kila mmoja, nilimfikiria sana wakati nipo katika benchi.. Wakati naingia uwanjani nilikuwa nawaza ni mbinu gani nifanye ili kuisadia timu yangu kukomboa zile goli tatu. Alichoniambia King ni kwamba nikafanye vitu muhimu ambavyo vitaisadia timu, nikamsikiliza na matokeo yakabadilika kama ulivyoona." William Lucian anasema.

 Brandts anasema wachezaji wake ni wazembe ila naye alishindwa kwenda na muda na kusoma mchezo. Alipigwa bao na King. Kiiza alikuwa msumbufu na nilifikiri alikuwa karibu kufunga 'hat-trick', ajabu akatolewa na kuwafanya walinzi wa Simba kusogea mbele zaidi.

ALLY MUSTAPHA
 Mimi binafsi nimekuwa nikisikitishwa na kiwango cha chini cha kipa huyu msimu huu. Katika magoli 12 aliyofungwa hadi sasa, saba hadi nane yametokana na mipira ya kona, krosi au faulo. Mipira hii imekuwa tatizo kubwa kwake japo aliweza kuendana nayo msimu uliopita. Nimekuwa nikijiuliza mbona anashuka kwa kasi sana badala ya kuendelea kupanda? tatizo ni nini? Amelewa sifa baada ya msimu wa mafanikio au kiwango cha mafunzo kimepungua. Magoli mawili ya vichwa aliyofungwa siwezi kumlaumu. Nitawalaumu wachezaji na walinzi ambao waliruhusu Joseph Owino na Gilbert Kazze kuruka wakiwa huru na kupiga mpira. Ni uzembe wa mabeki, ila hata yeye hawezi kukwepa lawama kuwa kiwango chake alichomaliza nacho msimu uliopita kinaporomoka kwa kasi. Alichangia sare ya timu yake, alitakiwa acheze na maeneo huku akiwapanga wachezaji wake kuhakikisha wachezaji wa Simba hawapewi uhuru wa kuruka peke yao

"Asante kaka, ila nimeshuka kiwango, sijui kufundisha, njoo unisaidie" alinijibu kocha wa makipa wa Yanga , Razaq Siwa nilipohoji kiwango cha kipa wake huyo.

JULIO AACHE MAZOEA 
Kocha wa Simba, King alikuwa na mambo mengi katika kichwa chake hasa wakati timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 3-1, kuna wakati alionekana akimsihi kocha wake msadizi asiwasemeshe sana wachezaji na kuwapigia kelele za mara kwa mara. Ni kweli wakati mwingine kelele za makocha huja wakati mbaya na mchezaji zinaweza kumtoa mchezoni zaidi. Najua, Julio alifanya vile kama sehemu ya kuwahamasisha na kuwakumbusha majukumu yao, ila wakati mwingine kelele za makocha hazifai na huwapoteza zaidi wachezaji

DHAIRA NA UREFU WAKE
 Mashabiki wa Simba waliondoka uwanjani baada ya nusu ya kwanza ya mchezo huku wengi wakiwakataa makocha wao, ila kipa Abel Dhaira aliionesha kuwakatisha tamaa kila mpira ulipokuwa ukienda katika lango lao. Aliishia kutema ' ovyo ovyo'. Nakumbuka niliandika kuwa mshindi wa mechi anaweza kuamuliwa na kipa atakayecheza vizuri zaidi katika mchezo huo, ila wote wakawa ' dhaifu' na tumepata mechi mechi mbovu iliyonogeshwa na udhaifu wa makipa MASHABIKI 11, wazimia ilikuwa ni balaaa

6 comments:

 1. Mbolembole umetuonyesha hauna jipya mechi tuliiona wote ulichoonyesha hapo ni ushabiki wako wa YEBOYEBO mpira hauchezwi jukwaani, Magazetini Wala Redioni, nyinyi ndo mnawaharibu hakina ngasa kwa kuamini matokeo ya DK 45 badala ya 90. UBORA WA SIMBA NDO ULIOBADILISHA MATOKEO huo ndo ukweli zingine porojo.

  ReplyDelete
 2. Nimeipenda thread hii. Very analytical and straight. Hata ambao hatukuwa uwanjani tumeburudika. Analysis nzuri kama hii nilizoea kuisoma enzi za Mkumbwa Ally na Stephen Rweikiza wakiandikia The Daily/Sunday News miaka ya 1970-80.
  Taifa linahitaji akina Mbolembole wengi kama huyu ili kuchangia maendeleo ya soka letu.
  Ni wazi kuwa Yanga na Simba ndizo "nguzo/pillars" za soka la nchi yetu, klabu zingine hazijajijenga kuwa sustainable kama klabu hizi kongwe hadi sasa na itatuchukua miaka kama sio miongo kwa klabu zingine kufikia kiwango cha uthabiti cha Yanga na Simba.
  Ni kwa mantiki hii, kila mpenda soka nchini ataungana na bw. Mbolembole kuziambia wazi klabu zetu, kuwa uzembe wa mchezaji na timu unaliangamiza soka la TZ.
  Tayari kuna minong'ono ya kila klabu kuhisi kuwa matokeo ya mechi ya jana ni zao la "hujuma". Lakini kwa aliyesoma uchambuzi huu, ataondokewa na taswishi hilo baya, ambalo aghalabu hupelekea kutimuliwa wachezaji na makocha.
  Hongera nyingi bw. Mbole Mbole kwa uchambuzi na Bw. Shaffih asante kwa kuiweka thread hii jamvini hapa.

  ReplyDelete
 3. Napenda kukupongeza mchambuziiiii kwakuweza kuonaaa mapungufu ktk mechi ilaaa ninavyoonaaa mie mdau nikupenda kupita kiac nakusahau majukumu yenu km waandishi wa habari nakuanza kuzungumziaa mtu baada yakuzungumziaaa timu na ukweli na uhalisia wake,,mpira ni mchezo wa makosa ndio maana kila siku makosa yanatokea na magori yanapatikana,mie nacikitika sn waandishi wengi mmeanza kupenyesha sumu ya chuki kwa kipa Dhaira,,,,kwa malengo na chuki tu juu yake,wkt anafanya kazi ya ziadaa na jana kafanya kazi kubwaaaa sn,,,,,,unadai eti anatema mipira ulizaaa makipa kaziii yakipaaaa,,kipa anaangalia options yakudaka au kuupanguaaa mpira,,,km anaona akiudaka ni salama zaidi atadakaa,,,km kuupanguaa ni salama bac atafanya hinyo,,,acheniiiii chuki zenuuuuuu kwa makipaaaaa tazameni timu yote cio kipa,,,,mwaka janaa mmewalisha sumu wanasimba eti Kaseja m-bovu kwakutumiaaa karamu zenu hadiii katolewa ss mmeanzaa kwa dhaira,,,,,tena kwa bhatez mmeanza....kuzitumiaaa karamu zenu vibaya,,,sio vibaya kutoa maoniiii ilaaaa yasionyeshe unazi,,chuki juu ya mtu fulani shortly Yanga ilicheza vizuri kipindi cha kwanza km timu,,,,,kipindi cha piliiiii timu ilipotea yote naniiii wakumlaumu km sio timu kulikooo kumlaumu mtu...hata hiyo simba unaposema humud sio humud ni timu ilikua weak first half..so plzzzz acheniii profesionalism ifanye kaziiiiii yake mwandishi wa michezo awe ni mtu anayejuaaaa mpiraa kaucheza vizuriiii,,,,,,Dauda chambua game,,,Ally Mayah mko wapiiiiiiiiii mnawaachiaaa watu wanaoletaa chukiiiiiiii nakutuludisha nyuma kisoka,,,nawaclisha

  ReplyDelete
 4. Nimeipenda hii thread. Ni uchambuzi very objective. Tunahitaji akina Mbolembole wa aina hii wawe wengi kusaidia kusahihisha kasoro za kila mchezaji, kocha na kila timu. Uchambuzi kama huu nilikuwa nausoma enzi za kina Mkumbwa Ally na Stephen Rweikiza wakiandikia The Daily /Sunday News.
  Ni ukweli soka la nchi hii linategemea uwepo na uchezaji mzuri wa Yanga na Simba, bado hatuna klabu zenye timu madhubuti na sustainable kuzidi hizo mbili, hivyo zinapoharibu, ndio kuharibika kwa soka la nchi hii.
  Hongera na asante bw. Mbolembole kwa anaylsis, na Bw. Shaffih kwa kuochapisha.

  ReplyDelete
 5. uwezo mdogo sana katika kuchambua soka kaka...nakuomba endelea na kuripoti taarifa tuu kama hapo ulivyofanya..Lucian amesema nn au Msuva amesema ila kuchambua huwezi itakushusha kaka.
  Kwa wasiokuwepo watakuona fubdi kwa walioangalia unawaboa na kuwafanya wasisome tena makala zako...Mimi sio mnafik kaka zingatia hayo.

  ReplyDelete
 6. Nalaumu bench la ufundi la team yetu ya Yanga sijawahi kumkubali Msuva hata siku moja sub alitakiwa aingizwe either telela au nizar na wakumtoa alikuwa niyonzima au ngasa kwani walikuwa hawakabi hongera kwa Kibaden kwa sub nzuri mpira umeisha ila kwauchezaji wa Yanga kipindi cha kwanza sijui wwaliutoa wapi ule mpira ulikuwa wa kiwango cha juu mno sijui nini kilitokea vyumba vya mapumziko Timu ilirudi ikiwa imelowa na uchovu wa kupitiliza. Shaffih ahsante kwa ku analyse vizuri anaepinga hayo ni mawazo yake

  ReplyDelete