Search This Blog

Friday, September 20, 2013

BAADA YA TAIFA STARS KUBORONGA - KOCHA KIM POULSEN APIME UZITO WA KIBARUA CHAKE NA AJIUZULU

MAKOCHA wa kigeni wanaoajiriwa kuzinoa timu za soka za taifa Tanzania – Taifa Stars, Kilimanjaro Stars, Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys – wana bahati.
Matokeo mabaya uwanjani huwa hayana athari zozote katika mikataba yao. Hata baada ya timu zao kufungwa vibaya, huendelea hadi mwisho na hata kuongezewa mpya.
Marcio Maximo wa Brazil aliletwa nchini na serikali kwa mbwembwe mwaka 2006, akaingia mkataba wa kuinoa Taifa Stars kwa miaka mitatu. Alipewa kazi ya kuipeleka Stars fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) 2008 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) mwaka 2009.
Baada ya kufanikiwa kuipeleka Stars CHAN, Maximo aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja ili aipeleke Stars fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2010 na Kombe la Dunia 2010. Hakufanikiwa.
Akaja Jan Poulsen wa Denmark akachukua dola zake akaondoka Stars haikufuzu kokote. Jahazi akapewa ‘mdogo wake’ Kim Poulsen ambaye alikuwa akizinoa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys, hajafanikiwa kwa lolote na haelekei kabisa kujisukuma ajiuzulu labda asukumwe.
Matokeo mabaya chini ya makocha hawa Maximo, Poulsen na Kim yalizindue Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka kipengele katika mikataba ya makocha kwamba wasipopata matokeo mazuri waachie ngazi; mkataba usitishwe.
Mfano, Chama cha Soka Malawi (FAM) kimeachana na kocha mkuu Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji baada ya kushindwa kuipa timu ya taifa, The Flames, tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014.
FAM iliingia mkataba wa muda wa miezi ya miwili na kocha huyo na angeongezewa mkataba ikiwa kungekuwa na matokeo mazuri, lakini baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Nigeria siku chache zilizopita ziliifanya FAM kumtupia virago Mbelgiji huyo kwa kutoingia naye mkataba mpya.
Kocha wa Tunisia, Nabil Maaloul alitangaza kujiuzulu nafasi yake wikiendi iliyopita baada ya timu yake kutolewa katika harakati za kufuzu Kombe la Dunia 2014, kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Cape Verde.
Matokeo hayo yaliyoiwezesha Cape Verde kufuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia, yalimkatisha tamaa Nabil huku akishindwa kuamini kilichotokea katika mchezo dhidi ya taifa hilo changa kisoka.
Hata hivyo, Tunisia imerejeshwa kufuzu Kombe la Dunia 2014 baada ya Cape Verde kubainika imemchezesha mchezaji asiyehalali kinyume cha kanuni zinavyoelekeza. Hii ina maanisha, Tunisia imerejeshwa kwa mlango wa uani.
Huko Libya, kocha wa timu hiyo Abul Hafidh Erbeesh naye alibwaga manyanga baada ya kuona timu yake imefungwa bao 1-0 na Cameroon na kukosa nafasi ya kusonga mbele. Japokuwa Libya haina historia kubwa katika soka Afrika, mategemeo yao yalikuwa makubwa kama ilivyokuwa kwa Tanzania.
Kwingineko duniani, kocha wa Czech, Michal Bilek ameamua kujiuzulu nafasi yake baada ya kuona mambo hayaendi sawa katika kikosi chake. Huyu anaonekana kutumia busara zaidi kuhusu nafasi yake na anafahamu namna wananchi wanavyojisikia uchungu kwa nchi yao.
Bilek amejiuzulu baada ya timu yake kufungwa mabao 2-1 na Italia hivyo kukosa nafasi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014.

JAMBO LA KUJIULIZA:
Malawi imeachana na Saintfiet, Nabil amejiuzulu Tunisia, Erbeesh amebwaga manyanga Libya na Bilek ameamua kukaa kando Jamhuri ya Czech wote kutokana na matokeo mabaya, kwa nini Tanzania inakaa na akina Maximo, Poulsen na Kim hadi mwisho wa mikataba yao?
Baada ya Kim kushindwa kuipeleka Stars kwenye michuano ya CHAN, fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia amebakiza nini kwenye mikoba yake ya ukocha kitakachoisaidia Stars kuwa na matumaini ya kucheza  CAN mwaka 2015? Je, bado anahitajika?
Makocha waliojiuzulu wameogopa aibu ya kutimuliwa kama mikataba yao inavyosema wasipofikia malengo, lakini kwa Tanzania makocha hawana hofu yoyote kwa vile mikataba yao haina kipengele cha kulazimishwa kujiuzulu.
Wakati umefika TFF na mkurugenzi wa ufundi wa TFF wawape makocha wa kigeni mikataba inayowawajibisha kwamba wasipofikia malengo waondoke bila fidia, la sivyo watafukuzwa.
Ni aibu kuendelea kukaa na kocha ambaye ameshindwa kuipeleka Stars hatua ya kupata ushiriki hata wa  CHAN baada ya kutolewa na Uganda ambayo ligi yake si bora kulinganisha na ile ya Tanzania Bara.
Wachezaji wengi Afrika Mashariki hupenda kuja kucheza Ligi Kuu ya Bara kutokana na msisimko wa ligi hiyo na malipo mazuri.
Udhaifu unaoonekana sasa kwa Stars ni uwajibikaji wa Kim na kurugenzi ya ufundi ya TFF. Hakuna anayeweza kumkemea Kim wala kumwajibisha kama ilivyo kwa makocha wa mataifa mengine.
Kim Poulsen apime uzito wa kazi yake kama makocha wa Libya, Czech na Tunisia asisubiri kutimuliwa kama Saintfiet aliyewahi kubangaiza akiwa na klabu ya Yanga, Dar es Salaam.

1 comment:

  1. Pia Shaff, watu wengi wanasahau nafasi ya kamati ya ufundi pia na mkufunzi wa ufundi wa TFF,.Hao watu wote wanatakiwa wabadilishwe.kwa maana wameshindwa kumpa ushauri mzuri kocha.Makocha wanafanya makosa yaleya, timu inashindwa kuwa na mafanikiokwa karibu miaka kumi, graph yake inashuka chini.

    ReplyDelete