Bia ya Castle Lager imepanga kuandaa kliniki za soka ambazo
zitaongozwa na makocha kutoka Klabu ya Barcelona inayoshiriki Ligi Kuu ya
Hispania maarufu kama La Liga.
Hayo yalidhibitishwa Agosti 17 mwaka huu katika Hoteli ya Hyatt jijini
Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Robin
Goetzsche wakati wa uzinduzi wa ushirikiano kati ya Castle Lager na Klabu ya
Barcelona.
Goetzsche alisema ushirikiano huo utahusisha shughuli za soka ambazo
zitashirikisha zaidi ya timu 120 nchini kote huku wakijitahidi mradi huo
kufikia jamii katika mikoa yote.
“Kutakwepo na kliniki za soka ambazo zitaongozwa na makocha kutoka Klabu
ya Barcelona na kuna uwezekano timu itakayoibuka bingwa katika mchezo wa soka
itakayoandaliwa na bia ya Castle kusafiri kwenda Camp Nou nchini Hispania
kucheza mechi ya kirafiki,” alisema.
Goetzsche alisema bia ya Castle Lager imeingia mkataba wa miaka mitatu
wa ushirikiano na Klabu ya Barcelona Julai 26 mwaka huu ambapo bia hiyo bora
Afrika ndiyo mdhamini mkuu wa vigogo hao wa Ulaya na duniani barani Afrika.
Alisema
ushirikiano huo haulengi tu biashara na wateja wao mbali jamii yote ambayo
bidhaa yao inawafikia lengo likiwa ni kukuza soka.
Mgeni rasmi katika shughuli hiyo alikuwa
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ambaye
alisifu bia ya Castle Lager kwa kupiga hatua moja mbele kutokana na
kushirikiana na Klabu ya FC Barcelona kuendeleza soka la humu nchini.
Dk Mukangara alisema ushirikiano huo umekuja wakati mwafaka ambao
Tanzania imekuwa ikitilia mkazo kukuza na kuendeleza vipaji vya soka katika
taasisi mbalimbali na akademi chache ambazo hazina miundombinu stahiki.
“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, napenda kuwashukuru Castle Lager
kwa kutusaidia na ninaamini hii itasaidia kuendeleza soka la humu nchini,”
alisema.
Dk Mukangara aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Castle Lager na Klabu
ya FC Barcelona iliyosheheni wachezaji nyota kama vile Lionel Messi, Neymar na
Andres Iniesta itakuwa changamoto katika kubadilisha maisha ya wachezaji wa
soka Tanzania.
Waziri huyo alihakikisha kufanya kazi kwa karibu na Castle Lager kuwawezesha
jamii nchini kote kupitia mchezo wa soka.
“Napenda kutoa wito kwa wanasoka wote Watanzania na wataalamu wa soka
kukumbatia fursa hii inayotolewa kwa ushirikiano wa Castle Lager na Klabu ya
Barcelona kutimiza programu zilizoainishwa kwenye mkataba kwa manufaa ya soka
letu,” alisema Dk Mukangara.
Miongoni mwa walikwa katika uzinduzi huo walikuwa Balozi wa Hispania
nchini Tanzania, Luis Manuel Ceuesta Civis, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Said Meck Sadik, Meya wa Ilala Jerry Slaa na Mkurugenzi wa
Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo.
No comments:
Post a Comment