Search This Blog

Thursday, May 23, 2013

TATHMINI YA LIGI KUU 2012/03 - UKATA, MIGOGORO VILIATHIRI LIGI KUU



UKATA na migogoro isiyoisha baina ya viongozi na wanachama ndiyo ilichangia baadhi ya timu kufanya vibaya na nyingine kushuka hadi daraja la kwanza.
Timu pekee ambazo hazikuathiriwa na migongano kati ya viongozi na wanachama au viongozi na wachezaji ni zile zinazomilikiwa na mashirika kama Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, na zinazomilikiwa na majeshi.
African Lyon, licha ya kuwa na wadhamini pamoja na Coastal Union, Toto African na matajiri wa udhamini Simba na Yanga zilikumbwa na migogoro iliyoziathiri kwa namna moja au nyingine.
Yanga, pamoja na kutambia Kocha Tom Saintfiet wa Ubelgiji, ilianza ligi kwa kutoka suluhu na Prisons na ilipochapwa 3-0 na Mtibwa Sugar akatimuliwa akaajiriwa Mholanzi Ernie Brandts, aliyeiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara baada ya kufikisha pointi 60.
Simba ilianza kwa shangwe, lakini ilipotoka sare kadhaa na kuambulia vichapo, wanachama wa tawi la Mpira Pesa wakaujia juu uongozi, baadhi ya viongozi wakaachia ngazi na kocha Mserbia Milovan Cirkovic akafukuzwa akaajiriwa Mfaransa Patrick Liewig ambaye alifurukuta na kuiwezesha kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45. Bila migogoro huenda Simba ingemaliza nafasi nzuri zaidi.
Azam FC isiyo na mashabiki wengi, ilianza msimu ikiwa chini ya Mserbia Boris Bujak 'Buka' lakini ghafla alitimuliwa na nafasi yake ikajazwa na kocha wake za zamani Mwingereza Stewart Hall aliyeisaidia kushika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 54. Vilevile timu hiyo ilivurugana na wachezaji watatu ikidai wamepokea rushwa.
Kwa tathmini, timu hizo zenye ukwasi wa fedha ndizo kwa mara nyingine zimeshika nafasi tatu za kwanza. Msimu uliopita Simba ilikuwa bingwa ikafuatiwa na Azam na Yanga.
Wakati Simba na Yanga zilikuwa na uwezo wa kutimua makocha na kuajiri wengine, Toto African ya Mwanza ilikosa uwezo huo ikabaki ikipigania kutoshuka daraja. Ukata ulipoielemea Toto ilibaki ikilalamikia ugumu wa ratiba na waamuzi hadi imeshuka daraja la kwanza.
African Lyon ilianza ligi ikiwa na mikakati ya kujinasua kwenye ukata lakini ilikwama. Kwanza kampuni ya Zantel iliyotaka kuidhamini iliwekewa kauzibe na pili kocha Muarentina Pablo Ignacio Velez aliyeajiriwa kuiboresha kikosi alitupiwa virago.
Timu ikabaki chini ya msaidizi wake Jacob Otieno naye aliposhindwa ikaachwa kwenye mikono isiyo salama ya Salum Bausi aliyeshuka nayo. Coastal Union chini ya Hemed Morocco ilianza vizuri na hata kutamba kuwania nafasi tatu za juu, lakini imeishia nafasi ya sita huku mchezaji wake Nsa Job akikabiliwa na tuhuma za kupokea mlungula kutoka moja ya klabu kubwa.
Timu ndugu za Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, zote zikimilikiwa na kampuni ya Super Doll, zimejitokeza kuwa kiboko cha vigogo baada ya kutoa vichapo kwa nyakati tofauti. Kagera chini ya Abdallah Kibadeni ilishika nafasi ya nne ilhali Mtibwa chini ya Mecky Mexime iliishia nafasi ya tano.
Kagera Sugar na Mtibwa Sugar hazina ukata lakini pia hazina mafungu makubwa kwa ajili ya kufanya usajili wa wachezaji ghali wanaoweza kuzisaidia kutwaa taji la Ligi Kuu.
Katika kipindi chote cha ligi, hayakusikika malalamiko wala manung’uniko ya hali ya kambi kutoka timu za Jeshi la Kujenga Taifa kama Ruvu Shooting, Oljoro JKT, Mgambo na JKT Ruvu. 
Aidha, hayakusikika malalamiko kutoka Prisons iliyo chini ya Jeshi la Magereza wala Polisi Moro iliyo chini ya Jeshi la Polisi hadi imeshuka daraja.
Hata hivyo, ushiriki wa kusuasua na uwezo mdogo wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa umeziathiri. Kisheria, timu hizo hazipaswi kusajili wachezaji nyota kutoka nje ya nchi.
Timu hizo, ambazo kwa muundo ni kwa ajili ya kutoa burudani kwenye majeshi, zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika Ligi Kuu japokuwa kwa ushindani wa wastani tu. Ni mara chache sana zimekuwa na uwezo wa kuzifunga timu kubwa za Simba, Yanga na Azam ila humudu kutoa sare.
Mara nyingi ushindani fulani huonekana zinapokutana zenyewe. Wakati fulani zimekuwa na matokeo mazuri kwenye viwanja vya nyumbani na nyingine kama Mgambo imeponea chupuchupu.
Polisi Moro, Toto na African Lyon zimeshuka daraja na kwa utaratibu zimepisha nafasi kwa Ashanti United ya Ilala, Mbeya City na Rhino ya Tabora zilizopanda daraja. Nazo zisipokuwa na mafungu ya kusajili wenye uwezo au zikiendekeza migogoro kwa muda mrefu zitajikuta zikirejea daraja la kwanza.
MAKALA HII IMETOLEWA KATIKA GAZETI LA MAWIO, IMEANDKWA NA ELIUS KAMBILI

No comments:

Post a Comment