Search This Blog

Thursday, May 16, 2013

SIMBA VS YANGA: - KUJIAMINI KUNAWEZA KUKAIGHARIMU YANGA DHIDI YA WATANI WAO WA JADI

GUMZO lililotawala medani ya soka nchini ni pambano la funga dimba ya Ligi Kuu ya Bara litakalowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo itafanyika huku Yanga ikiwa tayari imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 57 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote inayoshiriki michuano hiyo. Mchezo huu utakuwa wa kulinda heshima tu kwani Simba haiwezi hata kutwaa nafasi ya pili.
Mashabiki wa Yanga wamejiaminisha kwamba mechi hiyo itakuwa ya kulipa kisasi cha kipigo cha mabao 5-0 ambacho ilikipata katika mechi ya mwisho msimu uliopita. Yanga wanajipa imani hiyo kutokana na mzozo ‘ulioko’ ndani ya Simba.
Siku chache baada ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hii, Simba haikuwa ikipata matokeo ya kuridhisha kiasi cha kutafuta mchawi. Uongozi ukawasimamisha wachezaji wake kadhaa kwa madai ya kuhujumu timu.
Wachezaji waliosimamishwa ni Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu, Amir Maftah, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Paul Ngalema, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Abdallah Juma. Lakini baadaye Kazimoto na Sunzu walisamehewa na kurejeshwa kundini.
Baada ya kuwasimamisha wachezaji hao ikaanza kuwatumia vijana kama Haruna Chanongo, Christopher Edward, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano ‘Messi’, William Lucian, Miraji Adam, Hassan Khatib na Jonas Mkude.

TAZAMA KINACHOITWA KIKOSI CHA WATOTO
Hivyo kikosi cha sasa cha Simba mara nyingi hujumuisha wachezaji; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Shomari Kapombe, Mussa Mudde, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa, Messi, Felix Sunzu, Mkude na Haruna Chanongo.
Mashabiki wa Yanga wanabeza wanakiita kikosi hicho cha watoto, hivyo wanajipa imani timu yao inaweza kuinuka na ushindi wa mabao mengi wakiwa na ndoto ya kurudisha mabao 5-0 waliyofungwa katika mechi kama hii mwaka jana.
Uchambuzi unaonyesha Simba haina watoto. Katika kikosi hicho kinachoitwa cha watoto, unaweza kuona wachezaji watatu tu chipukizi au wasio na majina makubwa ambao ni Messi, Mkude na Chanongo.
Wachezaji wanane waliobaki ambao ni Kaseja, Chollo, Shamte, Kapombe, Mudde, Kiemba, Ngassa na Sunzu, wote ni wazoefu na wanaoweza kubadili matokeo wakati wowote ule. Mbali ya wachezaji hao, Simba ina Kazimoto ambaye yuko kikosini japokuwa tangu arudishwe amecheza mechi chache.
Hata hao chipukizi watatu ambao kuna uwezekano mkubwa wakawepo kikosi cha kwanza cha Simba,  ni wazoefu kwani wapo katika kikosi hicho kwa msimu wa pili sasa. Kikosi hicho kinaweza kutoka sare na Yanga au hata kushinda.
Wachezaji wanaoweza kuihofia Yanga ni chipukizi ambao msimu huu wanaichezea kikosi cha kwanza cha Simba kwa mara ya kwanza wakiwemo Lucian, Miraji na Khatib ambao hata hivyo kuna uhakika mdogo mno wa wao kuwemo kikosi cha kwanza.

YANGA WAKIJIAMINI, WAMEISHA
Wakati Yanga wataingia uwanjani wakijiamini, Simba kwa upande wao wataingia dimbani kufanya mambo mawili; kwanza kuthibitisha uwezo wao, pili kuwatibulia Yanga ili washerehekee kukabidhiwa kombe na kichapo juu.
Tatizo kubwa la kikosi cha Simba kwa sasa linaweza kuwa ni saikolojia kwa wachezaji baada ya kukosa hata nafasi ya tatu; pia kutoelewana miongoni mwao. Hata kufanya vibaya kwa Simba katika mechi za kwanza za mzunguko huu, kulisababishwa zaidi na uongozi.
Simba ilifanya vibaya katika mechi zake za Kanda ya Ziwa, kwani ilikubali kipigo cha bao 1-0 na Kagera Sugar kisha  ikatoka sare ya mabao 2-2 na Toto African ya Mwanza. Huo ulikuwa wakati ambao baadhi ya wanachama wa timu hiyo walikuwa wakipambana kumtoa madarakani Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Katika mzozo huo Makamu mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ akajiuzulu. Mwingine aliyejiuzulu ni mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope, lakini sasa amerudi kundini.
Ghafla ‘watoto’ wa Simba chini ya Mfaransa, Patrick Liewig wakaanza kutoa darasa, wakailambisha JKT Mgambo 3-1, huku Yanga ikitoka sare na Coastal Union katika mchezo wake wa mwisho kabla ya kuivaa Simba keshokutwa.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts na benchi lote la ufundi la Yanga, wanapaswa kutoruhusu mawazo ya mashabiki na baadhi ya viongozi wanaoibeza Simba.
MAKALA HII IMECHOTWA KATIKA GAZETI LA MAWIO IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI

No comments:

Post a Comment