Search This Blog

Thursday, May 16, 2013

MAKALA: UTITIRI WA TIMU ZA JESHI LIGI KUU UTAZAMWE UPYA - FIFA HAIZITAKI KAMATI YA LIGI YAZILEA


KLABU mbili kongwe za Simba na Yanga ndizo zimetawala soka kwa miaka mingi na wapenzi nchini wamegawanyika katika timu hizo.
Shabiki wa soka anaweza kudai ni mpenzi wa Azam lakini ukweli ama yuko Simba au Yanga. Vile vile, atakayesema ni mpenzi wa Ashanti ndani kuna u-Simba au u-Yanga.
Pamoja na Simba na Yanga kuteka mashabiki wa soka nchini, klabu zinazomilikiwa na majeshi ndizo zinanogesha Ligi Kuu ya Bara inayomalizika keshokutwa. Ligi inashirikisha timu 14 msimu huu ambazo ni; JKT Oljoro, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mgambo JKT, Prisons, Polisi Morogoro, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Azam FC, Simba, Yanga, African Lyon, Coastal Union na Toto African.

TIMU SITA ZA JESHI LIGI KUU, HAZIONYESHI USHINDANI LAKINI ZA WENZETU NI BALAA
JKT RUVU

Timu sita kati ya hizo zinamilikiwa na majeshi. Jeshi la Polisi lina (Polisi Morogoro) na Magereza (Prisons) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linamiliki nne ambazo ni JKT Oljoro, JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Mgambo JKT.
Kwa tathmini yangu, tofauti na timu za majeshi kutoka nchi nyingine za Afrika hasa kutoka Afrika Kaskazini na Magharibi, ushiriki wa timu za majeshi ya Tanzania ni wa wastani katika ligi kiasi cha kutoweka hamasa ya kutosha ya ushindani. Miaka yote zimekuwa zikishika nafasi za katikati.
Azam FC, klabu inayomilikiwa na kampuni ya S.S.Bakhressa safari hii ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo baada ya kuitoa Al Nasri Juba katika raundi ya awali ilikumbana na timu ya Barrack Young Controllers ya Liberia ambayo inamilikiwa na jeshi la nchi hiyo. Azam ilitoka jasho kuitoa timu hiyo kwa mabao 2-1 na kuvuka hatua hiyo.
Hatua iliyofuata Azam ikapangiwa timu nyingine ya jeshi ambayo ni Association Sportive des Forces Armées Royales yaani FAR Rabat ya Morocco. Ulikuwa muziki ‘mnene’. Azam ililazimishwa sare ya bila kufungana na kisha ikatolewa mjini Rabat kwa 2-1.
Ukitazama kwa haraka, utaona timu zinazomilikiwa na jeshi kutoka nchi za Morocco, Algeria, Misri na Libya si nyingi katika ligi husika na nguvu kubwa ya maandalizi inakuwa ya kutosha tofauti na hapa nchini. Hali ni tofauti nchini.
JKT ina timu nne katika ligi kuu, pia ina timu katika Ligi Daraja la Kwanza zinazopambana kupanda daraja huku Polisi ikiwa na timu moja na mlolongo wa timu za daraja la kwanza. Hata Prisons nayo ina timu katika madaraja ya chini.
Mtigwa Sugar na Kagera Sugar ni timu ndugu zote zinalikiwa na kampuni ya Superdoll Group of Companies. Ushiriki wa timu hizo si haba.
Mlolongo huu wa timu zinazomilikiwa na kampuni moja au jeshi moja au mfadhili mmoja, ndio unazifanya taasisi hizi za serikali kushindwa kupata huduma nzuri kutoka kwa wamiliki wake ili kuwa na ushiriki wenye tija katika michuano hiyo.
JKT haiwezi kuzihudumia ipasavyo timu zake kuhimili ushindani kutoka kwa timu zenye nguvu ya fedha kama Simba, Yanga na Azam.

FIFA HAIZITAKI TIMU HIZO, TFF, KAMATI YA LIGI YAZILEA

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeona tatizo hilo na limeagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liangalie uwezekano wa kupunguza utitiri huo ili zisiathiri matokeo.
Kwa mfano sasa Mgambo inahitaji pointi moja tu ili iweze kubaki ligi kuu, tazama imecheza mechi mbili dhidi ya Simba na Azam na kufungwa mechi zote kwa mabao 3-1 na 3-0.
Kamati ya Ligi imejitahidi kupanga ratiba mechi za mwisho timu ndugu zisikutane, lakini zilipokumbana zenyewe katikati ya ligi hali ilikuwaje. Mechi za mwisho Mgambo itamaliza na African Lyon, Toto itakwaana na Ruvu, JKT Ruvu na Mtibwa Sugar, Prisons na Kagera Sugar, JKT Oljoro na Azam na Polisi itakuwa mwenyeji wa Coastal Union.
Ofisa mmoja wa JKT anayeshughulikia michezo anasema hilo la kuwa na timu moja katika ligi na kuiandaa kikamilifu hata wao wameliona lakini vyama vya soka vya mikoa ndivyo vinavyozing’ang’ania timu zao.
“Kwa mfano ukitaka Oljoro uivunje, Chama cha Soka Arusha (ARFA) kitakwambia hakitaki na wanahitaji timu ya ligi kuu na ukitishia kutoihudumia watakwambia wapo tayari kuihudumia. Hata mikoa mingine hali ni hiyo hiyo.
“Timu hizi zinakuwa zetu zikiwa madaraja ya chini lakini zikifika madaraja ya juu vyama vya soka vinazing’ang’ania kuwa nazo. Hatuwezi kukataa kuwa na timu kwani michezo ni miongoni mwa vitu tunavyovipa kipaumbele jeshini,” anasema ofisa huyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia anasema; “Ni kweli hizo timu zipo na hata Fifa hairuhusu timu mbili zinazomilikiwa na taaasisi moja kushiriki ligi kuu.”
“Kutokana na mazingira yetu ya soka hasa suala la kiuchumi, sisi tumeruhusu timu hizo kucheza ligi lakini tukiziangalia kwa karibu huku tukibana mazingira ya kupanga matokeo kuanzia katika ratiba na mambo mengine,” anasema.
Ligi Kuu ya Bara inafikia tamati keshokutwa Jumamosi huku Yanga itakayokwaana na Simba ikiwa imeshatwaa ubingwa baada ya kujikusanyia pointi 57.
MAKALA HII IMECHOTWA KATIKA GAZETI LA MAWIO IMEANDIKWA NA ELIUS KAMBILI

No comments:

Post a Comment