Search This Blog

Friday, March 15, 2013

ZFA YAITAKA TFF MEZA MOJA KUMALIZA TOFAUTI ZAO


CHAMA cha soka Zanzibar (ZFA) kimelitaka shirikisho la soka Tanzania (TFF) kukaa meza moja na serikali kumaliza tofauti zao.
Kauli hiyo imekuja, baada ya malumbano kati ya Serikali na TFF yaliyoibuka kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umesimamishwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa).
Fifa imesimamisha kufanyika kwa  Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa TFF, baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika kwenye shirikisho hilo na kutuma ujumbe kushughulikia kwa suala hilo.
Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji aliliambia Mwanaspoti jana jijini Dar es Salaam haoni sababu za msingi kwa viongozi wa TFF kurushiana maneno na serikali.
"Nafikiri TFF wakae meza moja na Serikali kumaliza tatizo hilo. Hilo ndilo jambo la msingi ambalo limebaki kwa sasa."
Naye Rais wa TFF, Leodgar Tenga jana alisema jijini Dar es Salaam kuwa TFF imepanga kukutana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara Machi 19, mwaka huu.
"Waziri ameshatuahidi kuwepo kikao hicho kati yake na viongozi wa TFF kwa lengo la kumaliza tatizo lililopo." alisema Tenga.
Haji alisema TFF inatakiwa kuelewa kuwa Fifa ni wasimamizi wa mchezo wa soka, lakini haiwezi kuendesha mchezo wowote nchini pasipo serikali kutia mkono wake.

No comments:

Post a Comment