Search This Blog

Thursday, March 21, 2013

WAKATI KIKWETE AKIPONDA UONGOZI WA SIMBA NA YANGA MWANAE RIDHIWANI APEWA UONGOZI YANGA

 DAKIKA chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuponda mfumo wa uongozi wa klabu kongwe chini zikiwemo Simba na Yanga, mtoto wake, Ridhiwani leo ametangazwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kitega uchumi cha Yanga katika eneo la makutano ya Mitaa ya Mafia na Nyamwezi, Ilala jijini Dar es salaam.

Kikwete akiwa katika uzinduzi wa kituo cha michezo cha Azam Complex huko Mbande Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, alisema viongozi wengi wa klabu hizo wapo kwa maslahi yao binafsi na si kuzinufaisha klabu.

“Hawa Azam hawana gozigozi katika utawala tofauti na klabu kubwa za hapa nchini na mimi nawaambia Azam sasa ni timu kubwa na inazisumbua sana hizo mnazoziita timu kubwa,” alisema Kikwete na kuongeza;

“Leo hii ninyi mna kituo cha kukuza vijana, wenzenu Simba na Yanga hawana kitu kama hiki, wamekalia ukiritimba tu siku zote na ndiyo maana hawafanikiwi.”


Kikwete aliyasema hayo leo mchana huko Mbande Chamazi, lakini katikati ya jiji la Das es Salaam kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga yalipo makao makuu ya Yanga, Mwenyekiti wa timu hiyo, Yusuf Manji alikuwa akimtambulisha Ridhiwani Kikwete kuwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kitega uchumi katika eneo la klabu lililopo makutano ya Mafia/Nyamwezi eneo la Ilala jijini Dar es salaam.

Manji alisema uteuzi wa Ridhiwani umezingatia uwezo wake kwa taaluma yake, na moyo alionao katika kujitolea katika kazi mbalimbali za klabu ya Yanga.

"Wote tunamfahamu Ridhiwani amekua ni mwanachama wa Yanga kwa muda mrefu, amekua akijitoa katika kazi mbalimbali za maendeleo ya klabu, hivyo tumeona ni vizuri kumpa fursa hiyo ili aweze kusaidia katika kuleta maendeleo ya klabu" alisema Manji

Katika kamati hiyo ambayo Ridhiwani ameteuliwa, amepewa fursa ya kuteua/kuchagua wajumbe atakaoshirikiana nao katika ujenzi wa kitega uchumi hicho, pia atakua na uwezo wa kuongeza wajumbe au kupunguza kulingana na mahitaji kwa kipindi hicho.

Mara baada ya kutambulishwa kwa wanachama na waandishi wa habari, Ridhiwani alisema anashukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuahidi kuwa atajitahidi kadri ya uwezo wake kuhakikisha ujenzi huo unafanikiwa.

"Nitakaa na kuangalia ni wajumbe gani ambao tutaweza kukaa pamoja na wajenzi (wakandarasi) ili kuweza kufanikiwa katika ujenzi wa kitega uchumi, kwani napenda eneo hilo liwe sehemu ambayo litasaidia katika uchumi wa klabu" alisema Ridhiwani



Ridhiwan
MASWALI TATA

Je, leo Kikwete amewaponda viongozi wa klabu kubwa nchini, na wakati huo huo mtoto wake anateuliwa kushika nafasi kubwa katika klabu, Ridhiwani ni mmoja kati ya viongozi waliopondwa?

Ridhiwani anaweza kumfanya baba yake ageuze au kupindua kauli yake aliyoitoa leo?

Je, maneno ya Kikwete yalihusiana na uteuzi wa Kikwete?

Au Kikwete alitamka bila kujua kama Ridhiwani amepewa uongozi Yanga?

Kazi kwenu!

3 comments:

  1. yeye mwenyewe yanga hayo yalikuwa maneno ya kwenye sherehe za uzinduzi tuu!

    ReplyDelete
  2. Hapa ndipo huwa natilia shaka umakini, weledi na busara za waandishi kama huyu anayeibua hoja zisizo na msingi.
    Hivi Ridhiwan bado no mtoto (kwa maana halisi ya mtoto au binadamu mwenye umri mdogo sema chini ya miaka 18) kiasi kwamba kila afanyalo lazima lifahamike na kupata ridhaa ya baba yake JK?
    Kwa nini mwandishi usitumie fursa hii kwa manufaa zaidi badala ya kuendeleza fikra za kufifisha na kukosoa kila jambo?
    Rais amekosoa menejimenti za klabu (sio za soka tu) kwa maslahi binafsi. Wanachofanya Manji na uongozo wote wa Yanga ni kuibadili - gradually and evolutionary taratibu za uendeshaji klabu kisayansi na kisasa zaidi. Wanawekeza mtaji ili klabu ijitegemee.Sasa JK akisikia mwanae kateuliwa kusimamia programu ya maendeleo kama hii ambayo ilishindikana tangu enzi za Gulam-Alli na wenzie, wallah atampongeza kila aliyelitia wazo lake (JK) kwenye vitendo.

    Waandishi jamani, nyie ni kioo cha jamii si kwa akili tu, bali kwa elimu,hekima,busara na weledi.
    Inaniuma sana.
    Manji; Ridhiwani; Rage na wengine wenye nia njema, endelezeni mageuzi katika vilabu vyetu, wachumia tumbo tukae pembeni.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kaka naona ulichukua mawazo yangu na ukayaweka kwenye ukurasa huu. mara nyingi wadau wamekuwa wakimshutumu shaffii juu ya umakini na uweledi wake juu ya tasnia ya uandishi. Kwa nafasi yake alitakiwa aweze kuliona hilo. Kikwete ana role yake kama Rais wa nchi Na Ridhwani ana nafasi yake. sioni tatizo kwa Ridhi kupewa nafasi hiyo eti kwa sababu Kikwete ameponda management za yanga na simba. Shaffih atajuaje anachokuja kukifanya ridhi? ni kama vile anamhukumu kwa kitu ambacho hata hakijafanywa. kwani haiwezekani wakaleta mapinduzi ya kweli katika klabu hizo? hata Kikwete alivyoponda klabu hizo hakuwa na maana hazifai zivunjwe ispokuwa alitoa changamoto ili klabu hizo zibadilike. na muda wa kuzibadilisha kwa manufaa ya Taifa ni sasa.

      Bonta Zyuma.

      Delete