Search This Blog

Sunday, March 24, 2013

TUNAWEZA KUKANA AMRI YA UPENDO KWA KUJIVIKA ROHO YA UZALENDO


Huwezi kunidanganya kirahisi kuhusu dini ya kiislamu wala ya kikristo. Namshukuru Mungu nimepata malezi na mafundisho ya dini zote mbili.

Mwalimu wangu wa madrasa hakuwahi kunifundisha jambo lolote lililo kinyume na maadili ya dini ya kiislamu, vivyo hivyo kwa walimu wangu wa dini ya kikristo.

Nilifurahia sana mafundisho ya dini ingawa mafunzo mengine yaliniwia vigumu kuyaelewa. Suala la kutoa sadaka lilikuwa gumu kwangu, kila nilipopigwa somo kuhusu utoaji nilijaribu kufumba macho huku nikiacha masikio wazi, yakasikia.

Sikuweza kuelewa mpaka nilipogundua siri ya kutoa sadaka. Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na matajiri wenzake ndiyo watu wanaoongoza kwa sadaka lakini masikini wengi ni wavivu wa kutoa sadaka.

Ahsante Mungu kwa kunifundisha hili la sadaka. Eeh mola wangu nisaidie na hili la upendo. ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako’, hii ni ngumu sana kwa binadamu wa leo, mitume wetu wa zamani wengi wao waliweza.

Padri atafundisha, Mchungaji atahubiri, Sheikh atatoa darasa lakini wengi wao hawaishi kwenye yao mafundisho. Kiufupi, hakuna mtu anayependa nafsi ya mwenzake kama au kuliko nafsi yake.

Hakuna akupendaye kama unavyojipenda mwenyewe. Wenzetu wamepiga hatua zaidi kwa kupenda kwanza vya kwao. Ukikipenda utakithamini, asikwambie mtu.

Muitaliano, Mjerumani na Muingereza, hawa watu huwaambii kitu kuhusu nchi zao, hata bidhaa zao. Kwa Mjerumani, Berlin ndiyo mji bora na mzuri kuliko yote duniani, Muingereza naye atakuambia London ndiyo mji bora duniani na hata Muitaliano atakwambia Roma ndiyo mji bora na mzuri kuliko yote duniani.

Hawa watu ni wazalendo kwa nchi zao, hawawezi kupenda vitu kutoka nchi nyingine wakati kwao vipo. Wamekubaliana kutokukubaliana na bidhaa nyingine kutoka nje ya kwao huku wao pia wakiitengeneza.

Hii ni nadra sana kutokea kwenye nchi za Afrika, hususani kwa mpenzi wetu Tanzania.

UNAJUA KWA NINI?

Watanzania wengi tuna mapenzi na vitu vya nje hasa Ulaya na sasa China kwa sababu tumekosa uzalendo. Hakuna Mtanzania anayeamini bidhaa ya hapa nchini. Ikiandikwa ‘Made in Tanzania’ kila mmoja atapaza sauti na kusema, hiyo ni feki na hata kama ina ubora atakwambia; Hiyo haina ubora unaoizidi ile ya ‘Made in China au USA.

Waafrika wengi wana roho za ugunduzi. Hawa wamepeleka mawazo yao nje ya Afrika yakafanyiwa kazi ikatengenezwa bidhaa kwa chapa ya nchi husika, kisha bidhaa hiyo ikaletwa Afrika ikauzwa kwa bei mbaya na ikapata wateja wengi. Lakini ingetengenezwa huku kwetu Tanzania na kuuzwa bei nafuu hiyo bidhaa isingenunuliwa.

Watanzania hatuna uzalendo sambamba na kutoaminiana na kujiamini. Hali hii inasababisha kupenda bidhaa za wenzetu, tena kuliko vyetu. Kupenda sana cha jirani tunaweza sisi tusio wazalendo.

Hii hali inaathiri hata soka letu. Heri yenu Waafrika Ryan Giggs, Thierry Henry, Mario Balloteli mliokulia Ulaya. Kiungo wa Yanga, Athuman Idd Chuji angekulia Ulaya angekua mzuri kuliko Abou Diaby. Straika wa TP Mazembe, Mtanzania Mbwana Sammata angezaliwa jijini Manchester, leo hii usingemsikia Danny Welbeck.

Tatizo letu si kwamba hatujui mpira, tatizo letu tumekosa mapenzi na uzalendo. Hatuamini bidhaa zetu za uwanjani jambo linalowavunja moyo wachezaji wetu.

Tatizo Wapo wengi wenye mioyo miyepesi, wataenda uwanjani huku wakiwa na matokeo yao ya kufungwa, wengine wamejiandaa kwenda kumzomea Juma Kaseja wa Simba au John Bocco wa Azam FC kama siyo Frank Domayo wa Yanga.

Wazalendo wachache wamefichwa na makupe ya wengi. Nchi ndogo kama Togo iliweza tena na wachezaji wengi wasio na majina, kwa nini sisi tunashindwa? Muda wetu siyo kesho, muda wetu ni leo, kesho yetu tunaijenga leo.

Na leo yetu ni sasa. Hakuna jambo lisilowezekana wala hakuna muda wa kusubiri tena, hebu na tuamini Arusha ni jiji bora na zuri kuliko yote duniani. Sahau umaskini wa watu wake, sahau kila kitu kibaya cha Arusha, penda na kuthamini kidogo tu cha thamani Arusha.

Amini kizuri hicho kidogo ndiyo kinafanya Arusha iwe bora kuliko mji wowote. Sahau yote yaliyopita, anza mwanzo mpya. Na wewe anza kujivunia kuwa Mtanzania, hebu jivunie cha kwako.

Acha kupaza sauti kwenye vibanda umiza maana Wayne Rooney na Lionel Messi hawakusikii, hebu kapige kelele Uwanja wa Taifa Jumapili ya 24 Machi, 2013 pale Taifa Stars itakapovaana na Morocco katika mchezo wa awali wa Kombe la Dunia 2014.

Ukipaza sauti pale, kiungo chipukizi Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ atasikia sauti yako na atakupa cha kujivunia kama Mtanzania. Sure Boy atajituma kwa kusikia sauti yako na kuiletea ushindi Tanzania.

Nia tunayo na uwezo tunao, hebu twendeni kwa pamoja na kwa umoja tukawaonyeshe Wamorocco kama sisi ni Watanzania.
NCHI MOJA, TAIFA MOJA, HATMA MOJA,

TIMU MOJA YA TAIFA..

NAJIVUNIA KUWA MTANZANIA
Mimi Kaijage Jr..
Middle ya juu



10 comments:

  1. Daah, nimeipenda sana Huo ni ukweli mtupu naipenda tz

    ReplyDelete
  2. umesema kweli mkuu,ni jukumu letu kama washabiki kutimiza wajibu wetu kuishangilia timu kwa nguvu zote na siyo kusubiri mchezaji akosee ndio tupate la kusema,linapokauja swala la timu ya taifa tuache usimba na uyanga au kusubiri mchezaji wa azam kakosea basi mashabiki wa simba tunasema angecheza chanongo pale asinge kosea,bila hiyo siyo sahihi,uzalendo kwanza vingine baadae.

    ReplyDelete
  3. Hili neno uliendelezwe hata wewe una nafasi ya kulijenga taifa letu

    ReplyDelete
  4. mpaka ccm itoke madarakani ndo tutarudisha uzalendo baba!!! kikwete na ccm wameshatueonyesha kuwa nchi hii ni ya kwao na wengine ni vibarua tu

    ReplyDelete
  5. Hii imekaa vizuri,tena vizuri mno.asante mdau mwanamichezo!

    ReplyDelete
  6. Hay is mane no ya kawaida kwanza yanaumiza na kufundisha.....naomba yarushwe kwenye radio

    ReplyDelete
  7. kuwa na akili wewe...kikwete na ccm yake imekuja wapi kwenye mada hii. kwani huyo aliopo akilini mwako ndio atasababisha uwe mzalendo? mwanasiasa ni mwanasiasa na mwanamichezo ni mwanamichezo. wanasiasa na nyie vibarua wao mtuachie maada zinazotuhusu sie wanamichezo.. maneno yaliopo kwenye waraka huu unatufaa sie wapenda michezo kwani ndio wenye mapenzi ya kweli na tunavyovipenda.
    mtazamo: yeyote atakayeongelea siasa katika maada zetu za michezo maoni yake yazuiliwe.

    ReplyDelete
  8. nimeipenda sn hiyo article hapo juu,umeeleza kitu muhim sana ambacho kila mtan
    zania anapaswa kuwa nacho moyoni juu ya nchi yetu,bila kuipenda nchi yetu hatu
    wezi kuibadili na kuwa kama hizo nchi tunazozisifu tuanze sasa kuwa na moyo huo yote tunayopigania tutafanikiwa.BIG SANA MIDDLE YA JUU KEEP IT UP

    ReplyDelete
  9. Duu ccm tena imekujaje hapo mdau unahasira balaa

    ReplyDelete
  10. huyo Gabriel alloyce hayupo timam bila shaka

    ReplyDelete