Search This Blog

Wednesday, March 20, 2013

HUU NDIO UNDANI YA MARIDHIANO YA TFF NA SERIKALI KUHUSU UCHAGUZI WA TFF

HATIMAYE Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, zimekubaliana ujumbe kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kufika nchini muda wowote kuanzia sasa na kufanya mapitio upya (review) kwa wagombea walioenguliwa katika mbio za uchaguzi wa TFF.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga, leo hii amesema kimsingi wamekubaliana na wizara baada ya kikao cha jana kilichowaushisha Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fennela Mukangara, naibu wake, Amos Makalla, Tenga na viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kwamba Fifa waje kufanya review halafu uchaguzi uendelee.
“Tumeangalia mambo mengi ya msingi kwa mustakabali wa mpira wa miguu Tanzania, tuna  heshima kubwa ya uongozi bora katika soka duniani. Hivyo tusingependa sifa hii ipotee kienyeji, ndiyo maana TFF, wizara na BMT tulikutana na kukubaliana kwamba, Fifa waje kufanya review ya kile kilichotokea halafu majibu yakipatikana tuendelee na uchaguzi,” amesema Tenga.
 Tenga amesema, wamefikia uamuzi kwa kuwafikiria pia Watanzania wapenda michezo na hata wagombea ambao wana haki ya kupigiwa kura huku wakiwa hawahusiki na hiki kinachoendelea sasa.
“Kuna watu hawahusiki na jambo hili kwa namna yoyote ile, sasa hawa tumewafikirai sana na tumeamua tuwape haki yao haraka iwezekanavyo. Nina imani nchi itabaki kuwa salama katika soka na upepo huu utapita,” amesema Tenga.
Awali Tenga alikuwa ameridhia kufanyika kwa review za mapingamizi ya wagombea mbalimbali wa TFF, lakini ushauri wake huo ulitupwa mbali na Kamati Huru ya Uchaguzi ya TFF na ile ya Rufaa. Baada ya hapo, ndipo serikali ikaiagiza TFF kufuata katiba ya mwaka 2008 baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya wagombea walioenguliwa.
Baadhi ya wagombea waliochinjwa katika uchaguzi huo ni Jamal Malinzi anayewania nafasi ya rais, Michael Wambura anayewania nafasi ya makamu wa rais ma wengineo.

TENGA AKATAA KUZUNGUMZIA KATIBA

Katika hali ya kushangaza, Tenga alikataa kujibu maswali ya waandishi wa habari yaliyokuwa yakihoji kuhusu katiba itakayotumika katika uchaguzi huo baada ya awali serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuigiza TFF kutumia katiba ya mwaka 2008 na kuiacha ile ya 2012 inayoelezwa kupitishwa isivyo halali.
“Jamani swali kuhusu katiba sitalijibu hapa, hapa tunazungumzia uchaguzi na mambo mengine yahusuyo,” amesema Tenga na hata aliposisitizwa kuhusu umuhimu wa swali hilo, alijibu: “Hapa si mahala pake jamani.”

SERIKALI YAZIDI KUIKOMALIA TFF

Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi alisisitiza kwamba, Fifa watafika nchini na kufanya review yao kisha wao kama wasimamizi wa serikali wataipitia ripoti ya kazi hiyo kisha kuitolea maamuzi zaidi.
“Tumekubaliana hapa kwamba Fifa waje kufanya review, hawa mabwana wakimaliza kazi yao sisi tutaiangalia na kutazama kama haki imetendeka halafu ndipo tutaruhusu taratibu za uchaguzi kuendelea,” amesema Malinzi.
Malinzi alisema, kimsingi kikao chao na wizara na TFF kilikuwa cha amani na ana uhakika mambo yataenda vizuri na kila mmoja atapata haki yake ipasavyo.
FIFA WANAKUJA, UCHAGUZI SI ZAIDI YA MEI 25

Tenga baada ya maafikiano hayo, TFF itaiandikia Fifa ambao ndiyo wanaosimamisha mchakato huo ili watume wajumbe wake kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.
Tenga ambaye ameishukuru Serikali kwa kuruhusu mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali, na kuwa haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza uchaguzi ufanyike kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. Fifa wakija hata kesho wakituambia endeleeni sisi tuko tayari. Hesabu zetu ziko tayari, makabrasha yote yako tayari yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa muda tu kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita ghafla,” amesema Tenga.
Amesisitiza kuwa TFF ilishapanga tarehe ya uchaguzi, lakini ukasimamishwa na Fifa baada ya baadhi ya walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi kwa sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani haya maana hata kidogo.

WAGOMBEA KUHOJIWA NA FIFA NA KAMATI YA RUFAA

Tenga amewataka wagombea wote waliofika kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa vizuri, kwani Fifa watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina heshimu Serikali na itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu FIFA sababu iko kwenye mpira wa miguu, na FIFA ndiyo wasimamizi wa mchezo huo duniani. 
Amewakumbusha wanachama wa TFF, hasa wajumbe wa Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina katiba, lakini ni lazima pia wafahamu kwanini kuna Fifa.

5 comments:

  1. Chonde chonde malinzi Haki isiwe kuhakikisha bwana mdogo jamal anarudishwa kugombea, wache watu wafanye kazi kwa uhuru.

    ReplyDelete
  2. Dalili mbaya kwa tenga kushindwa kujibu swali linalohusu katiba

    ReplyDelete
  3. Kwanza waandishi wa habari walio uliza swali la KATIBA ni "MAKASUKU"! Toka hili suala lianze mpaka hapa lilipofikia naapata wasiwasi na ugumu wakuamini kwamba tatizo ni KATIBA. Nikijaribu kujiuliza Wambura na Jamali Malinzi pamoja na wagombea wengine walianza mchakato huu kwakutumia KATIBA gani? Malinzi alipitishwa na Kamati ya uchaguzi ambayo kamati hiyohiyo aliwapiga chini wagomea wengine kama Wambura, Omary Nkwaruro,na Shaffih Dauda lakini hawa wote walikata rufaa kwenye kamati ya Rufaa ambayo kwa kumbukumbu zangu Shaffih alifanikiwa kupita lakini Nkwaruro na Wambura wakabaki na ni Kamati hii ndio iliyopokea pingamizi za Malinzi na ndipo Jamal Malinzi alipoondolewa na utata kuanza kujitokeza. Maswali ninayojiuliza, WADAU wa mpira wakiwemo wanachama wa TFF/Vyama vya soka vya mikoa, waandishi wa Habari, wachambuzi wa soka, serikali yenyewe na wale wote wanainyoshea vidole KATIBA ya 2012 walikuwa wapi kabla ya kuenguliwa MALINZI? Je, MALINZI angepita katiba ingekuwa HARAMU? Mimi kwa mara ya kwanza kumsikia Mh. Makala naibu waziri akizungumzia hili suala akiwa jimboni nilimuelewa vizuri sana maana alitoa mawazo kama mtu wa kawaida na si kwa nafasi yake ya Unaibu Waziri (ingawa ningumu kutofautisha mwazo yake kama mtu binafsi na pale anapotoa mawazo kama Naibu Waziri). Kinachonifanya niwe na wasiwasi nipale ninapoliona hili suala kuwa linautata pale tu MTU/WATU flani walipoenguliwa. Je, hawa wadau wanaoulizia KATIBA walikuwa wapi kabla ya hapo? Kiukweli bado sijapata jibu la kunilizisha kama mwenye jibu yupo naomba anisaidie ila kwa sasa bado naamini TFF wako sahihi na Serikali pamoja na wote wanao inyoshea Vidole KATIBA ya 2012 hawana hoja na kama wanayo hoja basi wameijenga katika misingi ya UBINASFI na si kuokoa na kuendeleza soka letu.

    ReplyDelete
  4. TANGU MWANZO NILIKUWA NASHANGAA SERIKALI ILIINGIAJE KATIKA MGOGORO HUU.KIMSINGI HUU MGOGORO ULIKUWA KATI YA TFF NA UKOO WA MALINZI,SASA HAWA JAMAA NI WAJANJA WAJANJA NA WANA FEDHA HIVYO WAKAITUMBUKIZA SERIKALI KATIKA MGOGOROHUU BILA KUJIJUA.MBAYA ZAIDI WAANDISHI WA HABARI NAO WAKATUMBUKIZWA.KWA KAWAIDA MSHAURI MKUU WA WAZIRI NI KATIBU MKUU KWA KUWA YEYE NDIYE MTAALAMU NA ANAO WATAALAM CHINI YAKE.NAIBU WAZIRI NI MSAIDIZI MKUU WA WAZIRI KATIKA MASUALA YA KIWAZIRI,SIYO MSHAURI MKUU WA WAZIRI KAMA ILIVYOPOTOSHWA KATIKA SAKATA HILI.YEYE SIYO MTAALAM,NA NDIYO MAANA ALIMPOTOSHA WAZIRI WAKE KWA KUWA ALIPATA USHAURI TOKA KWA WAPAMBE BADALA YA WATAALAM.

    ReplyDelete
  5. Hakuna namna ya kukwepa kutumia katiba ya mwaka 2012,kwa sababu mchakato umefanyika chini ya katiba hiyo na kanuni za uchaguzi zilizoandaliwa chini ya katiba hiyo.Sasa kama FIFA watakuja na kuamua kama ilivyoamua kamati ya Mtinginjola halafu uamuzi huo upelekwe serikalini ukajadiliwe kwanza hapo si itakuwa kuingilia masuala ya soka?au ni mtego aliotegewa Tenga kwa kuwa tayari atakuwa ameandika barua FIFA KWAMBA MGOGORO UMEKWISHA?Halafu kutokana na conflict of interest, huyu Dionizi Malinzi kuanzia sasa hapaswi kushiriki kwenye vikao vinavyofuata sababu kwa sababu sakata la katiba limekwisha na vikao vinavyofuata vitahusu nafasi ya jamal malinzi katika uchaguzi mkuu wa tff

    ReplyDelete