Search This Blog

Friday, March 8, 2013

HII NDIO MIFUMO YA TIMU ZOTE ZA LIGI KUU NA NA SABABU KWANINI MAKOCHA WANAITUMIA


KILA kocha wa soka ana falsafa yake ya ufundishaji, lengo likiwa kushinda kila mechi na kufikia malengo ambayo amejiwekea.

Pia, katika soka kuna mifumo mingi na tofauti ya uchezaji ambayo huendana sana na aina ya wachezaji wa timu husika.

Baadhi ya mifumo ambayo imezoeleka katika soka la sasa ni 4:4:2, 4:3:3 na 4:5:2.

Makala haya yanakuchambulia timu zote 14 zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na mifumo yake.

YANGA SC

Mfumo; 4:4:2
YANGA hucheza mfumo wa 4-4-2, lakini Mholanzi Ernie Brandts amekiri kuwa mambo yanapokuwa magumu hubadilika na kucheza 4-3-3.

"Kwa kawaida huwa tunacheza 4-4-2. Lakini mambo yanapoharibika tunalazimika kutumia fomesheni ya 4-3-3." Brandts anaeleza kuwa anapotumia mfumo wa 4-3-3 hushambulia zaidi kutokana nakucheza na washambuliaji watatu ambao ni Jerry Tegete, Said Bahanuzi na Himis Kiiza.

"Wakati tunapokuwa kwenye mfumo wetu wa 4-4-2 tunafanya yote kwa pamoja. Kushambulia na vile vile kujihami kufungwa kirahisi." anasema kocha huyo aliyevaa viatu vya Mbelgiji Tom Saintfiet aliyetupiwa virago na Yanga.

SIMBA SC

Mfumo; 4:3:3
MFARANSA Patrick Liewig ameeleza kuwa tangu ametua na kuanza kazi ya kukinoa kikosi cha Simba akichukua mikoba ya Mserbia Milovan Cirkovic ameona mfumo 4-3-3 ndio ambao Simba wameonyesha kufiti tofauti na 4-4-2.

"Nilipokabidhiwa timu nilijaribu kutumia mifumo tofauti. Lakini nafikiri 4-3-3 ni bora zaidi kwetu." anasema kocha huyo. Liewig anafafanua kuwa aina ya wachezaji ambayo wanaunda kikosi cha Simba ni sahihi kucheza mfumo wa 4-3-3 kuliko 4-4-2.

AZAM FC

Mfumo;4:3:3
MWINGEREZA Stewart Hall ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo amefichua kuwa hucheza 4-3-3, ingawa wakati mwingine hubadilika na kutumia 4-4-2.

"Mara kwa mara tunacheza 4-3-3, lakini wakati mwingine tunapaswa kubadilika kutokana na mpinzani wetu anavyocheza."

Stewart anaeleza kuwa anapobadilisha fomesheni hucheza 4-4-2.

"Kwa aina ya wachezaji ambao ninao kwa sasa, nafikiri mfumo sahihi kwetu kucheza ni 4-3-3." anasema kocha huyo aliyetemwa na kurejeshwa kwa

mara nyingine kukinoa kikosi hicho.

MTIBWA SUGAR

Mfumo; 4:5:1
MECKY Maxime ambaye ni kocha mkuu wa Mtibwa anasema hutumia mfumo wa 4:5:1, lakini wakati mwingine hubadilika na kucheza 4:3:2:1.

Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars anaeleza kuwa lengo la kucheza 4-3-2-1 ni kutanua uwanja na kufanya mashambulizi mengi kusaka ushindi.

"Mara nyingi tunavyotumia mfumo wa 4-5-1. Tayari tumeshinda kwa hiyo tunataka kulinda ushindi wetu na kumiliki mpira." anasema kocha huyo.

COASTAL UNION

Mfumo; 4:3:3
KOCHA Mkuu, Hemed Morocco anasema hutumia mfumo 4-3-3 kwa lengo la kutanua Uwanja na kufanya mashambulizi yake kupitisha mipira pembeni ya uwanja.

"Nafikiri timu ambazo zinafanya vizuri duniani kwa sasa zinatumia zaidi mawinga wake kutengeneza ushindi. Pia, kwa aina ya wachezaji ambao ninao, nafikiri nalazimika kucheza 4-3-3." anasema Morocco aliyerithi mikoba ya Juma Mgunda aliyejiuzulu kukinoa kikosi hicho kwa shinikizo la wanachama na mashabiki wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara 1988.

Coastal inawatumia mawinga wake wawili, Daniel Lyanga na Seleiman Kassim 'Selembe' ambao wana uwezo mkubwa pia wakufunga mabao.

JKT RUVU

Mfumo; 3:5:2
NI moja kati ya timu ambazo zinasifika kwa soka la pasi fupi na kushambulia kama nyuki. Soka la JKT Ruvu halitofautiani sana na la Kagera Sugar.

Kocha Charles Kilinda anasema hana mfumo maalum wakutumia isipokuwa hutegemea na timu ambayo anakabiliana nayo.

"Sina mfumo maalum wakutumia isipokuwa nacheza kulingana na mpinzani wangu anavyocheza na aina ya wachezaji wake."

Kilinda anafafanua kuwa mara nyingi hutumia mfumo wa 3-5-2, Pia, wakati mwingine hubadilika na kucheza 4-4-2.

KAGERA SUGAR

Mfumo; 4:4:2
MRANGE Kabange ambaye ni kocha msaidizi wa Kagera Sugar anasema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitumia mfumo wa 4-4-2.

"Ni mfumo ambao wachezaji wetu wameonyesha kuushika vizuri na kumudu tofauti na mifumo mingine tunapojaribu kucheza." anasema kocha huyo.

Kabange anafafanua maana ya kucheza mfumo huo ni timu iweze kucheza soka la pasi fupi.

"Falsafa yetu ni kucheza soka la pasi fupi. Kwa maana hiyo lazima tucheze tukiwa karibu. Mipira ya juu kwetu mwiko." anasisitiza.

RUVU SHOOTING

Mfumo; 4:5:1
KOCHA mkuu, Boniface Mkwasa anasema lengo lake kutumia mfumo huo ni kuiteka sehemu ya katikati ya Uwanja.

"Falsafa yangu kubwa ni kucheza na viungo watano katikati ya uwanja."

Mkwasa anasema anaamini akiweza kutawala sehemu ya kiungo inakuwa kazi rahisi kwa timu yake kujenga mashambulizi ya kusaka ushindi. Pia, anasema inapotokea timu yake imebanwa hubadilisha mfumo na kucheza 4-4-2.

OLJORO JKT

Mfumo; 4:2:3:1
KATIBU wa Oljoro, Alex Mwamgaya ambaye kwa sasa anashirikiana na kocha msaidizi, Fikiri Edward kukinoa kikosi hicho anasema timu hiyo anatumia mfumo wa 4-2-3-1.

"Nafikiri mfumo ambao tunatumia ni kwa ajili ya kujihami na vile vile kushambulia."

Mwamgaya anaeleza kuwa mabeki wanne na viungo wawili wakabaji kazi yao kubwa ni kuhakikisha timu hairuhusu bao kirahisi.

Anasema kazi ya viungo watatu ni kuunganisha timu kutoka nyuma na kwenda mbele kushambuliaji.

"Majukumu yao ni mawili, kutengeneza nafasi za kufunga na pia kufunga inapotokea nafasi."

TANZANIA PRISONS

Mfumo; 4:2:3:1
KOCHA mkuu, Jumanne Chale aliyeinoa African Lyon msimu uliopita, anasema wacheza mfumo wa 4-2-3-1.

"Lengo letu ni kuhakikisha hatufungwi kirahisi. Pia tunashambulia." Chale aliyerithi mikoba ya Stephen Matata aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu msimu huu anaeleza kuwa mara nyingine hubadilika kutokana na timu anayokabiliana nayo.

"Wakati mwingine tulazimika kubadilika kulingana na mpinzani wetu."

Anasema anavyobadilika hucheza 4-4-2 na mara nyingine 4-3-3.

MGAMBO JKT

Mfumo; 5:3:2
KOCHA mkuu, Mohamed Kampira aliyerithi mikoba ya Stephen Matata anasema anatumia mfumo wa 5-3-2.
"Silaha yetu kubwa ni kushambulia na kurudi nyuma kwa pamoja kujilinda."

Kampira anaeleza kuwa lengo la kutumia fomesheni hiyo ni wasifungwe kirahisi, lakini timu yake ishambulie.

TOTO AFRICAN

Mfumo; 4:4:2
TANGU Toto imeanza kushiriki Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2.

Kocha msaidizi, Athuman Bilali 'Bilo' anasema mfumo huo umekuwa rahisi kwao kulingana na aina ya wachezaji wanaounda timu hiyo.

"Kila mwalimu anatumia mfumo wake kulingana na aina ya wachezaji alionao." Bilo anaeleza ni vigumu leo ukaitaka Chelsea icheze kama Arsenal.

"Lazima kuwe na maandalizi. Huwezi kukurupuka usingizini na kubuni fomesheni. Leo tucheze 4-3-3, kesho 5-3-2." anasisitiza kocha huyo.

AFRICAN LYON

Mfumo; 4:4:2
MKURUGENZI wa Ufundi, Charles Otieno anasema timu hiyo inatumia mfumo wa 4-4-2. Lakini mambo yanapokuwa magumu hugeuka na kutumia 3-5-2.

"Fomesheni yetu ni 4-4-2, Lakini inapotokea kumeshikwa tunageuka na kutumia 3-5-2. Nafikiri kila mwalimu lengo lake ni kupata ushindi kila mechi."

Otieno anafafanua kuwa timu hiyo inapotumia mfumo wa 4-4-2 hushambulia na pia kujihami.

"Tunapogeuka na kucheza 3-5-2. Lengo letu huwa ni kushambulia kuliko kujilinda."

POLISI MORO

Mfumo; 4:4:2
KOCHA mpya, Adolf Rishard anasema tangu ameanza kazi ya kuinoa Polisi Moro anacheza katika mfumo wa 4-4-2.

"Mifumo ni mingi ya uchezaji, lakini inategemea sana na aina ya wachezaji ulionao." anasema kocha huyo aliyerithi mikoba ya John Simkoko aliyetupiwa virago na Polisi kushindwa kupata ushindi ngwe yote ya kwanza ya ligi.

Rishard anasema mfumo ambao anacheza ni 4-4-2 kulinga na aina ya wachezaji wanaounda timu yake.

"Kwa kiasi kikubwa fomesheni ya 4-4-2 imenipa mafanikio makubwa."

Polisi imeshinda mechi mbili za kwanza, mzunguko wa pili wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na African Lyon ambapo imefikisha pointi 10.

3 comments:

  1. ni timu nyingi na mifumo inayo jirudia lakini si dhani kama wanaenda sambamba na timu ya taifa ili kumrahisihia kocha wa taifa ufundishaji nafikiri imefika wakati iwe lazima kufundisha mfumo wa timu ya taifa na mfumo mwingine unatakiwa natimu

    ReplyDelete
  2. Mifumo inaweza kuwa na jina moja lakini inapishana. Kwa mfano 4-4-2 inaweza kuwa flat 4-4-2, diamond 4-4-2, 4-1-3-2, 4-3-1-2, 4-2-2-2 nk. Kila kocha ana falsafa yake na mfumo wake lakini timu nyingi hujikuta zinacheza 4-4-2 kwa sababu ni mfumo rahisi kuufundisha. Kwa mtizamo wangu binafsi timu zenye kucheza 4-2-3-1 zimekuwa na mafanikio mazuri zaidi kwa sababu zinaweza kuwa na timu zenye urari. Panakuwa na wachezaji wa kutosha wanashambulia na kujihami.

    ReplyDelete
  3. Sidhani kama ni sawa kuwalazimisha makocha,kutumia aina fulani ya mfumo, taifa linahitaji philosophia tu,mambo ya mifumo,ni uwezo wa wachezaji kubadilika,ndio hasa kuwa mchezaji mzuri wa taifa! mi naona huyo Maxime, azaminiwe akasomee ukocha aje apewe timu ya taifa, maana ameonyesha kuwa na mawazo ya kujitegemea sana!

    ReplyDelete