Search This Blog

Friday, February 22, 2013

YANGA VS AZAM FC - NANI KUKAA KILELENI - VITA YA KAVUMBAGU DHIDI YA KIPRE TCHETCHE

LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 23 mwaka huu) kwa mechi tatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Uwanja huo wa kisasa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na makamu bingwa Azam. Ingawa Azam imecheza mechi moja zaidi, lakini timu hizo zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye msimamo wa ligi huku kila moja ikiwa na pointi 36.

Pia vinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa wanatoka katika timu hizo mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao tisa hadi sasa ndiye anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao manane.

Iwapo timu yoyote itafanikiwa kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, kasi ya mbio za kuwania ubingwa itaongezeka. Waamuzi wasaidizi watakuwa Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye kutoka Mbeya wakati mezani atakuwepo Oden Mbaga.

Mechi nyingine za kesho ni Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Jumapili (Februari 24 mwaka huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa katika hekaheka nyingine kwa Simba chini ya Mfaransa Patrick Liewig kuikabili Mtibwa Sugar inayonolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.

1 comment:

  1. prison vs polisi morogoro siyo polisi dodoma naona kuna error kidogo hapo kaka shaffih

    ReplyDelete