Search This Blog

Friday, February 1, 2013

PAMOJA NA KUPATA USHINDI MARA MBILI MFULULIZO KOCHA WA AZAM HAJARIDHIKA NA KIWANGO CHA TIMU


KOCHA wa Azam FC, Stewart Hall amesema bado hajaridhishwa na safu yake ya ulinzi, licha ya kupata ushindi katika mechi mbili za awali. 
Azam FC imeshinda mechi mbili za kwanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na Toto African na kuweka 'gap' la pointi mbili dhidi ya vinara Yanga yenye pointi 32 kibindoni.
Stewart aliliambia shaffihdauda.com baada ya mtanange huo kumalizika kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi kuwa pamoja na timu yake kushinda mechi mbili za awali kwa idadi ya mabao 3-1 kila mchezo, bado ana changamoto kubwa kuisuka safu yake ya ulinzi.
Mwingereza huyo alisema; "Nafikiri timu imeimarika kwa kiasi kikubwa. Lakini tuna tatizo sugu kwenye ngome yetu."
"Ukijaribu kufuatilia magoli mawili ambayo tumefungwa kwenye kila mechi dhidi ya Kagera na Toto hayana tofauti kubwa." alisema kocha huyo.
Alieleza kuwa mabeki wake wa kati Mkenya Jockins Atudo na Mtanzania David Mwantika kuna wakati wanajichanganya na kutoa mwanya kwa wapinzani kufunga mabao rahisi.
"Bado sijaridhishwa na uchezaji wao. Nimekuwa nikiwakumbusha kila wakati, lakini bado tatizo hilo wanalirudia." alisema Stewart.  
Aliongeza kuwa ni changamoto kwake kulifanyia kazi tatizo hilo na kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara.
Azam FC imewasimamisha wachezaji wake wanne kwa tuhumu za kuchukua rushwa kwenye pambano dhidi ya Simba mzunguko wa kwanza wa ligi.
Nyota hao ni kipa Deogratius Munishi na mabeki Aggrey Morris, Said Morad na Erasto Nyoni. 

No comments:

Post a Comment