Search This Blog

Monday, February 18, 2013

CHEKA: "NIPO TAYARI KUPIMWA ILI NITIHIBITISHE SITUMII DAWA ZA KUONGEZA NGUVU"

BINGWA wa uzani wa super middle wa mkanda wa IBF Afrika, Francis 'SMG' Cheka amebainisha kuwa yuko tayari kupimwa bangi na kusisitiza hata kama anatumia bado anajitambua kama bingwa.
 

"Sina tatizo kupima kama ningekuwa natumia dawa za kuongeza nguvu ningeshagundulika miaka mingi lakini nimecheza nchi mbalimbali za Ulaya na kote nilipimwa sikukutwa natumia," alisema Cheka.
 

Cheka anayejiandaa kutetea taji lake la IBF katika pambano litakalopigwa Mei Mosi kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam dhidi ya Thomas Mashali alibainisha kuwa mabondia wengi wanatumia bangi lakini si dawa ya kuongeza nguvu. 
 
"Cha muhimu ni kujilinda kwani mabondia wengi ni 'wahuni' na wengi wanatumia bangi hivyo hata kama mimi ni mmoja wa wanaotumia bado najitambua na niko tayari kupima," alisema Cheka.
 

Bondia huyo ambaye atalazimika kupima endapo anatumia dawa za kuongeza nguvu ikiwamo bangi sambamba na mpinzani wake (Mashali) alisema matumizi ya bangi kwa mabondia ni kitu cha kawaida.
 

"Hata hivyo sina 'presha' ya kupimwa kwani hata kama ningekuwa natumia ingenilazimu kuacha ili niweze kutetea taji langu, nasisitiza tena ninachokifanya kwenye ndondi nakijua cha muhimu ni kujitambua kwani inaweza kutokea kwa bondia yoyote si kwa Cheka," alibainisha mkali huyo wa masumbwi Afrika.
 

Kwa mujibu wa rais wa IBF Afrika, Onesmo Ngowi kabla na baada ya pambano hilo, Cheka na Mashali watafanyiwa vipimo kubaini endapo wanatumia dawa za kuongeza nguvu na bangi.
 

Ngowi alibainisha kuwa vipimo hivyo vitafanyika siku moja kabla ya pambano na dakika chache baada ya pambano na ikibainika mmoja kati yao anatumia hatua kali zitachukuliwa dhidi yake na kama atakuwa ameshinda atanyang'anywa ubingwa.

No comments:

Post a Comment