Search This Blog

Thursday, February 21, 2013

AZAM FC YATUMA MASHUSHU SUDAN KWA AL NASR

WAKATI klabu ya Azam ikituma 'mashushu' nchini Sudan Kusini, Serikali imewahakikishia wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la Shirikisho, usalama wao kwa kipindi chote watakachokuwa Sudan Kusini.

Azam itacheza mechi ya marudiano na timu ya Al Nasri ya nchi hiyo kati ya Machi 2 na 3, mchezo utakaopigwa mjini Juba nchini humo.

Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alikiri kuwepo kwa vita baina ya Sudan na Sudan Kusini licha ya kuwahakikishia Azam usalama wao.

" Azam iwe na amani kwani mapigano hayo yanafanyika mbali na mahali itakapochezwa mechi hiyo," alisema Waziri Membe katika mahojiano na Mwananchi.

Kwa mujibu wa Membe mapigano hayo yanafanyika mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini ambako ni mbali na Juba itakapochezwa mechi hiyo ya kimataifa.

"Juba ni mbali na yanapofanyika mapigano na shughuli zinaendelea kama kawaida hakuna tofauti na Dar es Salaam kuna amani ya kutosha," alisema Waziri Membe.

Akifafanua umbali wa kutoka Juba hadi yanapofanyika mapigano hayo Waziri Membe alisema ni sawa na Dar es Salaam na Songea.

"Cha msingi Azam ijiandae kikamilifu kwa ajili ya kupeperusha vema bendera ya Tanzania bila kuwa na uoga wowote zaidi wazingatie nidhamu ya ndani na nje ya uwanja kwenye mechi yao.

Azam inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-1 kwenye mechi yao ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo klabu ya Azam itaweka kambi nchini Uganda kabla ya kuondoka kwenda Sudan Kusini kwenye mechi yao ya marudiano.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall alisema timu hiyo itaondoka kati ya Jumatatu na Jumanne kwenda jijini Kampala itakapoweka kambi hiyo ikiwa ni baada ya mechi yao ya kesho dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

"Mechi yetu na Yanga itakuwa kipimo cha mwisho kabla ya kwenda Uganda," alisema kocha huyo raia wa Uingereza.

Kwa mujibu wa Hall, klabu yake imetuma wapelelezi nchini humo kwa ajili ya kuweka sawa mazingira watakayofikia ikiwa ni sambamba na kuangalia hali ya hewa ya mji wq Juba ambayo wameambiwa haina tofauti na ile Kampala.

Akizungumzia muonekano wa vijana wake kabla ya mechi hiyo Hall alisema wako katika hali nzuri na kusisitiza Azam inanafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo na hatimaye kutwaa ubingwa.

No comments:

Post a Comment