Search This Blog

Friday, February 22, 2013

AZAM FC VS YANGA: UMONY NA KIPRE BALOU WARUDI DIMBANI - KOCHA WA YANGA ASEMA ANATEGEMEA UPINZANI MKALI

YANGA inashuka leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumenyana na Azam FC katika mchezo wa kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha wa Azam, Stewart Hall amesema kurejea kwa majeruhi Brain Omony na Kipre Balou kumempa faraja kubwa na kutamba kushinda mchezo huo na kukalia kiti cha usukani wa ligi.
"Nafikiri Omony na Balou wana mchango mkubwa kwenye timu. Uwepo wao unaongeza chachu ya timu kufanya vizuri." anasema kocha huyo.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Ernest Brandts amesema Azam ni moja kati ya timu bora kabisa kwenye ligi hivyo anatarajia kupata upinzani mkali.
"Azam ni timu nzuri. Ina wachezaji wenye vipaji na uwezo wakucheza kwa maelewano makubwa." anasema kocha huyo.
"Nilikuwa shuhuda wakicheza na JKT Ruvu nakushinda mabao 4-0. Nafikiri ni timu nzuri. Mchezo utakuwa mgumu. Siwezi kutabiri lolote."
Timu hizo mbili zina pointi 36 isipokuwa Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam inashika nafasi ya pili, lakini yenyewe imecheza mechi 17 wakati vinara Yanga ikicheza 16.
Endapo Yanga itapoteza mchezo huo itakuwa imejiweka kwenye nafasi ngumu ya kutwaa taji hilo kwa msimu huu.
Yanga na Azam zimekutana mara tano tangu msimu wa 2011/12 katika mashindano tofauti.
Katika mechi hizo Yanga imeshinda mara mbili kama ilivyo kwa Azam FC.
Yanga iliifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali Kombe la Kagame na mechi ya ligi mzunguko wa kwanza kwa mabao 2-0.
Azam yenyewe iliifunga Yanga mechi mbili za ligi msimu uliopita kwa mabao 1-0 mchezo wa kwanza na ule wa marudiano ikiilaza 3-1 na kutokea vurugu kubwa baada ya Haruna Niyonzima kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Israel Nkongo ikiwa ni kadi yake ya pili ya njano kwa kosa la kumchezea rafu beki Aggrey Morris wa Azam ambaye amesimamishwa pamoja na Said Morad, Erasto Nyoni na Deogratius Minishi kwa tuhuma za kuchukua rushwa kwenye mchezo wa Simba.

Vita nyingine itakuwa kati ya washambuliaji Kipre Tchetche wa Azam na Didier Kavumbagu kama atanzishwa kikosi cha kwanza.
Jamaa hawa ndio vinara wa kufunga mabao kwenye ligi. Tchetche amefunga mabao 10 huku Kavumbagu akizamisha tisa na kuziweka timu zao katika nafasi mbili za juu.

1 comment: