Search This Blog

Friday, December 28, 2012

FEDHA ZILIZOCHUKULIWA NA TRA KWENYE AKAUNTI YA TFF NI ZA VILABU VYA LIGI KUU - VYATISHIA KUGOMEA LIGI WASIPORUDISHIWA

Klabu 14 ambazo timu zao zinashiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.

Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa haikati PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh. 157,407,968.

TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

OFISA WA CAF KUTUA MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.

Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Utekelezaji wa kazi yake nchini utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa Usalama wa TFF.

No comments:

Post a Comment