Search This Blog

Tuesday, December 11, 2012

BREAKING NEWS: NADIR CANAVARRO, AGRREY MORRIS, MCHA KHAMISI NA WACHEZAJI WENGI WASIMAMISHWA KUICHEZEA ZANZIBAR HEROES KWA MUDA USIOJULIKANA

Chama cha Soka Visiwani Zanzibar, ZFA, kimeivunja rasmi timu ya Taifa ya Zanzibar, 'Zanzibar Heroes' na kuwasimamisha kwa muda usiojulikana wachezaji 16 wa kikosi hicho kucheza soka ndani na nje ya nchi kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Akitangaza maamuzi ya kikao cha kamati tendaji cha ZFA Taifa kilichokaa leo mchana ofisi za Chama hicho zilizopo Kiembe Samaki nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Makamo wa Rais wa ZFA Taifa kwa upande wa Unguja, Alhaj Haji Ameir, amesema wameamua kuchukua maamuzi hayo ambayo kimsingi yameungwa mkono na wajumbe wote wa Kamati tendaji waliohudhuria kikao hicho ili kutoa somo kwa wachezaji wengine.


Kikao hicho cha dharura kimekuja kufuatia sakata la wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar, 'Zanzibar Heroes' kuamua kugawana kiasi cha dola 10,000 ambazo ilikuwa ni zawadi baada ya timu hiyo kushika nafasi ya tatu katika michuano ya kombe la chalenji iliyomalizika wiki iliyopita jijini Kampala nchini Uganda, baada ya kuifunga Timu ya Kilimanjaro Stars kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 6-5.


Inadaiwa kuwa wachezaji hao waliamua kugawana fedha hizo kwa madai kuwa wamekuwa wakidhulumiwa fedha zao na chama cha soka visiwani Zanzibar.


Hata hivyo katika ufafanuzi uliotolewa leo na Katibu Mkuu wa ZFA Taifa, Kassim Haji Salum amesema haijawahi kutokea wachezaji wa timu hiyo kudhulumiwa haki yao akikumbushia fedha za zawadi walizopata mwaka 1995 katika mashindano kama haya yaliyofanyika nchini Uganda na Zanzibar ikafanikiwa kutwaa ubingwa na mwaka 2009 walishika nafasi ya tatu na mara zote walipewa stahili zao.

Kufuatia maamuzi hayo wadau wa soka visiwani Zanzibar wameunga mkono hatua hiyo kwa kusema itasaidia kurejesha nidhamu katika timu ya taifa, mmoja wa waliotoa maoni yao ni Katibu mwenezi wa klabu ya New Boko, Mohammed Mrope amesema hatua hiyo ya ZFA itakuwa fundisho na kuleta nidhamu kwa wachezaji wa timu wa taifa, "Timu ya taifa ya Zanzibar imekuwa mfano mzuri kwa timu nyengine kwa wachezaji wake kuwa na nidhamu yahali ya juu....sasa hili lililofanyika imekuwa kama timu ya magengeni mimi naunga mkono 100 kwa 100 hatua ya kuivunja timu na kuwasimamisha wachezaji wote waliohusika katika suala hili'. Akisema Mrope.


Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Timu ya Zanzibar Salum Bausi ambaye jana alitangaza rasmi kujiuzulu kuifundisha timu hiyo amesema hatua hiyo ni sahihi kabisa kwa sababu kitendo hicho kimewafedhehesha wadau wa soka na wazanzibari kwa ujumla.


Tayari ZFA Taifa walikwishatuma barua rasmi kwa TFF juu ya hatua hiyo huku nakala ya barua hizo zikitarajiwa kusambazwa kwa vilabu wanavyochezea wachezaji hao.


Wachezaji wanne walionusurika na adhabu hiyo ni wale walioamua kuzirejesha fedha hizo ambao majina yao hayakutajwa kwa sababu maalum, hata hivyo taarifa zilizopo ni kuwa wachezaji hao wanatoka katika klabu ya Kipanga timu inayomilikiwa na JWTZ, Jamhuri, Zimamoto na KMKM.

5 comments:

  1. uwamzihuo nimzurisana maana watazoweya kilaki2kinataratibuzake,

    ReplyDelete
  2. Maamuzi waliyofanya ni sahihi kabisa,ila wangefanya mahojiano na wachezaji husika kabla ya adhabu,lakini ni fundisho kwa waliokosa na wasio kosa,ila kama kawaida yetu siasa itachukua mkondo wake,sababu kubwa ni baadhi ya wachezaji mafaza wanachezea vilabu vikubwa,,.

    ReplyDelete
  3. wengine washazoea uhuni tena nina wasiwasi na wanaomwita canavaro ndo aweza kuwa alihimiza wenziwe wagawane coz hata klabu anayotoka alishiriki kumpiga mwamuzi, so kwa hilo ni sahihi kabisa, wapeni nafasi wengine waonyeshe vipaji vyao hao wahuni achaneni nao

    ReplyDelete
  4. Tumia akili ww uliepost 11.05PM acha usimba wako ww unaona raha wachezaji wasote then viongozi wale hela kirahaisi. Ni haki yao na hawarudishi na watacheza mpira, chezea TZ ww

    ReplyDelete
  5. HIYO SIYO SURUHU!!!
    ZFA hawajazngatia chanzo halisi cha kituko hicho, watizame ni waapi wamejikwaa then watoe maamuzi, wachezaji wanajitoa kufa na kupona kwajili ya ya timu zao lakin wajanja wachachewanafaidi majasho yao, lazima hapo katkat kuna udhaifu wa viongozi hali kama hiyo haiwezi kuja hivhiv.
    Jones Kija, Arusha.

    ReplyDelete