Search This Blog

Friday, November 2, 2012

NI MAKOCHA WA KIGENI AU WAFANYA BIASHARA WA KIGENI?


Timu ya soka ya Azam FC imemfuta kazi kocha wake, Boris Bunjak baada ya kupoteza mchezo mmoja tu wa ligi kuu dhidi ya Simba wikiendi iliyopita. Azam ambayo tangu ipande ligi kuu mwaka 2008 imeshafundishwa na makocha wanne wa kigeni hivyo inahitaji kuwa na kocha wa tano wa kigeni ndani ya misimu minne ya ligi kuu, tangu wapande. Kwa nini hali inakuwa hivi kila siku kwa mpira wetu.



MAKOCHA BORA WANATOKA NCHI HIZI
Wakati, Mataifa mengi ya Ki- Afrika yakifanya vizuri katika mchezo wa soka ndani na nje ya bara hili, sehemu kubwa ya mabenchi yao ya ufundi yalikiwa na raia wengi kutoka mataifa ya Ujerumani ama Ufaransa. Mafanikio ya nchi kama Cameroon, Nigeria, yamebebwa sana na Wajerumani waliowahi kufanya kazi nchini mwao. Hata wakati nchi za Senegal na Tunisia au majirani zao, Morocco, katika miaka ya nyuma yalipelekwa na Wafaransa.

Nchi hizi zilipata mafanikio kwa sababu ya uvumilivu, uwezo wa kujitolea na kufundisha wa makocha wa asili wa kutoka nchi hizo, Ujerumani na Ufaransa, makocha wa kutoka huko pia ni wenye ufundishaji hasa wa mpira uwanjani, si walalamishi na wala si watu wa kutoja visingizio timu inapofeli. Wapo wazi na wepesi wa kusema ' kazi hii imenishinda'. Wanahitaji kuona wachezaji wakipata huduma muhimu kwanza kabla yao, ili wawafanikishie CV zao, kwani pesa tayari wameshachota wakiwa wachezaji muhimu katika vilabu vya Bundesliga ama League1. Vitu kama hivi vilizipaisha timu hizi lakini baada ya kuanza viongozi kujifikiria wao kwanza, kabla ya wachezaji wamejikuta wakikosa makocha bora.

Kutoka hizi hizo katika miaka ya karibuni, na hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa soka la mataifa haya kushuka. Wajerumani ama Wafaransa, kwanza wana moyo wa ufundishaji na wanataka kuona mataifa mengi duniani yanakuwa na mbinu bora za mchezo ili kuweza kusisaidia nchi zao katika michuano ya ki-dunia mbele ya Mataifa makali kwa soka ya kutoka nchi za Amerika ya Kati na Kusini, hivyo mara nyingi hupendelea kufundisha soka nchi za Asia na Afrika kwa sababu mataifa ya mabara haya bado hayana mbinu bora za kuzifunga timu kama, Argentina, Mexico, Uruguay ama Brazil. Na nchi nyingi za Ulaya hupata tabu pia mbele ya mataifa haya pindi wanapokutana.


Katika fainali za dunia pale Sauzi, Bara la Amerika ya Kusini lilikuwa na nchi za Brazil, Argentina na Uruguay na Paraguay wakati bara la Afrika lilikuwa na timu ya Ghana na lile la Asia halikuwa na timu yoyote baada ya Japan na Korea Kusini kufungwa na nchi za Paraguay na Argentina, Lakini, ili Ujerumani itwae ubingwa walitakiwa kuifunga Argentina katika robo fainali, ili Holland itwae ubingwa ilitakiwa kuifunga Brazil. Ni kazi sana unapokutana na ratiba hii na Wajerumani huwa hawaipendi itokee katika hatua hiyo, hivyo ili michezo mirahisi waipate katika hatua hii huja Afrika na Asia kuziimarisha nchi kama Cameroon, Nigeria, Senegal, Morocco, Tunisia, ambazo huwakilisha Afrika mara kwa mara katika kombe la dunia, ili walau ziweze kuvuka hatua ya makundi na kwenda kucheza kufa na kupona na kupona anapokuta na timu za Amerika kama ilivyotokea Afrika ya Kusini, wakati, Uruguay ikihitaji mapigo ya penati ili kuitoa Japan, na Argentina ikihitajika kutumia nguvu na maarifa zaidi kuitoa, Korea Kusini. Timu hizi za Amerika zote ziliondolewa kirahisi walipokutana na mataifa matatu ya Ulaya na kushindwa kutwaa taji hilo.


TANZANIA HATUJUI WAPI WANAPATIKANA MAKOCHA BORA

Bukhard Pape

Watanzania tumekuwa wepesi wa kusahau na wagumu wa kujifunza. Mwanzoni mwa karne hii, tulipata bahati kutoka FIFA, pale walipoamua kutusaidia mkurugenzi wa ufundi wa Kijerumani, Burkhad Pape. Chini ya Mjerumani huyu tuliweza kunufaika na mawazo yake japo serikali ndiyo ilikuwa ni kikwazo. Pape, kama, mkurugenzi wa ufundi wala hakuwa anapata zaidi ya alichokuwa akipewa na FIFA, kutokana na uwepo wake nchini, kama Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ufundi katika soka la Tanzania. Alikuwa akipigwa vita sana na waliokuwa watawala wa soka nchini wakati huo kutokana na misimamo yake, mara kadhaa walimdhihaki kwa kumsema kuwa si lolote, lakini matokeo yake tuliyaona katika muda wake mfupi aliofanya kazi Tanzania, tulitwaa taji la Castle Cup, huku tukiwa na mbinu zaidi ya ufundi na tukicheza soka la kueleweka.
 

VILABU VYA TANZANIA
Vilabu vya Tanzania kwa miaka kumi iliyopita vimekuwa vikiwatumia zaidi walimu wa kigeni. Wapo ambao wamekuwa wakitoka barani Afrika lakini asilimia kubwa wanatoka barani Ulaya. Nchi ya Serbia ndiyo imekuwa na maingizo mengi kuliko nchi nyingine, Wareno, Wabrazil, na makocha wa kutoka, Zambia, Uganda, Malawi, Argentina, India, Ubelgiji, Holland, Kenya ndiyo wamekuwa wakiziongoza timu zetu zenye unafuu kiasi kifedha.


James Siang'a
Lakini ukimtoa, Jack Chamangwana, ambaye aliipa Yanga, ubingwa wa ligi kuu mara tatu katika miaka yake mitatu aliyowahi kuifundisha timu hiyo tena ikiwa bila fedha ya kutosha, hakuna mwalimu mwingine wa kigeni ambaye amepata mafanikio zaidi ya James Siang'a wakati akiinoa, Simba. Makocha wote hawa wawili waliondolewa kwa sababu za nje ya uwanja na hawakupewa maandilizi yoyote ya maana wajati wakienda kuziongoza timu zao katika michezo ya Afrika. Wakaondolewa wakati, Simba ikiwa chini ya Kassim Dewji na ufadhili, mfanyabiara mkubwa nchini, Mohammed Dewji. Jacky Yeye aliondolewa wakati, Yanga ipo chini ya Francis Kifukwe na mwanzoni mwa ufadhili, wa mfanyabiara, Yusuph Manji.
 

Makocha hawa waliweza " ku- struggle'. na timu hizi hata pale walipodiriki kulala na njaa, walijua mazingira ya Tanzania na kisha waukautambua uchumi wa Tanzania, wakaamua kusafisha CV zao, ili wapate mahali penye marisho bora zaidi. Yuko wapi sasa, Jacky? Siang'a alipata heshima gani Tanzania? Kuna wakati ikambidi afundishe, Simba na Taifa Stars, na zote hazikuwa na pesa. Mathalani wakati anaingia, Simba aliletwa na uongozi wa mpira chini ya marehemu, Juma Salum, lakini alishindwa kufanya kazi na wafanyabiashara ndani ya Simba. Mwisho wa makocha bora wa kigeni ukawa hapa. Tukaanza kufundishwa na Wafanyabiara 'wa kigeni' na mawakala wa wachezaji ambao ndani yake hawana mbinu na walalamishi sana wanapokosa pesa katika mifuko yao.


WABRAZIL WALIOWAHI KUJA NCHINI

Kuanzia kwa Marcio Maximo, Marcus Tinocco, Itamar Amourin, Neidor Dos Santos na Rodrigo, wote hawa waliletwa nchi kibiashara zaidi na si kisoka. Makocha hawa walitumia muda mwingi kulalamikia mazingira ya kazi yao nchini, uku wakijaribu kufanya ushawishi wa kuwaaminisha Watanzania, kuwa safari zote za nje ya nchi zilizohusisha maandalizi ya klabu au timu za Taifa ni ya kisoka zaidi. Na walipobaini wanaanza kushtukiwa na Watanzania wakaondoka zao pasipo kuacha msingi wowote imara wa timu, iwe zile za taifa ama klabu.

Ni kweli, Wabrazil wanajua mpira lakini nani amewahi kuwa mfundishaji mzuri wa soka kutoka nchini humu? Hakuna, hata, Fillipe Scolari alishindwa alipotoka ' Brazil B' Ureno, na kutakiwa kuwafundisha mbinu kina, Michael Ballack, Didier Drogba, Frank Lampard na wengineo pale, Chelsea. Kuchukua kocha wa Kibrazil na kumleta Tanzania ni upumbavu, lakini, kibiashara, its, OK, Inafaa. Unajua kinachopatikana, Brazil? Chunguza makocha hawa walifanya kazi na timu gani ya uongozi, kuanzia klabuni kwao hadi wale wa timu za Taifa.


WASERBIA

Micho
Wa kwanza kuja na kufanya kazi nchini alikuwa ni Dragan Popadic kwenye miaka ya 90 ambaye alifanya vizuri, na baadae kwenye miaka hii ya hivi karibuni akaja kocha Milutin Micho, Mserbia huyu aliweza kujitangaza kama kocha bora katika ukanda wetu baada ya kuiwezesha timu ya SC Villa ya Uganda kuwa na mchezo mzuri uwanjani na timu inayotwaa mataji. Alipokuja Yanga ilikuwa chini ya Francis Kifukwe na Manji na kocha huyu alihitaji kuona Yanga ikipata mafanikio zaidi kimataifa baada ya kuwa watawala wa soka la ndani kwa miaka mitatu mfululizo, na mara baada ya kushindwa kupata sapoti ya maana wakati akiiandaa timu kwa michezo ya Afrika na kutolewa katika raundi ya Pili, Micho aliamua kuondoka Yanga mara baada ya kufungwa na El Merreikh ya Sudan katika michuano ya kombe la shirikisho ambayo waliangukia baada ya kutolewa katika ligi ya mabingwa. Alichukia kuona mfadhili akitoa millioni 100 kulipa viingilio vya mchezo kuliko kuandaa timu, huyu alikuwa anatafuta CV akaondoka zake haraka.
  Ukaanza msululu wa 'mawakala' Dusan Kondic akaja, Kostadin Papic, Boris Bunjak wa Azam na Milovan Curkovic, ambaye alifeli mara ya kwanza alipokuja nchini kuifundisha Simba, na msimu uliopita atleast aliwezesha Simba kumaliza msimu bila kupoteza katika ligi ambayo haina ushindani mkubwa, lakini  na sasa akielekea kutimiza mwaka mmoja tangu arejee amepewa mechi nne za kushinda kati ya tano za mwisho kabla ya raundi ya kwanza kumalizika, akishindwa anaondolewa. 

Nchini haina makocha bora na makocha wanaotoka huku huzikwamisha timu zao kwa kujitazama wao zaidi, kuliko timu, ni walalamishi sana na wasiokubali ukweli kuwa hali ya uchumi wa Tanzania haufanani na wa kwao, hatuna pesa ya kufanya kila kitu na wao wanajua ukweli huu, lakini wanaletwa kwa sababu za kiabiashara zaidi na pale wanaokosana na waajiri wao huondoshwa haraka kwa sababu ya kutovuruga madili ya biashara zao, wanabaki washkaji na timu inabadili tena makocha 'vimeo'.

TOM SAINTFIET, SAM TIMBE, PATRICK PHIRI, STEWART HALL

Hawa walikwamishwa na viongozi wa klabu zao, hawakutaka kuingia zaidi katika biashara zao na wakaamua kuachana na timu zao huku wakizidai pesa kibao. Makocha wangeweza kufanya kazi nzuri na yenye mafanikio Tanzania kama wangepewa sapoti ya uhakika. Walihitaji kuona timu za Tanzania zinafanikiwa kimataifa na walikuwa tayari kufanya kazi katika mazingira yetu. Lakini hawakuwa wafanyabiashara ndiyo maana wakaondolewa bila sababu. Stewart Hall afadhali amerudi Azam kuendeleza mazuri aliyoyaanzisha.

CHUNGUZA PIA MAKOCHA WA TIMU ZA TAIFA WANAPOTOKA
Makocha wa timu zetu za Taifa kwa kipindi cha miaka sita iliyopita hawajaweza kufikia uwezo wa kocha, mzawa Mshindo Msolla, ambaye pamoja na kazi yake nzuri kama kama kocha, Msolla alikuwa akitoa pesa yake mfukoni kuisafirisha timu ya Taifa nje ya nchi ama ndani ya nchi kucheza michezo yake. Alikuwa ni Mzawa hasa na mwenye uwezo mkubwa wa ufundishaji, lakini ukata uliokuwepo na migogoro isiyokwisha katika tawala za juu za soka letu zilimkwamisha lakini ni bonge la kocha ambaye hakuna wa kigeni yoyote anayeweza kuzifikia sifa zake. Sasa hadi TFF wanaleta makocha ambao wanakuja kutafuta pesa na si kutufundisha mambo ya ufundi, wanaondoka timu haina msingi wowote. Kwa upande wa Marcio Maximo ambaye kiukweli alikuwa mhamasishaji kuliko mjuzi wa kufundisha soka, na alipata bahati ya kupewa kila kitu akitakacho kutoka serikalini lakini hatukapata mafanikio makubwa ya kujivunia chini yake.

3 comments:

  1. Bravo! Good analysis. I hope wahusika watasoma na kufanyia kazi.

    ReplyDelete
  2. I like ur analysis. Good job Shafii.

    ReplyDelete
  3. Tuanze kuwang'oa mafisadi kina Tenga pale TFF , Halafu tumalizie na mazumbukuku kama kina Rage, akilimali, kaburu, manji , etc. kuna kazi kubwa ya kufanya ili soka letu lipande ila kwa sasa natamani hawa watu wasiwepo kabisa ktk ramani ya soka la bongo..let's get 'em out of the picture..tuache njaa jamani !!

    ReplyDelete