Search This Blog

Friday, November 30, 2012

MMILIKI WA GARI ALIYOPATA NAYO AJALI SHARO MILLIONEA AJITOKEZA NA KUZUNGUMZA - WEZI WALIOMUIBIA WAPATIKANA


MMILIKI wa gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na msanii maarufu nchini, Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ na kupata nalo ajali iliyosababisha kifo chake huko Muheza, Tanga, Mohammed Ismaili maarufu kwa jina la Mudi Suma, ameibuka na kueleza uhusiano wake na marehemu, huku akisema amekubali hasara.


Akizungumza kwa simu kutoka Muheza jana Suma alisema hana mpango wa kudai fidia au kupeleka malalamiko yoyote kwa ndugu wa marehemu kwa kuwa; “Kilichotokea ni kazi ya Mungu.” “Siwezi kudai hata kidogo hivyo ni vitu vya kupita tu. Marehemu alikuwa ni zaidi ya ndugu yangu, gari ni kitu kidogo sana katika uhusiano tuliokuwa nao,” alisema Suma na kuongeza kwamba hata Marehemu Sharo Milionea naye alikuwa amemwachia mali zake kadhaa ikiwamo gari.



“Siyo gari tu alilokuwa ameniachia. Kuna mikataba yake ya kazi, Bajaji yake na funguo za chumbani kwake. Nasubiri kukabidhi vitu hivyo baada ya kukaa na ndugu zake. Vitu viko kwenye mikono salama,” alisema.



Kuhusu gari lake lililopata ajali, Suma alisema lilikuwa na bima ndogo, lakini anapanga kwenda TRA atakaporejea Dar es Salaam kufuatilia baadhi ya mambo.

“Kabla ya kuondoka bima ile kubwa ilikuwa imekwisha kwa hiyo nikaamua kuikatia bima ndogo. Nitakapofika kesho (leo) Dar es Salaam, nategemea kwenda ofisi za bima kuzungumza nao,” alisema Suma.


Alipoulizwa kama kuna mtu mwingine atakayeathirika kutokana na gari hilo kuharibika katika ajali mbali na yeye, alijibu: “Hakuna tofauti na mimi mwenyewe na familia yangu.”



Kabla ya ajali

Suma alieleza kuwa kabla ya kuanza safiri yake, Sharo Milionea alifika nyumbani kwake mchana na kumweleza kuwa afya yake haikuwa nzuri.


“Kabla ya kuondoka aliniambia kuwa hajielewi elewi na kifua kilikuwa kinambana. Nikamshauri asiondoke peke yake, atafute mtu wa kuondoka naye ambaye atamsaidia kuendesha gari njiani,” alisema Suma na kuongeza:



“Tulianza kuwapigia simu jamaa zetu wanne wa kusafiri naye lakini kila tuliyemwambia hakuwa tayari. Ilikuwa ni changamoto mpaka ilipofika saa 10:45 hivi jioni, akaamua kuondoka peke yake. Wakati anatoa gari getini kwangu, nikamwambia, basi jaribu kuwa mwangalifu sana, maana alikuwa kweli anasumbuliwa na kifua. Tukakubaliana kwamba atakaporudi aende hospitali kucheki afya yake.”



Kuhusu uhusiano wake na marehemu, Suma alisema: “Mimi ni mfanyabiashara na yeye alikuwa msanii, lakini ilitokea tukawa marafiki sana mpaka ikafikia wakati nikaona kuwa ni ndugu yangu. Nilimwamini nikamtambua kama sehemu ya familia.”



Alisema marehemu alikuwa akitumia gari hilo kila alipolihitaji na safari ya kwenda nalo Tanga kwa wazazi wake ilikuwa ni ya tatu.“Siyo mara ya kwanza kuitumia gari lile, nilikuwa nimemwamini sana. Safari ya kwanza alichukua na kusafiri nalo mwenyewe, halafu safari ya pili ikafuata na hii ilikuwa safari ya tatu,” alisema Suma.



Eneo la ajali wakimbia makazi

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Songa Kibaoni mahala ambako Sharo Milionea alipatia ajali, wamezikimbia nyumba zao baada ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu kutoa siku moja kwa waliopora mali za marehemu huyo kuzisalimisha mara moja.


Wakati huo huo

Jeshi la Polisi la Polisi Mkoani Tanga na kushirikiana na wasamalia wema wamewatia mbaroni vijana wanne wanadaiwa kumpora vitu mbalimbali marehemu Sharo Milionea baada ya kupata ajali mbaya mwanzoni mwa wiki hii.

Habari za kuaminika toka Mkoani humo zinasema kuwa vijana hao wamekamatwa baada ya kazi nzuri iliyofanbywa na Jeshi la Polisi Mkoani humo kushirikiana na wasamalia wema ambapo hadi sasa vijana hao wako chini ya ulinzi mkali huku wengine wakiwa bado wanatafutwa.

Habari zaidi zilisema kuwa vijana hao wamekamatwa jana usiku na waliokamatwa wamefahamika kwa jina ya Issa Makunera, Farid Hassani, Rashidi Ayubu, Rashid Makunera na imeelezwa watuhumiwa hao wamekutwa na mali mbalimbali za marehemu.

Chanzo chetu toka mkoani humo zilisema watuhumiwa hao pamoja na mali  hizo zimekamatwa katika eneo linanaloitwa Songa Kibaoni na vitu hivyo ni SPEA TAILI, REDIO YA GARI, BETERI YA GARI, SAA YA MKONONI SURUALI AINA YA JINS PAMOJA TISHETI, BEGI PAMOJA NA SIMU YA MKONONI.

Hata hivyo habari  ziliendelea kusema kuwa licha ya Begi hilo kupatikana ambalo lilidaiwa ndani yake kulikuwa na pesa nyinge hazikuweza kukutwa na inasemekana katika ya watuhumiwa wanaotafutwa ndio wamekimbia na fedha hizo.

Kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao wananchi mbalimbali wamelipongeza  Jeshi la Polisi pamoja na wananchi waeneo waliyokamatwa watuhumiwa kwani wao ndio waliotoa msaada mkubwa hadi kukamatwa kwao.



Source: http://www.udakuspecially.com - http://xdeejayz.blogspot.com

No comments:

Post a Comment