Search This Blog

Wednesday, November 14, 2012

BARUA YA WAZI KUTOKA KWA WADAU WA SOKA KWENDA TENGA KWA UKIUKWAJI WA KATIBA YA TFF

-->

Bwana Leodger Chilla Tenga
Rais wa TFF

Ndugu Tenga,

YAH: UKIUKWAJI WA KATIBA YA TFF

Sisi wadau wa mpira wa miguu Tanzania tunakuandikia barua hii tukiwa na uchungu mkubwa kuhusu mwenendo wa uongozi wako.  Ulipoingia madarakani kwa mara ya kwanza Golden Tulip tarehe 27 Desemba 2004 ulitoa matumaini makubwa kuhusu kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa mpira wetu.  Pamoja na mapungufu mengi yaliyojitokeza ndani ya miaka minane ya uongozi wako haya mawili tutakayoyaeleza hapa chini hayawezi kufumbiwa macho na wanaoutakia mema mpira wa Tanzania.

1.     Kupitisha muda wa uongozi wako bila kibali cha mkutano mkuu.
Mkutano mkuu uliokuingiza madarakani ulifanyika siku ya Jumapili tarehe 14 Desemba 2008.  Kifungu 33(1) cha Katiba ya TFF kinatamka kuwa kipindi cha uongozi ni miaka minne tu.  Hivyo ukomo wa uongozi wako na kamati yako ya utendaji ni saa sita za usiku tarehe 13 Desemba 2012.  Aidha kifungu cha 10(1) cha kanuni za uchaguzi wa TFF kinatamka kuwa tangazo la uchaguzi litatolewa siku 40 kabla ya uchaguzi.  Kwa mantiki hii kamati yako ya uchaguzi ilitakiwa itangaze tarehe ya uchaguzi siku ya Jumatatu tarehe 05 Novemba 2012 au kabla ya hapo.   Leo ni tarehe 13 Novemba 2012 na ofisi yako iko kimya!  Hii haikubaliki, haiwezekani ujiongezee muda wa uongozi bila kibali cha Mkutano Mkuu.  Tutawaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu wakuadhibu kwa kosa hili la ukiukwaji wa Katiba.  Pamoja na mapungufu haya ni vyema ukatufahamisha uchaguzi umepanga ufanyike lini au unasubiri wajumbe wa mkutano mkuu wakulazimishe kwa maandishi?

2.     Kufuta nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF
Yapo maneno yanasemwa eti uongozi wako unataka kufuta nafasi ya pili ya Makamu wa Rais wa TFF kinyemela.  Kama tuhuma hizi ni za kweli tunaoma tukukumbushe yafuatayo:
2.1.1      Nafasi ya makamu wa pili wa Rais wa TFF iko ndani ya Katiba ya TFF kifungu 31(1)
2.1.2      Kifungu cha katiba 30(1) kinatamka wazi kuwa ni mkutano mkuu pekee wenye mamlaka ya kubadili Katiba ya TFF.  Hivyo hakuna njia mbadala ya kubadili Katiba ya TFF.
2.1.3      Kifungu cha Katiba 30(2) kinatamka kuwa tangazo lolote la nia ya kubadili Katiba ya TFF litatolewa siku 45 kabla ya mkutano mkuu.  Uongozi wako utawezaje kutoa tangazo hili ndani ya kipindi cha uongozi wako kilichobakia?
2.1.4      Kifungu cha Katiba 30(6) kinatamka kuwa ombi la kubadili katiba litapigiwa kura NDANI YA MKUTANO MKUU na ili lipite theluthi mbili ya wajumbe sharti iridhie.  Zingatia utashi huu wa Katiba.

Bwana Tenga kama kweli wazo hili lipo basi achana nalo, usijidhalilishe kwa kukiuka Katiba iliyokuweka madarakani.  Nafasi za uongozi katika uchaguzi ujao zitangazwe kwa mujibu wa Katiba iliyokuweka madarakani.  Kama kuna umuhimu wa kubadili Katia hakuna uharaka wowote, subiri awamu ijayo ifanyie kazi wazo hilo, awamu ambayo huenda wewe mwenyewe ukaingoza pia kama ukigombea tena.

Tunasubiri majibu ya hoja zetu za majibu haya tunaomba uwajulishe watanzania wote.

Nakala ya barua hii tunawapelekea wajumbe wote wa Mkutano Mkuu kwa taarifa.

Ni sisi kwa niaba ya wadau wa mpira wa Tanzania.

1 comment:

  1. Hakuna material hapa, hoja dhaifu kabisa hizi! na aliyeandika kwa kujipachika "jina la wadau wa soka" hebu na aende akafanye utafiti vizuri kisha aje na hoja za uhakika na siyo za kuhisi hisi. na una uhakika gani kwamba tangazo la kubadili katiba halijatolewa kwa mujibu wa taratibu za kisheria? au unasubiri litangazwe redioni clouds?

    ReplyDelete