Search This Blog

Wednesday, October 10, 2012

TENGA AZITAKA KAMATI ZA UCHAGUZI KUSIMAMIA KANUNI



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amezitaka Kamati za Uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki. Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga amesema uongozi wa mpira wa miguu unahitaji uamuzi mgumu, hivyo Kamati za Uchaguzi ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Katiba zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na si kuangalia sura za watu.

Amepongeza kamati zilizosimamia uchaguzi kwa kufuata kanuni, na ingawa kila mtu ana haki ya kuongoza, jambo lolote lazima liwe na kanuni, kwani hata kwenye mikutano ya hadhara kuna kanuni. “Huwezi kufika kwenye mkutano wa hadhara na wewe unaanzisha mkutano wako. Lazima kanuni ziheshimiwe ili kufanya uchaguzi uwe huru na wa haki. Nini kimetokea kwenye maeneo ambayo kuna matatizo? Kila mwanachama wetu (mkoa/chama shiriki) ana Kamati ya Uchaguzi ambayo imeundwa kwa mujibu wa kanuni.

 “Zile kamati hazitekelezi majukumu yake, unampitisha mtu unajua hana sifa unasema acha akafie mbele (Kamati ya Uchaguzi ya TFF). Kanuni zinasema jaza fomu mwenyewe, weka nakala za vyeti na si kwamba huyu tunamjua. Kanuni zinatakiwa zifuatwe, ukienda kinyume unaondolewa,” amesema. Amesisitiza kamati zifanye kazi kwa kufuata kanuni ili kusaidia mpira wa miguu kwani zimeundwa kihalali, kwa hiyo zisiogope kuengua hata walioziteua kama hawana sifa. Pia Rais Tenga amezitaka Kamati za Utendaji na Sekretarieti kutoziingilia Kamati za Uchaguzi katika mchakato wa uchaguzi, badala yake zinatakiwa kuziwezesha tu (facilitation).

Amesema baadhi ya wagombea nao ni tatizo kwani wanaingia kwenye uchaguzi bila kuzielewa Katiba za vyama vyao na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hivyo ni vizuri wakazielewa kwanza. Rais Tenga amesema ni vizuri wanachama wote wakafanya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa TFF utakaofanyika Desemba mwaka huu ili wapate fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo wa shirikisho. Vilevile amewataka wadau kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi kwenye chaguzi za vyama wanachama wa TFF, kwani mwitikio umeonekana kuwa mdogo kulinganisha na umaarufu wa mchezo wenyewe. Amepongeza vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi wao. Baadhi ya vyama hivyo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Morogoro, Mtwara na Singida. Boniface Wambura Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment