Search This Blog

Friday, October 19, 2012

SIMBA NA KAGERA SUGAR ZAINGIZA MILLIONI 58 - TIMU ZAGAWANA MILLIONI 22

Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar lililochezwa jana (Oktoba 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 limeingiza sh. 58,505,000.
 
Watazamaji 9,842 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 11,013,785.54 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,924,491.53.
 
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 440,000, mtathimini wa waamuzi sh. 254,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
 
Umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 3,183,890. Gharama za mchezo sh. 3,671,261.85, uwanja sh. 3,671,261.85, Kamati ya Ligi sh. 3,671,261.85, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,202,757.11 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,468,504.74.

 
TFF, FKF ZAANZISHA USHIRIKIANO MPYA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuinua kiwango cha mpira wa miguu katika nchi hizo.
 
Akizungumza baada ya mkutano uliowakutanisha vinara wa mashirikisho hayo Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema wameamua kurejesha uhusiano huo uliokuwepo zamani baada ya kuwepo utulivu katika uendeshaji mpira wa miguu nchini Kenya.
 
Amesema maeneo ya ushirikiano ambayo wameagiza yafanyiwe kazi na sekretarieti za pande zote (TFF na KFF) ili baadaye yaingizwe katika Hati ya Makubaliano (MoU) ni mafunzo, waamuzi, mechi za timu za Taifa za wakubwa, vijana na wanawake, na Ligi Kuu.
 
Rais Tenga pia amesema wameamua kuwepo ziara za mafunzo (study tours) katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Kenya wao Ligi Kuu yao iliingia katika mfumo wa kampuni mapema, hivyo itakuwa fursa nzuri kwa Bodi ya Ligi Kuu ambayo iko kwenye mchakato wa kuanzishwa kupata uzoefu kwa wenzao wa Kenya.
 
Naye Rais wa FKF, Sam Nyamweya aliyefuatana na Makamu wake wa Rais, Robert Asembo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria, hivyo wameamua kuuanzisha upya kwa faida ya nchi hizo.
 
Amesema hivi karibuni FKF ilichukua waamuzi kutoka Tanzania waliochezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana), hivyo wameamua kubadilishana waamuzi kwa lengo la kuwaongezea uzoefu.
 
“Waamuzi wa Tanzania walichezesha vizuri mechi ile. Unajua kwetu kuna upinzani mkubwa katika klabu kama AFC Leopards na Gor Mahia, ukipanga refa utasikia wengine wanalalamika, mara huyo ni Mjaluo. Hata akichezesha vizuri bado watalalamika tu kutokana na upinzani uliopo katika klabu hizo,” amesema.
 
Rais Nyamweya ameongeza kuwa ili kuondoa malalamiko katika mechi za aina hiyo wanaweza kuchukua waamuzi kutoka Tanzania, na vilevile waamuzi kutoka Kenya wakachezesha mechi za aina hiyo nchini Tanzania.
 
Amesema vilevile wamepanga kuangalia uwezekano wa kuwa na mechi za kuandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu za nchi hizo ambapo washindi watatu au wanne wa kwanza katika ligi hizo kushindana.
 
Kwa upande wa mafunzo, wamekubaliana kuwa kwa vile kila nchi ina wakufunzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na la Afrika (CAF) watawatumia kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa waamuzi, makocha, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi badala ya kusubiri mafunzo ya aina hiyo kutoka kwa mashirikisho hayo ya kimataifa.
 

No comments:

Post a Comment