Search This Blog

Wednesday, October 3, 2012

DAR-PACHA KUISIMAMISHA TANZANIA KWA DAKIKA 90

 HISTORIA YA TIMU HIZI
Kuna siku nilikaa na kuzungumza na mmoja wa viongozi wa juu wa bodi ya udhamini ya timu ya soka ya Simba, Mzee Hamis Kilomoni, alinieleza mambo mengi kuhusiana na mpira wa Tanzania tangu zama zile za ukoloni hadi leo hii. Wakati yeye alipokuwa kijana miaka ya 1962 hadi 1978, Mzee Kilimoni alijitambulisha kama mshamauliaji-mfungaji mahiri wakati huo, na katika mchezo wake wa kwanza wa ushindani akafunga mabao manne peke yake katika ushindi wa kusisimua wa Sunderland ( Simba hivi sasa) dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC mwaka 1962, tena akiwa na miaka 17. Ni rekodi iliyodumu kwa miaka mingi na hakuna uwezekano wa kuvunjwa hata katika mchezo wa kwanza wa mahasimu hao msimu .

 Yanga ndiyo timu ya kwanza kuanzishwa. Ilianzishwa mwaka 1935 na mwaka mmoja baadae Simba ikazaliwa ubavuni mwake na kutengeneza uhasama mkubwa wa soka nchini. Mwaka 1978 mara baada ya mchezo wa mahasimu hao ambao ulipigwa uko jijini Mwanza na kuchezeshwa na mwamuzi Ndimbo Manyota (marehemu) ulikuwa ni mchezo ambao ulionesha wasiwasi mkubwa kwa aliyekuwa rais wa Tanzania wakati huo hayati Baba wa Taifa, Mwl. JK Nyerere.
 Kwani mara baada ya Yanga kuifunga Simba mabao 2-1 , mashabiki wa Simba waliamini mwamuzi, Manyota aliwabeba Yanga kwani hadi dakika 90 zinamalizika Yanga walikuwa nyuma lakini, mwamuzi huyo hakumaliza mchezo hadi alipoona Yanga inasawazisha na kupata bao la ushindi katika dakika ya 98 na kushinda mchezo huo.
Lakini kutokana na soka safi lililooneshwa na timu yao Mashabiki wa Simba wa Dar es Salaam walijitokeza kwa wingi stesheni ya treni kuwapokea wachezaji wao kishujaa kwa kuonesha soka tamu, si hadithi ya kutunga bali hii ni simulizi ambayo nimepewa na mshambuliaji wa zamani wa Simba ambaye sasa ni mmoja wa wajumbe wa juu wa baraza  la wadhamini la klabu hiyo, Mzee Hamis Kilomoni.
Wakati msafara wa wapenzi wa Simba ukiwa njiani walikutana na msafara ‘rasmi’ wa Rais, Nyerere ( wakati huo) lakini, Nyerere alishtuka kuona watu wengi barabarani na kumuuliza aliyekuwa, Waziri Mkuu, Mzee Kawawa “ Kuna nini, na hawa ni kina nani?” Mzee Kawawa akamjibu; “ Hao ni mashabiki wa Simba”, Rais Nyerere akataka kujua zaidi, akauliza tena; “ Kwani hao, Simba wamechukua kombe gani?”, jibu alilopewa ni lilimchosha, aliambiwa ;” Hapana, wamefungwa jana na Yanga, uko Mwanza sasa mashabiki wao wamekuja kuwapokea baada ya kusemekana refarii aliwapendelea Yanga” maelezo hayo yakamchanganya, Rais Nyerere na akamuagiza, Mzee Kawawa kutazama upya kuhusiana na chaguzi za vilabu vya mpira na michezo mingine zisimamiwe na serikali kwani kama wasipofanya hivyo kuna siku kiongozi wa Simba au Yanga anaweza kuchaguliwa kuwa raisi wa nchi kutokana na idadi kubwa ya ,mashabiki ambayo aliiona siku hiyo. Rais kwa heshima akaamuru msafara wake usimame na kuupisha msafara wa kikosi cha Simba na mashabiki wao upite kwanza.
                                        MBINU ZA KIMCHEZO
Kuelekea mchezo wa mahasimu wa soka nchini, Simba na Yanga jumatano ya leo, vinara wa ligi kuu wamekuwa na matokeo ya ushindi wa asilimia 100, wakishinda michezo yote minne ya mwanzo, Simba imeweza kuzifunga timu za African Lyon, JKT Ruvu,
Ruvu Shootting na Tanzania Prisons na ushindi wote huo waliupata katika uwanja wa Taifa. Wakati wapinzani wao wakicheza michezo miwili nje ya jiji la Dar es Salaam na kushindwa kufunga bao lolote, Simba imeonesha uwezo mzuri wa kufunga mabao, kwani wameshafunga mabao tisa katika michezo minne, huku safu ya ulinzi ikionekana kuimarika kiasi imeruhusu mabao mawili tu, lakini kukutana na timu kama Yanga yenye wafungaji mahiri kama Hamis Kizza,
Simba inafahamika kwa aina yake ya mchezo wa kupasiana pasi za haraka haraka na kuna wakati hupigiana pasi za taratibu pale wanapokuwa wanatafuta mbinu za kuupoozesha mchezo. Yanga wao wana desturi ama tabia moja tu kwamba wao mpira ni matokeo kwanza huwa hawajali sana kupigiana pasi hasa wanapokuwa na matokeo-hasi mchezoni, aina ya wachezaji wanaoingia na kutoka katika klabu hiyo ni wale wale na daima mchezo wao mkubwa ni kutumia maeneo ya pembeni mwa uwanja, hasa ikiwatumia mawinga na mabeki wake wa pembeni. Kwa ujumla mchezo huu ni sawa na ule ambao huzikutanisha timu hasimu za Hispania, Barcelona na Real Madrid, Simba wanatabia za mchezo zinazoendana na Barca na Yanga wao wana kadesturi kama Real Madrid.
            UBORA/ UDHAIFU
Simba wapo vizuri sana katika safu ya mashamublizi kwani tayari wamefunga mabao tisa katika michezo minne waliyocheza hadi sasa. Yanga wao wanaingia katika raundi ya tano kuwakabili mahasimu wao huku tayari wakiwa  wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano, ni mchezo mmoja tu ambao hawajaruhusu bao. Kwa upande wa fowadi hata Yanga wanaonekana kuwa na maendeleo mazuri kwani baada ya kucheza michezo miwili bila kufunga wameweza kufunga mabao saba katika michezo miwili iliyopita, lakini bado timu haina uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao. Wakati viungo wa Simba wakiwa na udhaifu mkubwa katika kuzuia wale wa Yanga wanaoneka kuimarika zaidi katika hilo lakini bado wana tatizo la kuisukuma timu yao mbele.
Katika mabao saba ya Yanga, beki Nadir Haroob amefunga mabao mawili, kiungo, Nizar pia amefunga mara tatu huku washambuliaji wakiwa wamefunga mabao matatu tu, Simon Msuva na Didier Kavumbagu ambaye amefunga mabao mawili. Tofauti kidogo na Simba, wao tayari wameonekana kutengeza nafasi na kuzitumia vizuri, washambuliaji kama Daniel Akkufor ambaye amefunga mara mbili kwa penati, Haruna Moshi, Abdalah Juma, Felix Sunzu na kinda Edward Christopher wakiwa tayari wamefunga ni ishara nzuri kuwa wana uwezo wa kufunga mabao, lakini nao wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kwanza kwa kuwazuia ama Said Bahanunzi, Kavumbagu, Hamis Kizza, Jerry Tegete ama Msuva ambao wanahitaji kuthibitisha thamani yao.
Wakati Simba wakionekana bora katika kutengeneza nafasi Yanga wao wanaonekana bora katika kuziba mianya ya wapinzani kupitisha mipira kutokea katikati ya uwanja. Wanahitaji kuona Oscar Joshua akibaki katika kiwangoi chake cha kila siku ili kumzima, Mrisho Ngassa aliyepania kucheza ili kuthibitisha kuwa yeye mpira kwake ni kazi. Tatizo lingene kubwa kwa kila timu ni kushindwa kucheza mipira ya juu, japo Simba imekuwa ikisaidiwa na uzoefu wa kipa wao, Juma Kaseja, Yanga wanaonekana watapata shida kama Yaw Berko hatokuwa fiti, mana Ally Mustafa si mzuri sana katika kucheza mipira hiyo na alionesha udhaifu kubwa wakati alipofungwa mabao matatu na Mtibwa Sugar wiki mbili zilizopita.
Hata kwa upande wa mabeki, timu zote hazina walinzi wazuri wa mipira ya juu na uwepo wa washambuliaji wanaoweza kutumia mipira hiyo kama, Sunzu, Juma kwa upande wa Simba au Kavumbago na Tegete kwa upande wa Yanga inaweza kusababisha kupatikana walau bao moja ama mawili ya vichwa katika mchezo huo, japo inategemea zaidi na namna kila timu itakavyokuwa imejipanga kimbinu.
Simba tayari wanafunga na Yanga wanaanza kuyatafuta mabao yao, lakini kwa mechi kama hii ni lazima kila mmoja acheze ili kuthibitisha ubora wake na hapa ndipo mabao yatakapopatikana. Difensi ya Simba inaonekana iko vizuri, lakini kiukweli si imara kama inavyoonekana, kama Yanga wataingia kwa kutambua udhaifu wa wapinzani wao bila shaka tatizo kubwa la kwanza kwa Simba linaweza kuwa wao wenyewe.
Kwa nini nasema hivyo? Nimemtaza Juma Nyosso katika michezo miwili dhidi ya Azam FC, ule wa Kagame Cup na ule wa Ngao ya Jamii, ukweli bado hajabadilika na wala hana heshima katika michezo mikubwa. Anacheza rafu nyingi na hata pale mpira unapokuwa nje ya eneo lao la hatari yeye huonekana kumchezea ‘ubabe’  mpinzani kitu ambacho kinaweza kuigharimu timu yake, ni wakati wa Simba kumueleza kuhusiana na uchezaji wake huo kwani anaweza kutoa kadi nyekundu kwa sababu hivi sasa washambuliaji wa Yanga wakiguswa tu hujiangusha.
                   
                   WASEMAVYO MAKOCHA KUELEKEA MCHEZO HUU
Kocha mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic yeye aliweza kuibadilisha timu iliyokuwa inapoteza makali chini ya kocha aliyepita, na kutengeneza uwiano mzuri wa wachezaji vijana na wale wakongwe wenye uwezo. Ameifanya Simba kuwa timu inayocheza sana soka la kuvutia japo  bado timu yake inakabiliwa na matatizo kadhaa ya kiufundi na mbinu. Katika ngome bado kuna matatizo makubwa na yanaweza kuwaingiza katika majaribu ya kupoteza mchezo kama umakini wa ngome yake hautakuwa umeongezeka. Katika michezo minne iliyopita wameshinda michezo yote na kuwa juu ya msimamo, lakini hata pale walikutana na Paul Ndauka wa Ruvu Shooting aliweza kuwatia presha mashabiki wao, lakini ni kocha anayejua nini anatakiwa kufanya kulingana na aina ya mashindano au aina ya mchezo unaokuwa unaikabili timu yake, alibaki jijini  ili kuishuhudia Yanga ikicheza na African Lyon jumapili iliyopita na alisema hivi; “ Yanga si timu ngeni kwangu, lakini si vibaya kuitazama tena ili kuona mambo muhimu. Kama kocha najua nahitaji nini  kwa mchezo mkubwa kama huo’ alisema, Milovan
Kwa upande wa timu ya Yanga inaweza kuwa na kocha wake mkuu, Ernest Brandts katika benchi lake la ufundi endapo watakamilisha taratibu za upatikanaji wa kibali cha kufanyia kazi cha kocha huyo kutoka Uholanzi, vinginevyo itabidi irudie yale yaliyotokea Mei 6 mwaka huu kwa kocha msaidizi Fred Felix Minziro kukaimu nafasi ya ukocha mkuu katika mchezo huo. Brandts ambaye alikuwa kocha wa APR ya Rwanda si mgeni dhidi ya Simba na mara kadhaa ameweza kuifunga akiwa kocha wa timu yake ya zamani ya APR.
Yeye amedai amekiona kikosi cha Yanga wakati wakicheza na Lyon na kukisifia kwa kusema ni timu nzuri lakini zaidi ameomba muda wa kukaa zaidi na timu hiyo ili kutoa kile alichonacho; “ Kwa sasa siwezi kuahidi chochote kuhusiana na mchezo dhidi ya Simba. Lakini ninaimani Yanga ina kikosi kizuri na itafanya vizuri katika mchezo huo. Ugumu?.... Nadhani kila mmoja anatambua ugumu unakuwepo katika michezo mikubwa kama hii, huwa si rahisi kutabirika’ alisema, Brandts
          DONDOO ,MUHIMU
Shomari Kapombe anategemewa sana na mchezo wake ni maridadi sana, anachukuliwa kama mchezaji mwenye kujituma zaidi ndani ya timu hiyo, lakini uwepo wa Amri Kiemba katika nafasi ya kiungo-mlinzi inaweza kumuongea ‘CV’ katika mchezo huo kama Kiemba ataendelea kucheza katika mchezo wake aliouonesha tayari katika michezo iliyopita.
Edward Christopher huyu ni mshambuliaji-mfungaji hatari zaidi anayecheza ligi kuu ya Tanzania Bara , anahitaji michezo mikubwa kama hii ili kujijenga zaidi na kuthibisha ili ninalolisema. Kama atakuwepo uwanjani kwa walau dakika 20 anaweza kufunga bao ama mabao, kila nafasi anayoipata huwa ni hazina kwake na tayari amefunga bao moja katika dakika chache alizocheza.
Sunzu yeye amecheza michezo miwili na kufunga mabao mawili, mpigaji mahiri wa mipira ya vichwa katika ligi ya Bara, tangu aje Tanzania ameweza kuifunga Yanga mara mbili katika michezo mitatu aliyocheza dhidi yao, ANAWEZA KUFUNGA BAO LA KICHWA KAMA ATAKUWA FITI KWANI Yanga hawana uwezo wa kuiondosha mipira ya juu.
Said Bahanunzi bado hajafunga bao lolote lakini mchezo huu unaweza kumrudisha juu kama atatuliza akili yake, maana uwezo mkubwa wa kucheza kama mshambuliaji huru na pia ana uwezo wa kugeuka na kukimbia na mipira na kwenda kufunga.
Haruna Niyonzima anatarajiwa kuonesha uwezo wake lakini kung’ara si kitu kigumu kwake, jibu la Yanga kwa Simba wanayejivunia Haruna Moshi, Niyonzima bado hajaonesha kiwango cha juu msimu huu na hajatengeneza nafasi yoyote ile ya bao lakini siku zote michezo mikubwa ipo kwa ajili ya wachezaji wakubwa na Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji wa hadhi ya juu.
Athuman Idd hata kocha, Brandts anadhani ni mchezaji bora zaidi ndani ya timu yake, Chuji anapenda soka, anapenda kucheza michezo mikubwa kama hii na anapenda ushindi, popote atakapokuwepo Mwinyi Kazimoto, bila shaka Chuji atakuwepo na hapo ndipo tutakaposhuhudia soka la viungo wawili bora wa timu ya taifa ya Tanzania wakionesha dunia namna tulivobarikiwa kuwa na vipaji.
Mfungaji aliyewahi kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja wa mahasimu hao ni Hamis Kilomoni; Alifunga mabao manne mwaka 1964 wakati huo Simba ikifahamika kama Sunderland wakati ikiifunga Yanga mabao 4-0
Jerry Tegete ndiye mchezaji wa mwisho wa Yanga kufunga mabao mawili katika mchezo wa mahasimu hao, alifunga mwaka 2010 mwezi April wakati, Yanga ikilala mabao 4-3
Simba imekuwa na historia ya kuifunga Yanga mabao mengi kwa kila kipindi cha Rais anayeingia madarakani; Iliwahi kuifunga Yanga mabao 6-0 wakati huo Baba wa Taifa, hayatio JK Nyerere akiwa Rais wa Tanzania, pia iliifunga Yanga mabao manne katika kipindi cha Rais wa awamu ya pili ALLY Hassan Mwinyi, kisha wakaifunga mabao 4-1 wakati wa Rais Benjamini Mkapa na tayari Yanga imefungwa mabao 5-0 katika kipindi hiki cha Rais, JK Kikwete.
Abdalah Kibadeni ndiye mchezaji wa mwisho wa timu hizo kufunga hat-trick katika mchezo wa mahasimu hao, alifunga wakati Simba ikiifunga Yanga mabao 6-0
Katika kipindi cha miaka kumi sasa hakuna bao la kujifunga  ambalo limepatikana katika mchezo wa mahasimu hao

1 comment:

  1. Wale wasiojua mwaka 1968 yanga waliwafunga Simba 5 kwa 0 sasa mnasemaje? Mpira kufungana kawaida...yanga wamemchabanga simba mara 36 simba mara 32 tu
    Haya pia yalitakiwa kuwepo kwenye makala yako.
    Balance ya habari haikuwepo umeweka mzee kilomoni sijui wa simba mbona hamna hata mmoja wa Yanga?

    ReplyDelete