Search This Blog

Sunday, September 16, 2012

WIMBO HUU WA YONDANI PREMIER LEAGUE UTAISHA LINI????

 
Na Arone Mpanduka(Radio Tumaini)
 
Ni nyimbo ambazo zilianza tangu mwezi Juni mwaka huu, kipindi ambacho dirisha la usajili kwa timu za ligi kuu ya Tanzania Bara lilikuwa limefunguliwa.
 
Wakati nyimbo hizi zinaanza watu wengi hasa wapenda michezo ukiwemo mchezo wa soka walikuwa wakizipenda sana hasa kutokana na upya wake pamoja na vionjo vyake.
 
Nyimbo hizi hazikuishia hapo kwani ziliendelea kushika hatamu hata baada ya kuanza kwa michuano ya Kagame ambapo mwisho wa siku Yanga iliibuka mbabe baada ya kuichakaza Azam 2-0 katika mchezo wa fainali.
 
Mnamo mwezi Juni mwaka huu ulianza wimbo mtamu wa Kelvin Yondani ambaye ilidaiwa alitoroshwa kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa na kupelekwa kwenye makao makuu ya klabu ya Yanga kwa lengo la kusainishwa mkataba uliokuwa na vionjo vya mamilioni ya pesa.
 
Hali hiyo ilitokea katika wakati ambao watu wanamtambua beki huyo kuwa bado mali ya klabu ya soka ya Simba.
 
Wakati wimbo huo unaendelea kuchana mawimbi, ghafla ukaibuka wimbo mwingine mkali wa Mbuyu Twite ambapo vionjo vya wimbo huu vilipiku vile vya wimbo wa awali hasa kufuatia mchezaji huyu kuwaingiza ‘chaka’ viongozi wa Simba baada ya kuilaghai klabu hiyo na kunyakua fedha za usajili huku akijua fika kwamba alikwishakubaliana na Yanga juu ya kuitumikia timu hiyo.
 
Baadae kidogo ukaja wimbo wa Ramadhan Chombo Redondo, wimbo ambao nao kwa kiasi fulani ulitikisa ingawa haukudumu kwa muda mrefu sana.
 
Baada ya wimbo huu kuchuja sasa ikawa nafasi kubwa kwa nyimbo za Twite na Yondani kuendelea kutesa na kuleta ladha kwenye masikio ya watu ambapo mwisho wa siku wimbo wa Twite ukachuja ghafla na kuacha wimbo wa Yondani ukiendelea kupeta.
 
Ndugu msomaji kusikia habari mbalimbali za wachezaji tofauti tofauti hasa katika misimu ya usajili ni jambo la kawaida sana ambapo hata inapofika msimu wa usajili barani Ulaya kila kukicha huwa tunasikia taarifa tofauti tena za kugeuka geuka juu ya usajili.
 
Lakini hii inategemea na jinsi gani taarifa hizo za usajili zinatokea hasa kulingana na kile ambacho kinafanywa katika usajili huo kitu ambacho ukijaribu kulinganisha na taarifa zetu za ‘kibongo’unagundua kwamba sisi taarifa zetu kila msimu hujawa utata ambao kiuhalisia hufanywa na wahusika wa usajili.
 
Usajili ambao uliweza kuleta mvutano kuanzia mwanzo hadi mwisho ni ule wa Kalvin Yondani pamoja na Mbuyu Twite na kupelekea Kamati ya Sheria, Maadili na hadhi za wachezaji kuketi na kujadili pingamizi zote za usajili wa utata kutoka vilabu mbalimbali.
 
Suala la Mbuyu Twite lilionekana jepesi kwa kuwa Kamati ilibaini kwamba Yanga ilifuata taratibu zote za kumsajili ambapo Yanga nao walikiri kwamba beki wao huyo kutoka klabu ya Lupopo FC aliwadhulumu Simba kiasi cha dola elfu 32 na kuahidi kuzilipa wao kama klabu.
 
Ngoma nzito ilikuwa kwa Yondani ambaye bado uongozi wa Simba umepokea matokeo ya maamuzi ya Kamati kwa manung’uniko hivi na hata kutishia kugomea ligi kuu.
 
 Hii ni baada ya Kamati hiyo kudai kwamba Yanga ilifuata taratibu zote za kumsajili Yondani , kwa hiyo ni mchezaji halani wa wanajangwani hao na Simba ilitakiwa kutumia mamlaka zingine ili kuthibitisha kwamba beki huyo ni mali yao.
 
Labda ndugu msomaji nikukumbushe miaka ya zamani pia ambapo usajili wa utata ulikuwa ukifanyika.
 
Mchezaji Yusufu Bana; Akiwa mchezaji wa Pamba ya Mwanza mwanzoni mwa miaka ya 1980, beki huyo alisaini Simba katika fomu za usajili akitumia jina la Yussuf Ismail.
 
Lakini baadaye Yanga wakamfuata na kumrubuni asaini kwao. Akasaini Jangwani na kutumia jina la Yussuf Bana na Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) chini ya Mwenyekiti wake wa enzi hizo, Said Hamad El Maamry wakamuidhinisha kuchezea Yanga.
 
Mchezaji Charles Boniface Mkwasa; Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga aliyesajiliwa kutoka Tumbaku ya Morogoro, mwanzoni mwa miaka ya 1980, Simba ilimfuata na kumrubuni ahamie kwao.
 
Kiungo Charles Boniface Mkwasa, akakubali na kusaini Simba SC kwa jina la Charles Boniface alilokuwa pia akitumia Yanga na tangu Tumbaku.
 
Lakini Yanga wakamfuata na kumshawishi abaki, na baada ya kukubaliana naye, akasaini kuendelea kuichezea Yanga, safari hii akitumia jina la Charles Boniface Mkwasa.
 
Lakini hii mbele ya FAT ya El Maamry ilidunda na Mkwasa alifungiwa msimu mzima kabla ya kumaliza adhabu yake na kuendelea kucheza Jangwani. 
Mchezaji Ephraim Makoye; Akiwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga aliyesajiliwa kutoka Kagera Stars mwaka 2000 (sasa Kagera Sugar), Simba SC walimfuata na kumrubuni asaini kwao.
 
Makoye, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika sekondari ya Makongo, alichukua fedha za Simba akasaini.
 
Hata hivyo, siku hiyo hiyo Yanga walimnasa na kumchukua hadi kwa viongozi wa Simba kurudisha fedha alizochukua aendelee kuchezea Yanga.
 
Simba waligoma kuchukua fedha na kwa sababu wakati huo FAT ilikuwa haitambui mikataba ya klabu na mchezaji zaidi ya fomu za usajili, ambazo zilikuwa hazijatoka.
 
Makoye aliendelea kuchezea Yanga, ingawa baadaye alichezea Simba alipotemwa Yanga. 
 
Yote kwa yote kitu ambacho tunatakiwa kufanya kwa sasa hasa timu zetu za Simba na Yanga ni kutazama mbele na si kubaki nyuma na kuendelea kulaumiana kwasababu yapo mambo mengi ya kufanya ambapo Simba inakabiliwa na michuano ya ligi kuu sanjari na michuano ya klabu bingwa barani Afrika.
 
Macho na masikio ya watu kwa sasa yamechoka kuona ama kusikia nyimbo za akina Kelvin Yondani ama wachezaji wengine kuendelea kuzungumza na kuwa gumzo wakati dirisha lenyewe la usajili tayari limefungwa.
 
Kitu cha msingi ninachoshauri ni kwamba itumike diplomasia katika kuwekana sawa suala hili ili liweze kupita na hatimaye mambo mengine yaweze kufuata.
 
Nimelitaja sana jina la Yondani kwasababu ndilo jina pekee akwa sasa ambalo kila kukicha bado limekuwa likiendelea kuzungumzwa katika usajili na wakati mwingine kupelekea hata wadau wa michezo kususa kusoma kurasa za michezo za magazeti ama kusikiliza vipindi vya michezo vya redio nah ii inatokana na kwamba wadau kw asasa wanataka kusikia na kushuhudia nini kitatokea kwenye msimu mpya wa ligi kuu hasa baada ya klabu kujinadi kwamba zimejiandaa vya kutosha.
 
 Amani Kwenu  - 0713 896320

1 comment:

  1. wewe na timu yako ya sport extra ndio mnauendeleza huo wimbo, mwenyekitu wenu Rage ameshakubali yaishe lakini washika pembe wa clouds mnakomaliaaaa, nendeni shule mtajua jinsi ya kuingia mikataba na kufuata kanuni sio blah bla tu

    ReplyDelete