Search This Blog

Monday, September 17, 2012

TFF WADHAMINI WA LIGI SIO WAOKOZI - MIKATABA YA UDHAMINI LENGO NI KUVISAIDIA VILABU AU VINGINEVYO ?



TFF, jukumu lenu la kwanza ni kuendeleza mpira wetu hapa Tanzania. Mnajua mpira unapendwa sana hapa Tanzania na mnatambua kwamba wananchi wamewaweka nyie hapo msimamie na kutekeleza mikakati ya kuendeleza mpira wetu.

Mkataba kati ya mdhamini wa miaka iliyopita Vodacom na nyie umeisha mwisho wa msimu uliopita. Inaeleweka kwamba Vodacom walikuwa na nafasi ya kwanza ya kuongeza mkataba na pale pasipokuwa na makubaliano TFF walikuwa na haki ya kutafuta wengineo.

TFF – Kilichowashinda kuweka deadline ya kukubaliana ili muwaalike wengineo ni nini. Mnajianikaje hadharani mpaka dakika hii ya mwisho mkiongea na mdhamini huyo huyo. Mnaviwekaje vilabu vyenu kwenye wakati mgumu wa kushindwa kujipanga kwa sababu mmeshindwa kumdhibiti mdhamini achomoe au abaki.

TFF – Mdhamini anayekuja kwako sio mwokozi, anakuja kama partner na kama partner lazima awe kwenye sura mmoja na wewe kuhusu malengo yako na la muhimu zaidi majukumu yako ambayo ni kukuza mpira wetu hapa.

TFF – Mnatambua timu binafsi zinazoweza kujiendesha kiuhakika ni tatu, Simba, Yanga na Coastal ambao wamebahatika kupata wadhamini. Zilizobaki ni za kibiashara ambazo zinajiendesha zenyewe na jeshi/polisi ambazo nazo zinaweza kujiendesha wenyewe. Kuna timu mbili ambazo bila mdhamini wa uhakika hali ni ngumu. Kwenye ligi ya daraja la kwanza timu za binafsi ziko 15 na zote zikipanda hali itakuwa ni ngumu sana bila mdhamini.

TFF – Hivi kweli mlikuwa mnategemea vilabu visianze maongezi na wadhamini wako mpaka siku moja kabla ya ligi kwa sababu mkataba wa ligi haujulikani utakuwa vipi. Kama Timu imepata mdhamini shindani wa Vodacom kweli mngetaka wasikubaliane chochote mpaka dakika hii ya mwisho. Na ikatokea Vodacom akachomoa, hivi kweli mngetegemea timu ikimbilie tena kwa yule mdhamini wako kuwambia kwa sasa yawezekana. Hilo fungu kweli litakuwa linasubiri?

Sasa wewe utakubalije mdhamini wako (Vodacom) kusema kwamba hizi klabu zilizopo na zile ambazo zinaweza kupanda haziwezi kudhaminiwa na yule mwenye ushindani na yeye. Kweli wewe kama TFF unaona ukikubali kipengele kama hiko kwenye mkataba unasaidia kukuza mpira wetu au unachangia kuudumiza? Na pale ukata unapochanganya mwishoni wa ligi, na hizo timu zikashindwa kufika Kagera kwenye mechi, si mnazitoa kwenye ligi na kuharibu picha nzima ya ligi. Huoni jukumu lako kuu ni kuhakikisha kila timu inaweza kumudu na kushiriki ligi nzima? Hilo najua unalitaka. Sasa itakuwaje ukakubali kipengele cha kwenye mkataba na mdhamini wako wa ligi ambacho kinazuia timu hizo hizi kupata mdhamini ili ziweza kuanza na kumaliza ligi katika hali isio ya utata kifedha?

Vodacom sio mwokozi wako, yeye ni mdhamini ambaye lazima awe kwenye ukurasa mmoja na wewe wa kukuza mpira. Wadhamini waliopo ni hao hao, sio kwenye mpira sio kwenye burudani na maswala mengineo ya msingi, yaani namba yao ni ndogo sana, halafu bado unakubali iwe ndogo zaidi.

Na kwa nyie Vodacom, kama mnapenda maendeleo ya mpira basi tambueni, sio mpaka mle wote sahani mmoja lakini usile sahani peke yako tu, huo mpunga hautavunwa baadae. Mdhamini wa ligi ni mmoja, na kama inalipa kwako basi fanya hivyo. Unadhamini LIGI, acha wengineo wowote wadhamini hizi timu zetu maana zinahitaji wadhamini.

Hivi kweli kwa matatizo tuliyonayo katika kukuza mpira wetu, huwezi ukatambua kwamba tendo lenu hili haliendani kabisa na maendeleo ya mpira hapa Tanzania. Tunaelewa biashara ni mbele na hatuwazuii kwa hilo, tunawapongeza sana sana kwa mafanikio yenu ya kibiashara na tunawatakia mema. Lakini unataka kuniambia kweli kama timu ndogo, ikivaa jezi ambayo mdhamini ni mshindani wako, hilo litakuharibia biashara. Uko tayari kabisa kutodhamini ligi nzima kwa sababu hiyo? Hivi kweli baada ya hapo unaweza ukasema unachangia kwenye kukuza mpira wetu.

Watanzania tunaiona TFF yetu ikiburuzwa kila siku na haya mashirika yetu yanayodhamini hizi Bonanza zetu na ni mchanganyiko wa njaa binafsi pamoja na kutokuwa na skillset za kufanya kazi walizogombania na kuzipata.

Ningemaliza kwa kuwasihi tena Vodacom, muangalie upya hiki kipengele chenu. Hakijakaa vizuri na wapenzi wa mpira kwa sababu kinazuia ukuaji wa mpira wetu hapa Tanzania.

Na ningewaomba tena TFF, msiburuzwe ovyo ovyo na msijijengee shimo ambalo mnashindwa kutoka. Hilo shimo mmelijenga mapema sana mliposhindwa kusimamia deadline ya kuafikiana kabla ya kutoa tangazo rasmi kwa wadhamini wengineo kuja mbele.

Mkataba mpya ulikuwa unatakiwa uwe umeshapitishwa hata kabla ya ligi ya msimu uliopita kuisha la sivyo TFF wewe ni kama free agent, mwaka wa mwisho lazima uanze kuongea na highest bidder kama waliopo wanasuasua. Ndio inavyofanyika kote duniani, sio mifano ya kutafuta ipo tu hadharani.

No comments:

Post a Comment