Search This Blog

Friday, August 3, 2012

AZAM: 12 WAMEOMBA KAZI YA UKOCHA - HATUKUMFUKUZA STEWART HALL

Uongozi wa klabu ya Azam umesema tayari imepokea maombi ya makocha  12 wanaowania nafasi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo.Maombi ya makocha hayo yanatokana na uamuzi wa hivi karibuni uliotangazwa na uongozi wa klabu ya Azam wa kusitisha mkataba wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Stewart Hall.

Baada ya kutangazwa kuondolewa kikosini, klabu hiyo ilimtangaza kocha wa muda, Vivek Nagul raia wa India atakayesaidiana na Kalli Ongala.

Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed alisema kuwa miongoni mwa maombi yaliyopokelewa ni ya makocha wazawa na mengine ni ya makocha kutoka nje ya nchi.

"Kikubwa ni kwamba tumepokea maombi ya makocha 12 mpaka sasa miongoni mwao ni  wazawa na wengine kutoka nje ya nchi,".alisema Mohamed.

Hata hivyo, Mohamed hakuwa tayari kutaja majina ya makocha wala  nchi wanazotoka kwa madai kwamba bado wanafanya upembuzi yakinifu na muda si mrefu wataweka bayana.

Aliongeza kuwa, vigezo vitakavyotumika katika kumpata kocha wao mpya ni rekodi zake katika kufundisha soka na si vinginevyo.

Wakati huu huo, Mohamed amekanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa klabu yake imemtimua  Hall baada ya kumpanga Winga Mrisho Ngasa katika pambano dhidi ya Yanga.

"Niweke wazi kwamba uongozi wangu unafanya kazi kwa kuzingatia ushauri  wa benchi la ufundi ,hakuna tuhuma zozote zilizoletwa kwetu zinazomhusu  Ngassa, sasa kwanini tumfukuze kocha, huo ni uzushi tu. 


Kukanusha huku kwa Azam kwamba walimfukuza Stewart kunakuja siku mbili baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kwambakocha huyo alitimuliwa baada ya kumpanga Ngassa kwenye fainali japokuwa likatazwa kufanya hivyo na uongozi wa AZAM FC.

No comments:

Post a Comment