*Akutanishwa na mwanamke aliyemakatwa na madawa
*Amueleza kisa ni askari aliyemtongoza, akakataa
*Yanga waahidi kumsaidia, ila wampa kazi ya kufanya
Na Saleh Ally
WIKI ILIYOPITA, tuliishia sehemu Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ akiwa chini ya ulinzi wa polisi maalum wa kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya. Walitaka waanze kumpekua, akaubali na mara moja wakaanza kufanya hivyo huku akiwa amekodoa jicho kwa umakini mkubwa. Itakuwaje baada ya hapo? Endelea.
POLISI waliendelea kupekua mizigo yangu nami nikawaangalia kwa umakini mkubwa, walivyofanya hivyo wakifungua begi moja baada ya jingine. Hawakukuta kitu chochote, nikashukuru sana Mungu.
Bado niliendelea kutoamini kilichokuwa kinatokea, niliona kama sinema inaendelea. Nikaendelea kuwauliza kuwa walichokuwa wananiambia kama ni kweli. Kilichonishangaza ni kusema yule dada ameshikwa na madawa ya kulevya.
Ule mzigo ambao alipewa na yule jamaa kule Afrika Kusini niliuona, ulikuwa umefungwa vizuri sana. Uliandikwa jina la mtu husika aliyetakiwa aupokee pamoja na namba yake ya simu. Sasa inawezekana vipi madawa ya kulevya mtu ajiandike jina na namba ya simu.
Mmoja wa maaskari akaniambia wanaohusika na madawa ya kulevya wanakuwa wajanja sana, wanaweza wakafanya lolote kumlaghai mtu. Lakini baadhi walionekana kutoniamini, walishangazwa na mimi kuhusika na biashara hiyo wakati mambo yangu yalishakuwa mazuri, maana nilishapata timu na nilikuwa nacheza.
Nilitamani kulia labda wakiyaona machozi yangu wangeweza kunielewa, kwamba sikuwa nahusika wala sikujua kitu chochote. Nikawaomba wanisaidie kukutana na yule dada angalau nizungumze naye hata kidogo kujua kilichokuwa kinaendelea, maana niliona kila kitu kama sinema inayorekodiwa.
Ilikuwa kazi sana wale askari kunikubalia, niliendelea kuwaomba. Baadaye kwa kuwa baadhi walionekana kunionea huruma, waliahidi kunisaidia. Usiku yule dada aliletwa nilipokuwa na nilianza kuzungumza naye nikitaka kujua kilichotokea.
Aliponiona alianza kulia, alijua wazi hata mimi sikumjua yule mtu. Alinieleza namna mambo yalivyokwenda, alisema baada ya kuingia kwenye ndege. Kweli yule mtu alisema anafanya kazi shirika la ndege la hapa nyumbani, alipanda hadi kwenye ndege na kumpa ule mzigo, naye akauweka kwenye sehemu maalum ya kuwekea mizigo.
Ndege haikuwa na watu wengi sana, wakiwa angani kuna mwanaume mmoja aliyejitambulisha kuwa yeye ni askari polisi kwa ajili ya usalama wa ndege alimfuata na kuanza kumtongoza. Hata hivyo, dada naye akamtolea nje kwa kuwa hakutaka kuwa naye.
Baada ya kuona amekataliwa, yule askari alianza kuzungumza maneno ya shombo na kumueleza atakiona kwa kuwa ameona akikabidhiwa mzigo ambao anajua lazima utakuwa na madawa ya kulevya. Hali hiyo ilimshitua huyo dada, ndege ilipotua akaona haitakuwa salama kwake kuubeba ule mzigo, akaona auache kwenye ndege.
Yule askari alishashuka mapema na kwenda kuripoti kuhusiana na mzigo huo, hivyo wakati anatoka alikamatwa na kuanza kupekuliwa, hawakumkuta na kitu. Basi yule askari akawaongoza maskari wengine wakaingia hadi ndani kwenye ndege kwenda kupekua na kweli wakafanikiwa kuupata ule mzigo na ulipofunguliwa, ukakutwa na madawa ya kulevya.
Niliendelea kumsikiliza kama vile nilikuwa ndotoni, kila kitu kwangu hakikwenda sawa. Bado sikuamini kwamba nimesharejea Dar halafu usiku ule nilikuwa pale airport, tena ninashikiliwa na kwa tuhuma za kuhusika na madawa ya kulevya!
Baada ya kuzungumza na yule dada, kwa kuwa wale askari walinisaidia tu, basi akarudishwa sehemu aliyokuwa amefungiwa. Hivyo mimi nikatakiwa kusubiri hadi kesho yake kwa ajili ya mahojiano maalum kuhusiana na suala hilo. Bado sikuwa nikiamini kilichokuwa kinaendelea.
Asubuhi wale jamaa waliniweka kati tena, mahojiano yaliendelea kwa zaidi ya saa tano. Walinihoji kutaka kujua kila kitu, sikutaka kuficha kitu, nilieleza kila nilichokijua. Ingawa niliona kama suala hilo huenda lingeisha kilahisi lakini baadaye niliona mambo yamebadilika.
Ugumu nilianza kuuona, nilichanganyikiwa kutokana na hali ilivyokuwa. Kwani nilipata taarifa kuwa kwenye vyombo vya habari ilisharipotiwa kwamba nilikamatwa na madawa ya kulevya. Ugumu ukazidi kuongezeka, nikachanganyikiwa.
Nilipata faraja kidogo kwa kuwa siku hiyo angalau nilipata nafasi ya kuzungumza na ndugu zangu ambao siku iliyopita walikataliwa kuniona. Niliwaeleza kila kitu na kuwathibitishia sikuwa ninahusikia na kitu chochote. Wakaahidi kuanza kunisaidia.
Pamoja na wao, watu wa Yanga walikuwa wamefanikiwa kuniona na nikawaeleza kila kitu kuhusiana na mambo yalivyokwenda hadi kufikia hapo. Nao wakaahidi kunisaidia ikiwa ni pamoja na kuniwekea wanasheria lakini walitaka kuna kitu nikitekeleze ili wanisaidie.
Nilitaka kujua haraka kuhusiana na kitu hicho lakini haikuwezekana wakati huo, wakanitaka kutokuwa na haraka kuhusiana na hilo. Wakaniambia tukapokuwa tumetulia watanieleza kila kitu ili niweze kutekeleza kitu hicho, nao watoe msaada wao.
Siku hiyo ikapita na siku iliyofuata nikachukuliwa pamoja na yule dada, tukapandishwa kwenye gari aina ya Toyota Rav4 pamoja na askari wanne, tukaanza safari ya kwenda Mahakamani ya Kisutu. Bado niliona kama hadithi kwa kila kilichokuwa kinaendelea.
Tukiwa njiani, kwa mara ya kwanza niliiona tena Dar es Salaam. Kilichoniumiza sikuwa huru tena hata kushuka kwenye gari na kuendelea na shughuli zangu. Bado niliendelea kuona mambo kama hayako vizuri lakini yanaendelea ndotoni.
Tuliwasili Mahakama ya Kisutu na kukuta watu wengi sana wakiwemo wana habari ambao walikuwa na hamu kubwa ya kufuatilia kesi yangu ya kukamatatwa na madawa ya kulevya ambayo wakati huo tayari ilikuwa ni gumzo nchi nzima.
MALIMA akiwa chini ya ulinzi amewasili kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, anasubiriwa kwa hamu. Huenda ambao walikuwa hawajaamini taarifa za vyombo vya habari wanataka kumshuhudia ‘live’ akipandishwa kizimbani. Je, nini kitafuatia? Endelea.
Looking forward for the next episode........
ReplyDeleteMdau
Mike